Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anko Kitime: Utamu wa gitaa la solo

Muktasari:

  • Katika mfumo wa awali kuanzia miaka ya 50,  bendi zilikuwa  na mfumo wa kutumia magitaa matatu, gitaa la Solo, gitaa la rythm na gitaa la bezi. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu, huku rythm ikiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho Bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine.

Dar es Salaam. Gitaa la solo limekuwa sehemu muhimu sana katika muziki wa rumba kwa muda mrefu. Gitaa hili lilipata jina hili ambalo maana yake ni ‘pekee’ kwa vile katika nyimbo za wawili za rumba, gitaa hilo lilipigwa kwa kujitokeza pekee kwa mtindo uliopendezesha sana wimbo.

Katika mfumo wa awali kuanzia miaka ya 50,  bendi zilikuwa  na mfumo wa kutumia magitaa matatu, gitaa la Solo, gitaa la rythm na gitaa la bezi. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu, huku rythm ikiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho Bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine.

Kimuundo gitaa la rythm na la solo hakuna tofauti. Yote yana nyuzi 6,lakini katika kutyuni kwenye amplifier, gitaa la rythm hunyimwa treble (ukali) kiasi na kuongeza bezi  zaidi kuliko gitaa la solo ambalo huwa na treble zaidi ya magitaa mengine. 

Mwanzoni mwa miaka ya 60 likaanza kutumika gitaa la nne lililojulikana kama ‘second solo’ au Wakongo waliliita ‘mi solo’. Inasemekana kaka yake mpiga solo maarufu wa Kongo wa enzi hizo Dr Nico, ndiye aliyeanzisha mtindo wa kuongeza gitaa hilo la nne.

Hili lilikuwa likipigwa kwa mifumo mbalimbali katika bendi. Bendi nyingine zilitumia second solo kama gitaa lililokuwa linajibizana na solo, na bendi nyingine lilikuwa linajibizana na rythm na hata kulikuweko mfumo ambapo gitaa hilo aidha lilikuwa likipiga ‘harmony ya gitaa la solo au ya gitaa la rythm.


Bendi nyingine , mfano  Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza liliongeza ubunifu na kuongeza gitaa la 5 na kuliita ‘chord guitar’. 

Ubunifu huu uliongeza sana uzito wa muziki na hata kuleta ladha mbalimbali za muziki wa dansi. Na uamuzi wa aina ya mpangilio wa magitaa uliweza kuleta tofauti kubwa kati ya bendi moja na nyingine. 

Katika miaka ya nyuma mpiga solo alikuwa mtu muhimu sana katika bendi, mara nyingi ndiye aliyepewa mshahara mnono zaidi ya mtu yeyote na katika bendi nyingi alipewa uongozi ili asihame bendi. Gitaa la solo liliweza pia kuweka nembo ya bendi.

Kila mpiga solo alijitahidi kuja na aina yake ya upigaji ili kuleta utamu mpya katika bendi yake. Hakika wapiga magitaa ya solo katika nchi hii kuanzia miaka ya 60 walifanya mambo makubwa sana.

Bendi zilikuwa nyingi na kwa kuwa kila bendi ilikuwa na mpiga solo, si rahisi kuwakumbuka wote lakini niwataje wachache ambao wanakuja kwenye kumbukumbu ambao wameacha alama ya kudumu.

Nianze na mkonge Michael Enoch, wengi humkumbuka kama mpiga saksafon wa Dar International Orchestra na Mlimani Park Orchestra ambako alipata jina la King Enoch, mwanamuziki huyu asili yake ilikuwa ni Zambia na aliletwa nchini na mwanasiasa maarufu aliyeitwa John Mwakangale, mwanzoni mwa miaka ya 60 kwa ajili ya kupiga kwenye bendi yake iliyokuwa pale Mbeya iliyoitwa Three Bothers.

Moja ya ziara za bendi hii ilifikisha bendi katika jiji la Mwanza, kukatokea mkasa ambapo vyombo vya bendi viliibiwa baada ya dreva wa gari walilokodisha kusafirisha vyombo pale Mwanza kukimbia na vyombo.

Michael Enoch na wenzie wakalazimika kutafuta kazi wakawa wanapiga kwenye bendi moja ya palepale Mwanza. Wakiwa pale wakagundulika na mdau mmoja wa Dar es Salaam Jazz Band aliyekuwa ametumwa Mwanza kutafuta mpiga gitaa la solo. 

Na ndipo Michael Enoch akajikuta kwenye safari ya kujiunga na Dar es Salaam Jazz Band. Kwa miaka mingi baada ya hapo Michael Enoch aliweza kuwa na aina yake ya upigaji wa gitaa la solo katika bendi ya Dar Jazz ambayo ilijiita pia ‘Majini ya Bahari’, mpaka leo  hata wapigaji maarufu wa zama hizi hawajaweza kurudia baadhi ya nyimbo zilizopigwa na mwamba huyu miaka ya 70. 

Mpigaji solo mwingine hodari naye aliitwa Michael vile vile , jina lake kamili aliitwa Michael Vincent. Huyu alikuwa mpiga solo wa bendi iliyokuwa mali ya kiwanda cha nguo kilichojengwa na serikali ya China na kuitwa Friendship Textile Mills, jina lililoashiria Urafiki wa Tanzania na China.

Meneja Mkuu kiwanda hicho marehemu Joseph Rwegasira akanunua vyombo vya muziki na kuanzisha bendi iliyoitwa Urafiki Jazz Band. Michael Vicent akawa ndiye mpiga solo wa bendi hii, kama ilivyo kwa Michael mwenziye niliyemtaja hapo juu hakika aliweza kurekodi nyimbo nyingi zilizopendwa sana, bendi ikatumia mtindo wake wa Chaka Chua.

Bendi kongwe ambayo inafahamika zaidi kwa mtindo wa Msondo, toka ilipoanza mwaka 1964, imekuwa na wapiga gitaa la solo bora sana,  wakiwemo akina Hamis Franco, Wilson Boniphase, Abel Balthazar, Said Mabela,Kassim Mponda, Ridhwan Pangamawe, kila mmoja wao aliweza kuja na upigaji wa aina yake.

Wapigaji solo wa bendi ya Mlimani Park, wana Sikinde nao hali kadhalika, toka enzi za akina Joseph Mulenga, Henry Mkanyia na wengine waliweza kuipa Mlimani Park Orchestra sauti ya aina ya pekee.  

Kama nilivyosema awali ni ngumu kuwataja wote lakini baadhi ni, kama Hamza Kalala, Shem Karenga, John Kijiko, Alphonce Makelo, Ndala Kasheba, Nguza Viking na Dekula Kahanga.