Biashara United Kutoka michuano ya CAF hadi First League

Muktasari:
- Timu hiyo maarufu kwa jina la Wanajeshi wa Mpakani, ilipata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kumaliza nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2020-2021, ilipokusanya pointi 50, ikishinda mechi 13, sare 11 na kupoteza 10.
BIASHARA United ni miongoni mwa timu zenye umaarufu hapa nchini kutokana na wasifu wake iliojitengenezea, huku ikikumbukwa zaidi msimu wa 2021-2022 iliposhiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Timu hiyo maarufu kwa jina la Wanajeshi wa Mpakani, ilipata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kumaliza nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2020-2021, ilipokusanya pointi 50, ikishinda mechi 13, sare 11 na kupoteza 10.
Katika ushiriki wa michuano hiyo, ilienguliwa raundi ya pili baada ya kushindwa kusafiri katika mechi ya marudiano dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya, mchezo ambao ulitakiwa kufanyika Oktoba 23, 2021, kwenye Dimba la Martyrs Benina jijini Benghazi.
Sababu kubwa iliyoelezwa ilikuwa ni kukosa kwa wakati vibali vya Kimataifa vya Anga katika nchi za Sudan, Sudan Kusini na Libya, ingawa kikosi hicho kilishinda mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar kwa mabao 2-0, Oktoba 15, 2021.

Baada ya hapo timu hiyo ikakumbwa na jinamizi la kutofanya vizuri na kushuka Ligi ya Championship inayocheza sasa, japo kwa bahati mbaya imeporomoka hadi First League, hivyo Mwanaspoti linaelezea sababu zilizochangia anguko la kikosi hicho.
TATIZO LILIANZIA HAPA!
Kitendo cha aliyekuwa mfadhili na rais wa timu hiyo, Revocatus Rugumila kujiweka pembeni, kulichangia kwa kiasi kikubwa kikosi hicho kukumbwa na ukata wa kujiendesha, hali iliyosababisha kushindwa kufika kwenye vituo vya mechi kwa wakati.
Rugumila aliyejiuzulu nafasi yake Oktoba 10, 2024, katika mahojiano na gazeti hili anasema sababu kubwa ya yeye kujiweka pembeni ni kutokana na wadau wa mkoani Mara kumsusia timu hiyo, jambo aliloona halina afya na hawawezi kutimiza malengo.
“Nilikuwa natoa fedha zangu za kuendesha timu kuanzia usajili mwaka 2023 hadi nilipoondoka, wanachama wana hisa asilimia 51, ila hawajishughulishi na chochote kwani hata tukiitisha kikao wanakuja wawili tu wakati tuko zaidi ya 20,” anasema.
Rais huyo anasema ataondoka kabisa katika timu hiyo endapo tu atauza hisa zake zote ila kwa sasa amejiweka pembeni na hawezi kuiombea mabaya, kwa sababu ya watu wachache ambao hawaitakii mema timu hiyo ili irejee tena Ligi Kuu Bara.

Kuondoka kwa Rugumila, kukaifanya timu hiyo kuandamwa na ukata ulioifanya hadi kushindwa kufika katika mechi ya ugenini dhidi ya Mbeya City, iliyotakiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Desemba 3, 2024 na kusababisha kupokwa pointi 15 na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), hivyo kuchangia kushuka daraja, ikiwa na pointi 15, baada ya kushinda mechi nane, sare sita na kupoteza 15 kati ya 29, ilizocheza hadi sasa.
VIONGOZI/ MASTAA WASEPA
Ukiachana na kuondoka kwa Rugumila kikosini humo, hata aliyekuwa kaimu mwenyekiti wa timu hiyo, Augustine Mgendi alijiweka pembeni kutokana na changamoto hizo za kiuchumi zinazoendelea, zilizochangia kikosi hicho kufika hapa kilipo.
Ukata wa timu hiyo uliwafanya baadhi ya mastaa wa kikosi hicho akiwemo aliyekuwa nyota wa Yanga, Ditram Nchimbi kuondoka na kujiunga na Mbeya Kwanza, sawa na Sadalla Lipangile (KenGold), Faustine Kulwa na Elias Maguri waliotua Geita Gold.
Mbali na nyota hao waliotazamwa kukipigania kikosi hicho kwa ajili ya kukirejesha tena Ligi Kuu Bara msimu ujao, hata Mussa Rashid aliyekuwa akiliongoza benchi la ufundi, aliondoka na kutua Polisi Tanzania.

Kuondoka kwao, Biashara United ikasuka upya kikosi hicho ambacho licha ya jitihada za nyota kama Pascas Wagana, Khalid Zuberi, Stewart Theodore, Timotheo Franswa na Abdumalik Hamad Jumbe lakini walishindwa kukibakisha kutokana na kutokuwa na uzoefu.
YAWEKA REKODI
Katika timu sita zilizoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa misimu ya hivi karibuni, Biashara United imeweka rekodi ya kushuka daraja hadi kushiriki First League, kwani kabla ya hapo hakuna nyingine iliyowahi kufanya jambo hilo.
Kwa miaka ya hivi karibuni, timu zilizofuzu michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ni KMC FC, Namungo, Coastal Union na Singida Fountain Gate iliyokuja kutenganishwa baadaye, huku nyingine ni Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship kwa sasa.
Biashara United imefuata nyayo za mabingwa wa Ligi Kuu Bara mwaka 1982, Pan Africans iliyowahi kushiriki pia michuano ya CAF, ingawa kwa sasa inashiriki First League baada ya kutokuwa na msimu bora wa 2023-2024, katika Ligi ya Championship.
Msimu huo wa 2023-2024, Pan Africans ambao ni mabingwa wa Kombe la Muungano mwaka 1982, ilimaliza nafasi ya 15, katika Ligi ya Championship ikiwa na pointi 20, baada ya kushinda mechi tano, sare tano na kupoteza 20, kati ya 30 ilizocheza.

KAULI YA UONGOZI
Mwenyekiti mpya wa timu hiyo, Gabriel Ipyana anasema licha ya changamoto zilizojitokeza ila bado wao kama viongozi wana morali kubwa ya kuendelea kukipigania kikosi hicho, huku akiwaomba wadau na mashabiki wa Mara kuendelea kuwaunga mkono.
“Ukiangalia msimamo ulivyo, utagundua zile pointi 15 tulizokatwa ndizo zilizotushusha daraja, kiukweli imetuuma lakini hatuna budi kupambana ili kuirejesha timu katika ushindani, bado tuko katika uwanja wa vita na hatujakata tamaa kabisa,” anasema Ipyana.
Ipyana anasema baada ya Ligi ya Championship kuisha watakuwa na kikao cha viongozi kwa ajili ya kujadili namna nzuri ya kuipambania timu hiyo, ingawa hadi sasa jambo analolishukuru kuna mwekezaji mpya aliyepo tayari kukiokoa kikosi hicho.