Matovolwa: Mimi handsome kuliko wao

Muktasari:
- Achana na yule Pepe Kalle jitu la miraba minne kutoka Congo, au Osama Bin Laden mwenye ndevu nyingi. Huyu ni Lumole Mtovolwa ‘Kobisi’ mwigizaji wa Bongo Movie ambaye wengi huvutiwa na mikogo yake kwenye runinga huku mwonekano wake ukigeuka kivutio kikubwa.
Dar es Salaam. Unaweza kumuita jitu la miraba minne, bonge la bwana au kibonge mwepesi kutokana na mwonekano wake. Mwili menene, amepanda hewani huku uso wake ukiwa na ndevu nyingi.
Achana na yule Pepe Kalle jitu la miraba minne kutoka Congo, au Osama Bin Laden mwenye ndevu nyingi. Huyu ni Lumole Mtovolwa ‘Kobisi’ mwigizaji wa Bongo Movie ambaye wengi huvutiwa na mikogo yake kwenye runinga huku mwonekano wake ukigeuka kivutio kikubwa.

Hakika katika hili tunaweza kusema jicho la marehemu mwongozaji wa filamu George Otieno ‘Tyson’ halikumtazama kwa wasiwasi kwani ndiye mtu wa kwanza kupagawa na mwonekano wa Matovolwa hadi kupelekea amvute na kumsogeza zaidi kwenye macho ya wapenzi wa filamu.
“2000 kulikuwa na tamasha la chuo cha Splendid lilikuwa linafanyika kila mwaka. Kulikuwa na vikundi vingi hadi ambavyo vipo kwenye Tv walikuwa wanafanya maigizo bahati nzuri na mimi kundi langu la Mwananyamala Arts lilishiriki lakini kwenye mchezo mimi nilikuwa kama director (mwongozaji).
“Nilikuwa nimesimama mbele najaribu kuwaongoza wenzangu ndipo George Otieno ‘Tyson’ aliniona. Akasema huyu jamaa ananifaa, basi akamtuma jamaa anaitwa Saimon akanichukua tukazungumza nikaenda kwenye kikundi chao akaniambia anataka nizibe nafasi ya JB. Nikamwambia hapana siwezi kuziba nafasi yake mimi nitasimama kama mimi,” anasema.
Anasema kwa kipindi hicho waigizaji wanene walikuwa wachache. “Sasa hivi wanene wengi, watu wanakula sana machipsi, watu maarufu wanene kipindi hicho alikuwa JB, Mashaka Matongo ‘ Abiola’ nilivyoongezeka na mimi tukawa watatu. Siwezi kusema kwamba sitapungua kwa sababu ni sehemu ya ajira yangu, ukipungua sana ni tatizo na ukizidi sana ni tatizo.

“Siwezi kusema nifanye diet nishuke mpaka kufikia kilo 80 ni ngumu sana. Ila naweza kuzidi sana na kushuka nikishuka sana madairekta wengi wanasema aaah big! tumekuzoea katika mwonekano ule, maneno yanakuwepo lakini ninachoangalia ni afya yangu pia,” anasema.
Ile kauli ya bonge la bwana inakuja kuthibitishwa na kilo za mwigizaji huyo ambapo analiambia gazeti hili kuwa mara ya mwisho kupima alikuwa amefikisha Kg 180
“Mwili wangu haunisumbui, kwa sababu mimi ndiyo nauongoza kama mtakumbuka nilicheza sinema inaitwa ‘Komando Yoso’ kule nilikuwa nakimbia sana. Sasa unaweza kujiuliza, mpaka kuna watu wakasema ni ‘editing’,” anasema Matovolwa “Mimi handsome”
Utakumbuka Matovolwa ndiyo ‘video king’ kwenye wimbo wa Bahati Bukuku ‘Kampeni’ uliotoka miaka kumi iliyopita. Hata hivyo, licha ya wimbo huo kutoka miaka mingi nyuma hivi sasa umechukua usikivu upya na kusababisha baadhi ya watu kupingana na Bahati Bukuku juu ya mashairi aliyoimba wakiyalinganisha na mwonekano wa Matovolwa.
“Alikuwepo baba jina lake Tupatupa , alikuwa tajiri tena mwenye sura nzuri,”aliimba Bahati kwenye wimbo wake Kampeni.
“Ubishi wa watu wengi unaibuka katika huo mstari wa sura nzuri.”

Lakini waswahili wanasema muhimu kujikubali. Hivyo basi akiwajibu wanaodai sura yake siyo nzuri, Matovyolwa anasema yeye ni ‘handsome’ tofauti na watu wanavyomuangalia.
“Bahati alinifuata akaniambia anataka tufanye video ya gospo kwa sababu hapo nyuma nilikuwa nimeshafanya na Frola Mbasha. Nikamuuliza wimbo upoje akanielezea, sasa kwani hakukuwa na ‘ma-handsome’ zaidi yangu mpaka anichague.
“Mimi ndiyo handsome kuliko waliokuwepo. Ule wimbo wa siku nyingi lakini hiki kizazi cha sasahivi ndiyo kinasema, oooh Bahati katupiga huyo siyo handsome wananikosea mimi ni handsome sana tu au wanataka mpaka nijichubue, nichonge nyusi na nilambe midomo,”anasema.
Kinachoendelea kwenye Kombolela
Mbali na hayo Matovolwa ni kati ya waigizaji wanaocheza kwenye tamthilia ya Kombolela huku wengi wakivutiwa na uhusika wake aliouvaa kama kijana mzembe katika maisha, anayetoka kwenye familia ya Kiswahili.
“Kombolela ni tamthilia ya Taifa tulipopita msimu wa kwanza watu walipenda sana, muda ulivyoisha watazamaji wakalalamika mimi nilimwambia mkuu wa chaneli ile uhitaji wa nje bado mkubwa lakini yule bibie akasema acha iishe.
“Lakini ghafla bin vuu akapita Abdul (Mzalishaji wa Kombolela) akasema ameitwa wanataka warudishe Kombolela wakaweka bajeti tukaanza kazi ilikuwa tuanze Desemba lakini Sofia akasema tuanza Novemba.
“Familia ya mzee Kikala ni bora sana kwa sababu yale ni maisha ambayo sisi waswahili na watu wa hali ya chini tunaishi. Baba anataka aone watoto wake wote na ukiangalia nchi za Kiarabu wanaishi hivyo, mtu atakulia nyumbani ni kama mzee wetu Kikala tatizo kilichozidi ni maneno mengi na ukorofi,” anasema.
Anasema kinachoendelea kwenye tamthilia hiyo hata yeye amewahi kukipitia kipindi anajitafuta kimaisha.
“Hata mimi nimesharudi nyumbani sana naenda napanga pesa ikiisha narudi namuuliza bibi mkubwa kile chumba changu si kipo. Hiyo ndiyo hali halisi. Kwenye tamthilia niliuza nyumba kutokana na mapenzi, kuna watu wanapenda mpaka wanapitiliza.
“Ngoja niwape stori ya uhalisia wangu kabla sijaoa nilikuwa nafanya vitu viwili nikiwa na mtu naangalia tabia zake huyu ataweza kuishi na mama yangu. Kwa sababu anavitu vidogo vidogo vingi hapendi, nilikuwa nikiona tutashindwana nampotezea.

“Siku nilipopata huyu mke wangu nilimwambia mama nimepata mke nataka kuoa. Huu ni mwaka wa 15 sijapata malalamiko kutoka kwa mama yangu,”anasema
Licha ya kuigiza katika tamthilia hiyo kama kijana mzembe, mwigizaji huyo anasema maisha ya Kobisi katika tamthilia ya Kombolela hayana uhalisia na maisha yake binafsi.
“Mimi ni mcheshi lakini siyo mzembe kama Kobisi. Kuna mama nilikutana naye aliniambia anavyoniona kwenye maigizo ni tofauti na anavyoniona kwenye uhalisia. Maigizo yatabaki kuwa maigizo, ndiyo maana leo waigizaji wengi wanasema wao ni mastaa wanaigiza maisha mimi naweza kupanda daladala lakini kuna waigizaji hawawezi.
“Siyo kwamba sina hela ya kuchukua gari binafsi hapana, ninapenda kukutana na mashabiki wangu wanijue tufurahi pamoja. Mimi nikipanda tu hata kwenye daladala utasikia abiria wanaanza kucheka hivyo ndivyo inatakiwa yaani maisha ya kwenye video yabaki huko,”anasema.