Mabantu: Mambo bado kabisa

Mwanzoni mwa mwaka 2023 Mabantu walikaa kimya bila kuachia ngoma yoyote. Ukimya wao waliuvunja miezi kumi iliyopita, baada ya kudondosha Ep yao iliyoitwa ‘University’, ikiwa na ngoma nane ambazo ziliwarudisha tena kwenye chati.
Kati ya ngoma zilizofanya vizuri kutoka kwenye Ep hiyo ni ‘Muhuni’ ambayo kwenye mtandao wa YouTube ina watazamaji 267k, ‘Shemeji’ 719k. Mwaka 2024 wameuanza kwa pini jingine liitwalo ‘Mali Safi’ 60k, nyimbo hizi zote zinachangia kwa kiasi kikubwa Mabantu kusimama tena kwenye gemu.
Mashabiki wengi wamekuwa wakiwachukulia Mabantu kama makundi mengine lakini utofauti wa wasanii hawa ni ndugu ambao hawakujuana mpaka pale walipokutana kwenye taasisi ya kuibua vipaji inayomilikiwa na Said Fella.
Kwa mashabiki wa Bongo fleva jina Mabantu siyo geni masikio mwao, kundi hili linaundwa na wasanii wawili, Twaha Kanengo (Twaha Mabantu - Julai 9, 1997) na Mwarami Kajonje (Muuh Mabantu - Januari 21, 1999).
Kundi hili lilianza safari ya muziki kwa ‘Mkubwa na Wanae’ zaidi ya miaka 11 iliyopita baada ya wakali hawa kukutana kwenye taasisi hiyo yenye lengo la kusaidia na kuibua vipaji mitaani.
Safari ya Mabantu inaanza baada ya wasanii hawa kuacha shule, Muuh aliacha akiwa kidato cha pili huku Twaha akiwa darasa la saba. Kabla hawajakutana, Muuh alikuwa ndiye wa kwanza kuingia ‘Mkubwa na Wanae’ mwaka 2011.
Wakati huo Twaha alikuwa Mbagala kama ombaomba huku akilala kwenye vituo vya mabasi, hadi alipopata habari kuhusu maadhimisho ya miaka saba ya Tanzania house of Talent (THT), Desemba 11, 2012 ndipo habari hiyo aliitumia kama tiketi ya kufikia malengo yake.
“Muuh alikuja mwaka mmoja kabla yangu, aliingia 2011 na mimi niliingia 2012. Kipindi hicho nilisikia habari za THT wakisherehekea kutimiza miaka saba. Muuh na Aslay walikuwa wakitumbuiza wakati huo, niliwaomba waandaaji na mimi nipande jukwaani, niliruhusiwa na hiyo ndiyo ilikuwa ‘tiketi yangu’,” anaeleza Twaha.
Baada ya kufika ‘Mkubwa na Wanae’, Muuh na Twaha walianza kuimba pamoja, hiyo ilitokana na umri wao kupishana kidogo. Kulingana na Muuh, wakati huo wasanii wengi walikuwa wakubwa kuliko yeye.
“Urafiki wetu ulianza baada ya Twaha kuchaguliwa kuwa sehemu ya Mkubwa na Wanae. Urafiki kati yetu ulikua kwa kasi kwa sababu tulikuwa katika umri sawa, kutoka hapo tumekuwa marafiki wakubwa na tunashiriki kila kitu tulichonacho,” anasema Muuh.
Wakiwa katika kituo cha Fella walipata fursa ya kushiriki mazoezi mbalimbali ya kuwaondolea hofu mbele ya watazamaji na matumizi ya vifaa vya sauti na ala za muziki.
Hata hivyo, mbali na kuwa marafiki wakubwa, Muuh anasimulia kuwa marehemu baba yake alipotembelea kwenye taasisi hiyo kwa ajili ya kumpatia mahitaji, aligundua kuwa yeye na Twaha ni ndugu.
“Ilikuwa ni siku ya kutembeleana, nakumbuka marehemu baba yangu alinitembelea kuniletea nguo na pesa, wakati namtambulisha, Twaha alianza kumsimulia baba maisha yake, alitaja jina ambalo baba alikuwa akilifahamu, na kutoka hapo alituambia kuwa tuna uhusiano wa kindugu,” anasema Muuh.
Mnamo 2013, wawili hao walihitimu mafunzo ya muziki na kuamua kuishi pamoja, ndipo walikuja na jina la Mabantu. Kwa kuanza walijaribu kupata nafasi kwenye studio mbalimbali ili waweze kuonesha mashabiki uwezo wao kwenye muziki.
Wanasema msanii chipukizi kupata studio ni changamoto kwa sababu hakuna anayeamini katika kipaji chake. Ili kuonesha kuwa unapigania kile unachotaka, unatakiwa kuwa studio wakati wote ili upate nafasi ya kurekodi.
Hali hiyo iliwafanya wakalazimika kulala studio kwa miaka minne mfululizo, ili kuhakikisha wanafanikiwa kupitia muziki. Licha ya wao kupenda muziki familia yao, haikuamini, kuna wakati waliambiwa waache na watafute kazi nyingine.
“Familia yetu haikutaka tuamini muziki kwa sababu mafanikio yake hayana uhakika. Walitaka tuondoe matumaini kwenye muziki, lakini tulijaribu kuwapa matumaini kwamba siku moja tutakuwa mastaa na tutatengeneza nyimbo nyingi zitakazovuma,” anasema Muuh.
Mnamo 2018, Mabantu walianza kuachia ngoma zao kama vile ‘Sundi’, ‘Bodaboda’ na ‘Kama tulivyo’, ngoma hizo ziliwasaidia kutambulika, lakini si utambulisho ambao walikuwa wakiutamani hapo awali.
Kwa mujibu wa Muuh, Twaha alishauri kuwa wanatakiwa kubadili mtindo wao na kuanzisha aina fulani ya Bongoflava ambayo ni mpya kwenye tasnia ambayo itafanya wafanikiwe.
Kufikia 2020, Mabantu walitoa wimbo ‘No love, No stress,’ lakini haukuvuma sana hadi ulivyofanyiwa remix. Msanii wa muziki wa Hip-hop, Young Lunya na Moni Central zone waliruka kwenye remix hiyo na kuisaidia ngoma kupenya zaidi kwa mashabiki.
“Toleo la kwanza la wimbo halikufanya vizuri kama inavyopaswa kuwa, lakini tulipotoa toleo la pili, likawa kubwa na kila mtu alitufahamu na ikawa mwanga kwenye muziki na mtindo wetu kwa ujumla,” anasema Muuh.
Kuanzia hapo mambo yakaanza kuwa mepesi, wimbo wao wa ‘Sponsor’ ukawa wimbo wa taifa. Baadaye walitoa wimbo wa ‘Nawakera’ ambao walishirikiana na Young Lunya, pia walishiriki kwenye wimbo wa R the DJ ulioitwa ‘Shobo’ uliotoka miaka mitatu iliyopita.
Ndani ya mwaka huo, Mabantu walitoa EP ‘No Stress’ yenye nyimbo tano ‘Nakesha’, ‘Hit Song’, ‘Show Show’, ‘Hachiti’ na ‘Umenuna’. Katika nyimbo zote, Marioo ndiye msanii pekee aliyeshirikishwa.
Juhudi zao kwenye muziki zinawaweka kwenye orodha ya wasanii wakubwa nchini. Walitumbuiza katika matamasha mbalimbali kama vile Fiesta, Mziki Mnene, Wasafi Festivals na Nandy Festival. Wakizungumzia wasanii wanaotamani kufanya nao kazi, wametaja P Square alikuwa kwenye orodha yao.
“Kwa kuwa tuko kwenye biashara ya muziki, ndoto yetu ilikuwa ni kushirikiana na P Square. Lakini haikutokea kama ilivyopangwa kwa sababu ya kutengana kwao,” anasema Twaha.
Licha ya mafanikio yote waliyoyapata, Mabantu wanasema ni vigumu kuzungumzia mustakabali wao, lakini wanachoamini ni kupeperusha bendera ya Bongoflava.
“Tunapambana kupata mafanikio katika muziki wetu na kupeperusha bendera ya bongo flava na ya nchi kupitia muziki wetu,” wanaeleza.
Twaha na Muuh wanaeleza kuwa ushirikiano wao kwenye muziki utaishi milele bila kundi lao kuvunjika kwa sababu uhusiano wao pia ni mpango wa Mungu, hivyo hauwezi kuvunjika kirahisi.
“Tumejifunza mengi kutoka kwa ndugu zetu na kila siku tunajifunza kutoka kwao na jinsi ya kuvuka vikwazo tofauti, lakini kila siku tunaomba ili tuzidi kuwa na nguvu,” wanasema.
Kauli yao ya kutotengana inajidhihirisha kila kukicha kutokana na wawili hao kuendelea kuachia ngoma mbalimbali ambazo zinafanya vizuri mtaani, huku kwa mwaka 2024 wametoa pini lao linaloenda kwa jina la ‘Mali safi’.
Mabantu wanasema wamekuwa wakiuchukulia muziki kama kazi yao na ndiyo maana wanaachia vitu bora zaidi ya vilivyopita, kila wakati wanategemea kuachia kazi nzuri ambayo haitawaangusha mashabiki wao.
Wanasema ‘Mali Safi’ ni wazo ambalo walikuwa nalo kwa muda mrefu, lakini kwa mwaka 2024 wameona ndiyo wakati sahihi kwao kupita nayo.
“Mali Safi ni moja ya idea ambayo tumekuwa nayo muda mrefu sana, tulikuwa na neno ambalo linatumika nchini Kenya, tukawa tunaamini tukiweza kulibadilisha, kuja kwenye muziki tunaweza kutengeneza biashara nzuri nchini kwetu na kwenye nchi za Afrika Mashariki kwa sababu ‘Mali Safi’ ni neno ambalo linatumiwa sana huko.
“Hadi siku ambayo tuliamini tumepata ‘melodi’ na aina ya ‘saundi’ ambayo tunaweza kuitumia ndipo tulipokamilisha audio ya Mali Safi, uzuri tulichotegemea ndicho kimetokea kwa sababu umekuwa wimbo pendwa sana kwa nchi hizo,” wanasema Mabantu.
Mabantu wanasema wanaamini huu umekuwa muda mzuri kwao kuachia wimbo kwa sababu watu pia wanatamani kusikiliza muziki tofauti, kwani kwa sasa muziki uliotawala ni Amapiano, lakini kama wasanii wanaamini mashabiki wanatakiwa kusikia vitu tofauti.
Idea za nyimbo zao ndiyo kitu pekee ambacho kinafanya Mabantu waendelee kufanya vizuri na kupata mashabiki wengi, wanasema mara nyingi hupenda kuandika nyimbo zao wakiwa nyumbani au safarini, wanaweka wazi kuwa nyimbo zao nyingi zilizofanya vizuri wameandika wakiwa nyumbani na siyo studio kwa sababu kunakuwa na mambo mengi.
Mabantu wanamaliza kwa kusema wanaamini mtandao wa kijamii kama vile Tiktok umekuwa ukisaidia sana wasanii kuuza kazi zao, hasa kutokana na mtandao huo kuwa na wafuatiliaji wengi.
“Sisi ni moja ya wasanii wa kwanza kabisa kuweza kuutumia huo mtandao, nikisema wa kwanza namaanisha, tulikuwa wa kwanza kuutumia kusambaza nyimbo zetu, watu walikuwa wanafanya tu video kwenye mtandao huo, lakini sisi tukaufanya kama mtandao wa kutangaza wimbo wetu.
Tulianza na wimbo uitwao ‘Utamu’, ambao ndiyo ukatupatia darasa tukaona mbona kama umepokelewa kwa ukubwa, tangu hapo tukawa ‘siriazi’ zaidi tukajiandaa kwa kazi inayofuata, ilikuwa inaitwa ‘Star’ tukaandaa kila kitu kwa ajili ya Tiktok kuanzia ‘madansa’, kwa asilimia mia tulifanikiwa, tangu hapo tukaanza kuona wasanii wengine wakitumia Tiktok katika ‘kusapoti’ muziki wao.