Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anko Kitime: Utamaduni wa gitaa ulivyoingia Tanzania

Muktasari:

  • Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu, huku rythm ikiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho Bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine. Kimuundo gitaa la rythm na gitaa la solo hayana tofauti. 

Dar es Salaam. Kuanzia ngwe ya pili ya muongo ulioanzia mwaka 1950, bendi za hapa nchini zilianza utamaduni wa mfumo wa kutumia magitaa matatu, gitaa la solo, gitaa la rythm na gitaa la Bass.

Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu, huku rythm ikiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho Bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine. Kimuundo gitaa la rythm na gitaa la solo hayana tofauti. 

Yote yana nyuzi 6 lakini katika kurekebisha sauti  kwenye amplifaya, gitaa la rythm hunyimwa ukali (treble) kiasi na kuongeza bass zaidi kuliko gitaa la solo ambalo huwa na treble zaidi ya magitaa mengine, na hata sauti (volume) huwa kwa kawaida juu kuliko gitaa la rythm. 

Kwa kuwa kabla ya ujio wa gitaa la solo, bendi zilikuwa zikitumia banjo au mandolin kwa ajili ya solo, kuna wanamuziki waliogoma kuhamia  mfumo wa upigaji gitaa la solo na kubaki na banjo na mandolin kwenye bendi zao. 

Kati ya waliokuwa maarufu katika kukataa gitaa la solo ni marehemu Mzee Salum Zahoro ambaye wakati bendi nyingine zikiwa zimehamia kwenye magitaa ya umeme katika upigaji wa solo yeye akabaki anapiga mandolin.

 Na hakika alipokuwa na bendi yake ya Kiko Kids, aliendelea kutoa nyimbo nyingi ambazo bado ni maarufu mpaka leo ambazo alipiga mandolin badala ya gitaa la solo kama ilivyokuwa kawaida. 

Nyimbo za Kiko Kids kama  ‘Kijana Sudi’ na ‘Nalia S’ ni baadhi ya nyimbo ambazo Mzee Zahoro alitumia mandolin. Mwanzoni mwa miaka ya 60, bendi ya African Fiesta iliyokuwa chini ya mpiga solo mahiri sana Dk Nico illingiza mtindo mpya wa kupiga magitaa manne, hivyo kukawa na magita yale matatu ya awali, solo, rhythm na bass na sasa likaongezeka gitaa jingine, waanzilishi waliliita mi solo, na huku kwetu likajulikana kwa jina la ‘second solo’.

 Katika bendi ya African Fiesta gitaa la second solo lilikuwa likijaza nafasi kati ya gitaa la solo lililokuwa likipigwa na Dk Nico na gitaa la rhythm. Bendi nyingi Afrika Mashariki na kati zikaanza kutumia second solo lakini kila bendi ikibuni staili yake.

Bendi nyingine zilitumia second solo kama gitaa lililokuwa linajibizana na solo, na bendi nyingine gitaa hilo lilikuwa linajibizana na gitaa la rythm, na hata kulikuweko mfumo ambapo gitaa hilo aidha lilikuwa likipiga melodia ileile  ya gitaa la solo au ya gitaa la rhythm na kuweka manjonjo ya kupendeza. 
Bendi nyingine, mfano  Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza liliongeza ubunifu na kuongeza gitaa la 5 na kuliita ‘chord guitar’. 

Ubunifu huu uliongeza sana uzito wa muziki na hata kuleta ladha mbalimbali za muziki wa dansi. Na uamuzi wa aina ya mpangilio wa magitaa uliweza kuleta tofauti kubwa kati yabendi moja na nyingine, sifa moja kubwa ya bendi za zamani.

Lakini leo tuzungumzie gitaa la rythm. Chombo hiki bado kinapigwa katika bendi nyingi lakini umuhimu wake umeshuka sana, unaweza kuingia bendi nyingi sana usikute gitaa hili.

Katika kipindi cha miaka ya 60 na 70, gitaa hili lilikuwa na umuhimu mkubwa na wapigaji wake waliweza kujijengea sifa kubwa.

Kati ya wapiga gitaa la rythm maarufu alikuweko marehemu Harrison Siwale, jina lake la kisanii alijulikana kama Sachmo,  huyu alikuwa kijana mwenye asili ya Zambia, wazazi wake walihamia Tanga kufuata kazi katika mashamba ya mkonge.

 Sachmo alikuwa mpiga gitaa mzuri sana hivyo alianzia Atomic Jazz Band na hatimae Jamhuri Jazz Band, bendi zote zilikuwa za mji wa Tanga. Satchmo alikuwa na staili peke yake ya kupiga gitaa la rythm,  lakini hakika wapiga rythm wengi walichukua mtindo wake na kama ilivyokuwa kawaida wakati huo, nao wakabuni vionjo vya aina yao. Upigaji wake ulitawala katika nyimbo za Jamhuri Jazz Band wakati huo. Ufundi wake unaonekana sana katika nyimbo kama Mganga no 1 na 2, au Blandina. 

Wakati huohuo kule Tabora kulikuwa na mpiga gitaa la rhythm mwingine aliyekuwa na staili yake, nae si mwingine ni Mzee Kasim Kaluwona, wapenzi wake walimuita Kassim Rhythm, nae alikuwa na staili tofauti ya upigaji wa gitaa la rythm uliyoifanya Tabora Jazz kuwa na staili yake peke yake. 

Ukisikiliza nyimbo kama Dada Asha, au Lemmy, unasikia vizuri sana aina ya upigaji wake wa gitaa hilo. Charles Kazembe  kijana kutoka Masasi aliyeingia jiji la Morogoro na kubadili upigaji wa gitaa la rhythm katika bendi zote mbili kongwe pale Morogoro, kwani alianzia Cuban Marimba kisha akahamia Morogoro Jazz Band.

 Wanao kumbuka wimbo Wajomba Wamechacha, wanakumbuka jinsi watu walivyofurahi alipokuwa akiachiwa peke yake apige kipande chake cha rhythm. Hao ni wapigaji wachache tu kwani kila bendi ilikuwa na mpiga gitaa la rhythm, na kila moja alikuwa na umahiri wake.

 Mwanzoni mwa miaka yay a sabini aina mpya ya upigaji wa gitaa la rhythm iliingia. Hii ilianza kwa kufunga nyuzi kwa namna ambayo si kawaida katika magitaa, wapiga rythm wakauondoa uzi namba nne katika gitaa hilo na kuweka uzi namba moja badala yake, hivyo kukawa na nyuzi namba moja 2 katika gitaa moja, hapo ndipo akina Vata Mombasa wakaweza kuleta utamu mpya katika upigaji wa rythm, ufungaji wa aina hii wa nyuzi za gitaa ulifahamika kama ‘double string’.  

Utamu wa ufungaji wa nyuzi kwa staili hii uliweza kusikika vizuri katika gitaa lililopigwa mwanzo kabisa wa wimbo Andoya wa Orchestra Kamale.  

Wapiga gitaa la rhythm wa Orchestra Kiam wakawa na staili yao ya kupiga gita hili lenye double string kwa spidi kali sana, mtindo wa upigaji huo ulikuweko katika nyimbo zao kama Kamiki, Bomoto, Mbale, Afrika nzima ikafurahia nyimbo zao. 

Umuhimu wa gitaa la rythm ulikuwa ukionekana kwa bendi nyingi kuwa na mtindo wa ‘kuachia rythm’, huo ulikuwa ni mpangilio ambapo gitaa la rythm liliachwa lipige peke yake wakati magitaa mengine yakiwa kimya. Hapo mpiga rythm aliachiwa kucheza na gitaa lake kwa kulipiga alivyotaka na  kuonyesha umahiri wake wote. 

Mtindo huu ulipendwa sana na wapenzi wa enzi hizo lakini kila zama na vitabu vyake kitabu cha zama hizi hakina hadithi ya gitaa la rhythm.