Wasanii wa Tanzania bado hawajatambulika ipasavyo

Muktasari:
- Kama zilivyo nchi nyingine, tasnia ya muziki hapa kwetu ina washiriki wa aina mbalimbali wakiwemo wanamuziki, mameneja wao, watayarishaji wa kazi za muziki, maarufu kama ‘maproducer’, ma promoter, wasambazaji wa kazi za sanaa, mafundi mitambo, wenye kumbi za muziki, wenye bendi, watumiaji wa kazi za muziki na wengine wengi.
Siku chache zijazo itasomwa bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba niwakumbushe wawakilishi wa wananchi kuwa tulio chini ya wizara hii tuna mengi sana ya kusema, lakini pa kusemea ndio pagumu.
Mheshimiwa mbunge mara ya mwisho umeongea na wasanii wa jimbo lako ni lini?
Kama zilivyo nchi nyingine, tasnia ya muziki hapa kwetu ina washiriki wa aina mbalimbali wakiwemo wanamuziki, mameneja wao, watayarishaji wa kazi za muziki, maarufu kama ‘maproducer’, ma promoter, wasambazaji wa kazi za sanaa, mafundi mitambo, wenye kumbi za muziki, wenye bendi, watumiaji wa kazi za muziki na wengine wengi. Hali hii imewezesha watu wengi kutamka kuwa tasnia imekua.
Kukua huku hutolewa mifano ya mafanikio yaliyofikiwa na wasanii kama Diamond Platnumz, Ali Kiba,Harmonize na wengineo waliofanikiwa kifedha na kupata majina makubwa Kitaifa na Kimataifa katika tasnia hii. Lakini kuna tofauti kubwa nyingi kati ya tasnia ya utamaduni na sanaa hapa nchini na tasnia za aina yake nchi nyingine.
Pamoja na kuweko kwa wadau wengi kama nilivyotaja hapo juu, maamuzi ya muelekeo wa tasnia yako katika mikono ya watu wachache sana. Ukiingia katika tasnia hii, ili ufanikiwe ni lazima paweko na mkono wa mmoja wa hawa watawala wa tasnia hii.
Ukicheza nje ya himaya ya waamuzi hawa, uwezekano wa mafanikio katika tasnia hii ni mdogo sana au wa muda mfupi sana. Ili kufanikiwa katika tasnia ya muziki ni lazima uweke mguu mmoja Dar es Salaam au kuhamia kabisa katika jiji hili, kwa hali hii unaweza kudhania kuwa wasanii wazuri wanatoka Dar es Salaam tu, jambo ambalo kwa vyovyote si la kweli.
Kwa hili labda nirudie neno ambalo niliwahi kuandika wiki chache zilizopita, huwa inashangaza jinsi wawakilishi wa wananchi, yaani Waheshimiwa Wabunge, wanavyolichukulia swala la wasanii, ni nadra kusikia Mbunge akidai haki zozote kwa ajili ya wasanii wa jimbo lake, japo mara nyingi tumesikia wawakilishi hawa wakitetea maslahi ya wasanii maarufu wanaoishi Dar es Salaam, nini kinawafanya wasiamini kuwa wanaweza kupata wasanii maarufu kutoka katika majimbo yao? Kwanini hawadai miundombinu ya sanaa kutengenezwa katika majimbo yao?
Nalazimika hapa kuwapa hongera wabunge ambao wameanzisha matamasha ya muziki wa asili katika majimbo yao, japo ingekuwa vizuri zaidi matamasha yasiishie kwa wasanii hawa kuonyesha tu umahiri wao katika matamasha hayo tu, lakini ingekuwa vizuri kuwatafutia nafasi za kushiriki katika matamasha ya kimataifa, kuwaelimisha jinsi ya kupata haki zao.
Kwa mfano karibu kila wilaya iliyokuweko enzi za mkoloni ilikuwa na ukumbi wa umma, Community Center, ambapo wasanii wengi wa zamani ndiko walikokuwa wanaonyesha kazi zao za sanaa. Muziki wa dansi, kwaya, taarab, na sanaa mbalimbali za maonyesho.
Tofauti nyingine ya tasnia yetu na za wenzetu hata wale majirani ni ukosefu wa elimu ya msingi ya shughuli mbalimbali za tasnia. Wanamuziki, mameneja , maproducer, mapromoter, na kadhalika karibu wote wamejifunzia ujuzi mtaani. Ukimtafuta meneja umuulize kuhusu haki za msanii wake hazijui, hata haki zake mwenyewe hazijui.
Wanamuziki wengi hutamka kuwa wanataka kuingia katika soko la kimataifa lakini hata njia ya kufika huko hawaijui, mengi ya mapungufu haya ni kutokana na kukosa elimu rasmi ya shughuli zao.
Tanzania ina miongozo rasmi ya ufundishaji wa sanaa, inayoongiza kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita, lakini haitekelezwi, vyuo vya waalimu wa sanaa kama vile Chuo Cha Ualimu Butimba vimepotea, hivyo watoto wa Kitanzania wananyimwa haki ya sehemu muhimu ya elimu.
Ni jambo la ajabu kuwa wale wenye uwezo hupeleka watoto wao kwenye shule za kulipia ambako sanaa ni moja ya somo muhimu, na hujisifu sana watoto wao wanapoweza kumudu kupiga piano au gitaa, au kuchora na kadhalika, sasa swali kwanini hawataki elimu hii isambae kwa kila mtoto nchini?
Kiini macho ni kuwa pamoja na kuwa hakuna elimu ya awali ya sanaa, jambo la ajabu ni kuwa vyuo vikuu vina Idara zinayowezesha watu kupata Shahada ya Sanaa, unapataje digrii ya somo ambalo huna msingi nalo? Kimsingi tasnia inaendeshwa kiujanja ujanja, na katika ulimwengu wa leo shughuli za kiujanja ujanja haziwezi kufikisha tasnia kuwa na uwezo wa kuhimili mashindano yaliyoko katika soko la kimataifa, na ndio maana unaona kazi za wanamuziki wetu zikiwa kama kivuli cha kazi za wanamuziki wa mataifa mengine, kuna wanamuziki kazi yao kubwa ni kuiga kila litakalofanywa na wanamuziki wa Kongo, wengine huiga kila linalofanywa na wanamuziki wa Nigeria, wengine wakiegamia Afrika ya Kusini, kama vile hatuna mbegu ya kuanzisha kilicho chetu na kukifikisha kwenye uso wa ulimwengu.
Lakini mnyonge mnyongeni, japokuwa singeli inatuheshimisha katika tasnia ya muziki duniani.Wakati umefika kwa wasanii wenye busara kukaa chini na kuangalia wapi tulikotoka na wapi tunakwenda, na kutoa ushauri kwa serikali, kwani kutokana na mfumo wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, uwezekano wa Wizara kuanzisha mada hii ni mdogo.