Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dabi ya Kariakoo yapangiwa tarehe, kupigwa Juni 15 Kwa Mkapa

Muktasari:

  • Mechi ya mzunguko wa kwanza ya Ligi Kuu baina ya Simba na Yanga ilimalizika kwa ushindi wa bao 1-0 ambao Yanga iliupata kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imepanga mechi ya mzunguko wa pili ya Ligi Kuu baina ya Yanga na Simba ‘Kariakoo Derby’ kuchezwa Jumapili Juni 15, 2025.

Ratiba hiyo imeanikwa saa kadhaa baada ya uongozi wa Yanga kutangaza kutokuwa tayari kucheza mchezo huo ambao awali ulikuwa ufanyike Machi 8 mwaka huu.

Mechi ya Machi 8 haikuchezwa baada ya kuahirishwa na TPLB kufuatia vurugu zilizojitokeza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa siku moja kabla ya mchezo baada ya Simba kuzuiwa na waliotambulika kuwa ni walinzi wa Yanga ‘makomandoo’ kufanya mazoezi uwanjani hapo.

Ratiba mpya iliyotolewa na TPLB imeonyesha kuwa mechi hiyo ya watani wa jadi itachezwa Juni 15, saa 11:00 jioni.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, mechi za mwisho za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu zitachezwa Jumapili, Juni 22 mwaka huu.

Wiki moja baadaye kutachezwa mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB siku moja kati ya Juni 26 hadi Juni 28.

Msimu utamalizika Julai 7, 2025 kwa mchezo wa marudiano wa mchujo baina ya timu ya Ligi Kuu baina ya timu ya Ligi Kuu na timu ya Ligi ya Championship.

Hata hivyo jana, Jumatatu, Mei 5, 2025 Yanga ilitangaza kuwa haitocheza mechi hiyo licha ya shauri ambalo ilifungua katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kutupiliwa mbali.

"Msimamo wa klabu yetu juu ya mchezo namba 184 wa Ligi Kuu Msimu huu uko pale pale kuwa hatutashiriki kwenye mchezo huo kwa namna yoyote ile," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilihitimisha kwa kuwataka wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa tayari kupambana kwa njia zote kuhakikisha haki inapatikana na kulaani kile walichokiita "dhulma na uvunjwaji mkubwa wa kanuni unaofanywa na mamlaka za soka."

Mei Mosi mwaka huu, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ilitoa taarifa ya kufuta na kutoendelea na shauri lililofunguliwa na Yanga kuhusu mchezo wake wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ulioahirishwa dhidi ya Simba, Machi 8, 2025.

Yanga iliiomba CAS mechi ya marudiano ya Ligi Kuu baina yao na Simba isipangiwe tarehe na pia ipewe pointi za mezani.

Mechi hiyo ilikuwa ichezwe Machi 8 mwaka huu lakini ikaahirishwa baada ya Simba kuzuiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, siku moja kabla ya mchezo.

CAS iliamua kutupilia mbali shauri hilo kwa vile Yanga haikufuata utaratibu wa kushughulikia malalamiko yake kwa kupeleka shauri hilo CAS kabla ya kuanza na vyombo vya ndani.

CAS iliiagiza Yanga kupeleka shauri hilo kwanza katika mamlaka za ndani za uendeshaji soka na baada ya hapo ndio ilifikishe katika mahakama hiyo.