Tryphon: Hauwezi kuwa mwalimu wa muziki kama siyo msanii

Muktasari:
- Akizungumza na Mwananchi Tryphon amesema moja ya kigezo ambacho mtu nayetaka kuwa mwalimu wa muziki anatakiwa kukizingatia ni kuhakikisha kuwa yeye ni mwanamuziki.
Zanzibar. Mwanamuziki na mwalimu wa sanaa katika Chuo cha Muziki DSMA (The Dao Country Music Accademy) kutoka Zanzibar, Tryphon Evarist amesema ili mtu awe mwalimu wa muziki lazima awe msanii.
Akizungumza na Mwananchi Tryphon amesema moja ya kigezo ambacho mtu nayetaka kuwa mwalimu wa muziki anatakiwa kukizingatia ni kuhakikisha kuwa yeye ni mwanamuziki.

"Uzuri sisi kwenye chuo chetu walimu takribani wote ni wale ambao walihitimu kwahiyo unakuta mimi nilipomaliza miaka minne kusoma, mwaka wa tano nikaanza kupewa training hapo hapo ya kupata uzoefu wa ufundishaji kwa hiyo tangu nimekuwa mwalimu ninamiaka kama sita ya kufundisha,”amesema.
Akizungumzia kuhusu muziki wa Taarab amesema, asili yake ni Zanzibar licha ya kuwa uliletwa na watawala.
“Taarab asilia yake ni Zanzibar watu waliupokea kutoka kwa watawala wa Kiarab kwenye miaka ya 1870, lakini sasa hivi unavyopigwa sivyo vile ambavyo walipokea. Kwa hiyo baada ya watu kuchanganya na vitu vyao wakakubali kwamba hii iwe sehemu ya muziki ya utamaduni ya Zanzibar ndipo watu wakaupiga kwa zaidi ya miaka 100,".

Amesema kawaida taarab huwa na misingi yake kama vile mashairi, melodi na kinjia.
“Taarab hasa huwa haiweki kila kitu wazi hata kama utakuwa wimbo wa mapenzi haitumii ukali sana wa maneno. Ni kweli taarab inatumia lugha ya mafumbo hilo hatuwezi kulikataa,” amesema mwalimu huyo.
Akizungumzia mwenendo wa biashara ya muziki huo amesema zamani ulifanya vizuri kutoka na uchache wa aina ya miziki iliyokuwa inapigwa tofauti na sasa.
“Tunajiongopea sitaki nilaumu, lakini w azee wamefanya kazi yao kwa namna ambayo walivyofanya. Na kwa kipindi hiko labda pengine aina za miziki haikuwa mingi ilibidi hata baadhi ya media zicheze hivyo vitu. Ambavyo vipo karibu lakini sasa hivi kuna miziki ya aina tofauti tofauti kwa hiyo watu wanaangalia tupeperushe twende na upepo upi.

"Wazee walikuwa hawana hiyo nguvu wao walikuwa wanafanya, muziki kwa kujifurahisha lakini kizazi cha sasa ndiyo tunaweza kusema kupitia muziki tunapata manufaa,"amemalizia.