Anko Kitime: Athari za Ukimwi katika muziki Tanzania
Muktasari:
- Wajerumani ndio walileta vifaa vya muziki vya kwanza vya kigeni. Baadhi ya vifaa hivi vilikuwa ni vyombo vya bendi za kijeshi, mfano vyombo vya kupuliza kama saksafon na tarumbeta na ngoma ambazo zilitengenezwa huko kwao. Kuingia kwa muziki huu mgeni pia ndiko kulikoingiza neno ‘muziki’.
Dar es Salaam. Desemba 1, huwa ni siku ya Ukimwi Duniani, makala hii tuangalie athari ya Ukimwi katika muziki wa Tanzania.
Kuna mambo katika historia ambayo yameweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa muziki hapa nchini. Ujio wa Wajerumani waliokuja kuitawala nchi hii mwishoni mwa karne ya 19, ni mwanzo muhimu sana wa historia ya muziki wetu huu wa vyombo vya muziki vya kigeni.
Wajerumani ndio walileta vifaa vya muziki vya kwanza vya kigeni. Baadhi ya vifaa hivi vilikuwa ni vyombo vya bendi za kijeshi, mfano vyombo vya kupuliza kama saksafon na tarumbeta na ngoma ambazo zilitengenezwa huko kwao. Kuingia kwa muziki huu mgeni pia ndiko kulikoingiza neno ‘muziki’.
Wenyeji walikuwa na ngoma zao mbalimbali ambazo hazikuwa na jina moja la ujumla. Kila kabila lilikuwa na ngoma zilizoitwa majina tofauti kutokana na sababu za ngoma ile na mara nyingine hata aina ya ngoma zinazotumika.
Hivyo kulikuwa na majina tofauti kwa ngoma za matambiko, ngoma za matibabu, ngoma za kusherehekea mambo mbalimbali kama mavuno na kadhalika. Baada ya wenyeji kuona aina ya muziki uliokuwa unapigwa na wanajeshi wa Kijerumani, nao wakaiga na kuanzisha aina mpya ya muziki waliyoiita ‘muziki wa beni’.
Muziki huu ulipata umaarufu mkubwa kwa vijana wa wakati huo na ulisaidia sana kuanza kueneza Kiswahili katika nchi yetu.
Utawala wa nchi hii ulipobadilika na kuchukuliwa na Waingereza mambo kadhaa yalitokea, baadhi ya wanajeshi wa Kiafrika walioshiriki katika vita kuu walirudi makwao na vifaa vipya vya muziki kama magitaa banjo, na akodian na kuingiza muziki wa aina nyingine katika jamii zao.
Teknolojia ya gramafoni ambayo iliwezesha kupiga santuri, na baadaye kuingia kwa teknolojia ya radio, viliwezesha wenyeji kuanza kusikia muziki kutoka kona mbalimbali za dunia.
Wakati huohuo Waingereza waliingiza utamaduni wa kuwa na klabu, ambazo zilikuwa vyanzo vya vikundi vya kwanza vya kupiga muziki uliosikika katika santuri na radio.
Kati ya vikundi vya kwanza vya muziki ni YMCA Social Orchestra na Dar es Salaam Social Orchestra, ambayo inasemekana kuwa ndio iliyokuja kuzaa Dar es Salaam Jazz Band. Huo ukawa mwanzo wa muziki wa vikundi vingi vilivyokuja kuenea nchini kote.
Baada ya Uhuru, karibu kila mji mkubwa ulikuwa na bendi moja au zaidi, bendi zilikuwa zikipiga muziki wa aina mbalimbali, kuna bendi zilikuwa zikipiga muziki kutokana na kabila ambapo bendi ilikuwepo.
Bendi nyingine nyingi zilikuwa zikipiga muziki kwa kuiga muziki kutoka Cuba, kwani kulikuwa na santuri nyingi zilizokuwa za muziki kutoka nchi hiyo ambazo zilipendwa sana bara lote la Afrika, na pia kulikuweko na vikundi vingi vilivyopiga muziki kwa kuiga muziki kutoka nchi za magharibi.
Miaka kadhaa baada ya Uhuru, nchi yetu ilianza kuendeshwa kwa mfumo wa Siasa ya Ujamaa, mashirika ya umma na taasisi za kiserikali vilihamasishwa kuwa na vikundi vya sanaa, bendi nyingi zilianzishwa nchini kote na kazi zilizofanywa na bendi hizo, bado zinasikika na zimepewa jina maarufu la ‘zilipendwa’.
Katikati ya miaka ya 80 tuliokuwa wanamuziki tukaanzia kusikia kuhusu ugonjwa ambao ulikuwa ukimpata mtu ana dhoofu na kisha kufa. Ugonjwa huu ulipewa majina mengi sana, yakiwamo Juliana, Ngoma, Udude, kule Iringa ugonjwa huo ulijulikana kama Lugandaganda, yaani wa Kukondakonda, na Uwamuledio, yaani ugonjwa wa redioni kwani redio ndio zilikuwa zikiuzungumzia sana, zikishauri watu kubadili tabia na kubaki na mpenzi mmoja.
Kwa hakika pamoja na taarifa za ugonjwa huo wa kutisha, wanamuziki hatukubadilika, tulikuwa maarufu hivyo kuweza kuwa na wapenzi wengi. Mfumo wa biashara ya muziki katika zama hizo ulilazimisha vikundi vya muziki kusafiri kuzunguka kila kona ya nchi, na katika mizunguko hiyo utamaduni wa wapenzi wengi uliendelea.
Nakumbuka katika safari moja nilipokuwa Vijana Jazz Band tulipata ziara ya kuzunguka mkoa wa Kagera, tulipotua tu na meli Bukoba, asubuhi saa kumi na mbili, kabla ya hata kupata mahala pa kulala tulipelekwa ofisini kwa Mkuu wa Wilaya bwana Pius Mlowe, kuonywa kuwa tutulie tusitishe tabia zetu. Hii ilikuwa dalili tosha ya hali ilivyokuwa mbaya.
Kuanzia miaka hiyo ya 80 wanamuziki wengi sana walifariki wakiwa bado wadogo sana, na wengi wakiwa katika ubora wa hali ya juu. Sauti zao na kazi zao zimebaki kumbukumbu tu zinazoitwa zilipendwa.
Ukimwi umefanya kuweko na pengo kubwa kati ya wanamuziki bora wa zamani na wanamuziki bora wa zama hizi. Kumekuweko na pengo kubwa sana katika muziki wa kambi hizi mbili pengo ambalo si kubwa kiasi hicho katika nchi nyingine, ambako wanamuziki wakongwe wamekuwa ndio washauri wa wanamuziki wapya.
Muziki wa sasa ni kama umezaliwa katika ombwe, hata muziki wa dansi ambao ungetegemea kuwa ungekuwa unaendeleza mazuri ya muziki ule uliopewa jina la ‘zilipendwa’ nao umekuwa kama unazaliwa upya na hauna mizizi ya muziki wa Kitanzania.