Shilole apata ajali akitoka kushiriki 'Pilau Day' Kigoma
Muktasari:
- Msanii Shilole amehamishiwa jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi kufuatia ajali aliyopata baada ya gari alilokuwa akisafiria kugonga ng’ombe.
Tabora. Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Zuwena Mohamedi maarufu kama Shilole, amepata ajali ya gari na kulazimika kuhamishiwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi.
Mwananchi ilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philemon Makungu, majira ya saa tisa na dakika 45 alasiri, ili kupata ufafanuzi zaidi kuhusu ajali hiyo iliyotokea usiku wa kumakia Januari 3, 2026.
Hata hivyo, Makungu alisema kuwa wakati huo hakuwa na taarifa rasmi kuhusiana na tukio hilo na kueleza kwamba anahitaji kulifuatilia kwa kina tukio hilo kabla ya kutoa maelezo ya kina kwa umma.
“Sina taarifa ya kwamba kuna ajali imetokea ikimuhusisha msanii Shilole, lakini ngoja nifuatilie niweze kujua,“ amesema.
Dakika 40 baadaye Mwananchi ilimrejea tena Makungu, kwa ajili ya kufahamu maendeleo ya uchunguzi wa ajali hiyo.
Makungu amesema kuwa bado hakuwa amepata taarifa za kina kuhusiana na tukio hilo, akieleza kuwa anaendelea kulifuatilia ili kupata undani wake kabla ya kutoa maelezo rasmi kwa umma.
“Bado sijaipata naendeleo kuifatilia nijue undani wake vizuri ila kwa sasa bado sijafanikiwa kuipata sawa sawa,” amesema.
Shilole amepata ajali hiyo usiku wa kuamkia Januari 3, 2025, akiwa safarini kutoka mkoani Kigoma alikoshiriki hafla ya Pilau Day iliyoandaliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus maarufu Baba Levo.
Msanii huyo akiwa na dereva wake walipofika eneo la Malagarasi mkoani Kigoma, umbali mfupi kabla ya kuingia Mkoa wa Tabora, gari walilokuwa wakitumia liligonga ng’ombe aliyekuwa barabarani.
Akizungumza na Mwananchi, Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus maarufu Baba Levo, amesema Shilole alipata ajali hiyo akiwa ametokea mkoani Kigoma, jimboni kwake, alikokwenda kushiriki tafrija maalumu aliyoiandaa mbunge huyo iitwayo Pilau Day.
“Ametoka hapa jimboni kwangu akiwa salama kabisa wakiwa na dereva wake na gari yao aina ya Alphard wakaanza safari nashangaa usiku wananimbia wamepata ajali na Shilole amepata mshtuko na ana maumivu,” amesema Baba Levo.
Baba Levo ameeleza kuwa gari walilokuwa wakisafiria liliyumba baada ya kugonga ng’ombe aliyekuwa mkubwa, jambo lililosababisha kutoka nje ya barabara ingawa halikuanguka.
Amesema tukio hilo liliwatia hofu lakini dereva aliweza kulidhibiti.
Baba Levo ameongeza kuwa jitihada zilifanyika kuwahi Uwanja wa Ndege wa Tabora ili Shilole asafirishwe haraka kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu, lakini hazikufanikiwa kutokana na kukosa safari ya ndege siku hiyo ya Januari 3.
Kutokana na changamoto hiyo, walilazimika kuendelea na safari ya barabara hadi mkoani Dodoma ambako alipata ndege ya kuelekea Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
“Uwanja wa ndege Tabora tulikosa ndege ya kuondoka leo na kwamba ndege ni mpaka siku ya Jumanne, ikalazimu sasa kuchukua gari mpaka Dodoma ili kupanda ndege na kuwahi Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu na kweli ana maumivu,” amesema.