Prime
Shughuli imekuwa nzito Chamazi... Azam yarusha taulo

Muktasari:
- Wakati ukisoma hapa, nyuma ya pazia la timu hizo kuna vita ya kuwania kiatu cha mfungaji bora wa ligi, mchezaji bora, kipa bora na hata timu pia kuvizia tuzo mbalimbali ifikapo mwisho wa msimu.
MSIMU wa Ligi Kuu Bara ni kama umebakiza mechi zisizozidi tano kwa timu zote kuhitimishwa, lakini kuna harakati kibao zinazoendelea kwa kila timu kuweka hesabu zake sawa katika dakika hizi za lalasalama.
Wakati ukisoma hapa, nyuma ya pazia la timu hizo kuna vita ya kuwania kiatu cha mfungaji bora wa ligi, mchezaji bora, kipa bora na hata timu pia kuvizia tuzo mbalimbali ifikapo mwisho wa msimu.
Lakini, kwa sasa ukienda katika ofisi za klabu ya Azam, kuna mkataba mnono upo mezani wenye thamani ya Sh3.1 bilioni ukimsubiri kiungo fundi wa kikosi hicho, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kumwaga wino kuendelea kuitumikia timu hiyo kwa miaka miwili zaidi.
Hata hivyo, mkataba huo ambao upo mezani tangu Machi mwaka huu baada ya majadiliano ya mwisho, bado Fei Toto ameukaushia huku ikionekana hayupo tayari kuendelea kuitumikia Azam.
Wakati Fei Toto akiukaushia mkataba huo, uongozi wa Azam nao umeonekana kurusha taulo juu ya kuendelea kumshawishi kiungo huyo kusalia katika viunga vya Chamazi huku kukiwa na taarifa za Simba, Yanga na Kaizer Chiefs zinaiwania saini yake.
Fei ambaye mkataba wake na Azam umebaki msimu mmoja ukitarajiwa kumalizika 2026, alijiunga na timu hiyo Julai 2023 akisaini mkataba wa miaka mitatu akitokea Yanga.
Taarifa kutoka ndani ya Azam zinabainisha kuwa katika mkataba ambao uongozi wa klabu hiyo umemuwekea Fei, kuna kipengele cha mshahara mnono wa Sh80 milioni kwa mwezi, ada ya usajili na kuwa balozi wa bidhaa za kampuni za Azam.
Chanzo hicho kimefichua kuwa mapema mwaka huu uongozi wa klabu hiyo ulianza majadiliano na Fei juu ya mkataba mpya wenye maslahi makubwa zaidi kwani hivi sasa Azam inamlipa mshahara wa Sh23.5 milioni kwa mwezi.
Katika majadiliano hayo, awali uongozi ulikuwa tayari kumpa mshahara wa Sh40 milioni lakini Fei Toto akawa anapiga danadana hadi kiwango cha mwisho kikafika Sh80 milioni.

“Awali, mshahara wa Sh40 milioni alisema ni mdogo anataka Sh50 milioni, uongozi ukakubali kumpatia, makubaliano yakawa ni kwamba atakuja kusaini.
“Baadaye alivyorudi akabadili maneno akasema anataka mshahara wa Sh80 milioni ambapo pia uongozi ukakubali lakini mwenyewe akasema akimaliza majukumu ya timu ya taifa atakuja kusaini. Tukamuacha aende.
“Kama utakumbuka mara ya mwisho Taifa Stars imecheza Machi 26 mwaka huu dhidi ya Morocco na kupoteza kwa mabao 2-0, lakini tangu hapo hajaja kusaini mkataba na uongozi umeamua kukaa kimya. Inaonekana kuna ugumu wa kuendelea kumshawishi kubaki,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliendelea kubainisha kuwa, mbali na mshahara, pia Fei aliwekewa dola laki mbili kwa mwaka kwenye mkataba atakaosaini ambayo ni sawa na Sh539 milioni. Kiasi hicho ukija kukiweka kwa miaka miwili ambayo mkataba huo umeonyesha itakuwa ni dola laki nne (Sh1.1 bilioni).
“Ukiweka kando mshahara wa Sh80 milioni na dola laki nne za usajili kwa miaka miwili, pia kuna ofa ya kuwa balozi wa kampuni za Azam ambapo kila mwezi ni atapata Sh5 milioni,” kilisema chanzo hicho.

UGUMU WA KUONDOKA
Mtoa taarifa huyo aliendelea kufichua kuwa inavyoonekana Fei Toto hataki kubaki Azam, lakini kama anataka kuondoka kirahisi hivi sasa itashindikana bali inabidi asubiri mkataba wake umalizike kutokana na kipengele cha kulipa dola 500,000 (Sh1.3 bilioni) kilichowekwa kama ada ya kuvunjia mkataba wake kuonekana kuwa kikubwa.
“Tumejifunza kilichotokea kwa Prince Dube wakati ambao alikuwa anataka kuondoka kuna mgomo aliuweka, uongozi ukakaa naye mezani na kumalizana.
“Lakini kwa Fei Toto ni tofauti, hawezi kuondoka kwa staili hiyo bali kama kuna timu inataka kumnunua iweke mezani Dola 500,000 za kununua mkataba.
“Kama akigoma kuendelea kucheza akidhani ataondoka kama ilivyokuwa Dube anajidanganya kwani mkataba unamfunga, asubiri tu mkataba uishe sisi tutamuachia aondoke lakini sio kwa sasa,” kilimaliza chanzo hicho.
Huu ukiwa ni msimu wa pili ndani ya Azam, Fei Toto amekuwa mchezaji muhimu wa eneo la ushambuliaji ambapo msimu wa kwanza 2023-24 alimaliza wa pili katika ufungaji bora kwenye ligi akipachika mabao 19 nyuma ya kinara Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyefunga mabao 21.
Msimu huu, Fei namba zake zimekuwa juu kwa upande wa upishi wa mabao akitoa asisti 13 akiwa ndiye kinara huku pia akifunga mabao manne.
Ubora wake katika kutengeneza nafasi na kufunga, umekuwa ukizivutia timu nyingi kuwania saini yake huku Azam ikipambana kumbakisha lakini sasa imekuwa ngumu.

MCHANGANUO WA DILI JIPYA
Mkataba huo mpya ambao Azam imemuwekea Fei mezani wenye kipengele cha mshahara wa Sh80 milioni kwa mwezi, usajili Sh539 milioni kwa mwaka na ubalozi Sh5 milioni kwa mwezi, utamfanya kiungo huyo kuwa mchezaji mzawa anayelipwa zaidi.
Kwa mshahara pekee, ndani ya kipindi cha miaka miwili sawa na miezi 24, Fei Toto atakuwa amekunja kiasi cha Sh1.9 bilioni.
Ukija upande wa ada ya usajili, kwa miaka miwili itakuwa Sh1.1 bilioni huku fedha ya ubalozi ambayo kwa mwezi ni Sh5 milioni, ndani ya miezi 24 itakuwa Sh120 milioni. Jumla ya fedha hizo zote katika mkataba mpya ambao Azam imemuwekea Fei Toto ni kiasi cha Sh3.1 bilioni.
OFA YA SIMBA
Simba inamtaka Fei Toto huku kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids amewahi kufichua kwamba klabu hiyo ipo kwenye mawindo ya kuwania saini ya kiungo namba 10 bora Tanzania, ambaye watu wa soka fasta wamemhusisha Mzanzibari huyo.
Wekundu hao kwenye hesabu zao hadi sasa, ingawa hawajaifuata rasmi Azam lakini wamempa ofa kiungo huyo ya Sh600 milioni na mshahara mkubwa wa kiasi kisichopungua Sh30 milioni.
Simba pia inajipanga kuishawishi Azam, iwapeleke Chamazi wachezaji wawili ndani ya dili hilo wakiwamo winga mmoja na kiungo wa kati mmoja wote wazawa ukiweka mbali na fedha za kununua mkataba wa Fei, lakini wekundu hao wanaona uzito kutoa kiasi cha Sh1 bilioni kumaliza dili hilo.
Wekundu hao wanatafuta saini ya Fei Toto, ikiwa ni kutamani kiungo namba 10 bora zaidi, wakiona kama staa wao msimu huu Jean Charles Ahoua licha ya kuongoza kwa kufunga mabao kikosini hapo akiwa na mabao 12, bado hawapi kitu kikubwa wanachotamani hasa kwenye mechi kubwa.

YANGA IKO HIVI
Yanga ambayo ilimuuza ‘kinguvu’ Fei Toto kwenda Azam alipogoma kucheza, nayo imemaliza kiume mgogoro kati yake na kijana wake huyo, kisha hapohapo ikampa ofa ya kufuru ili arejee klabu kwake kuendeleza pale alipoishia.
Yanga imemwambia Fei Toto, atakapokubali kurejea, hatarudi kinyonge, kwani itamkabidhi fedha za kufuru Sh800 milioni, ikimwambia pia itampa mshahara wa Sh40 milioni.
Mbali na ofa hiyo, Yanga pia imemtaka Fei Toto kuchagua kujengewa nyumba anapopataka na pia atapewa gari la kifahari kwenye dili hilo, huku ikimwambia kuhusu kumalizana na Azam auachie uongozi wa timu hiyo ya wananchi kwani wanajua wapi watamalizana na mabosi wa timu yake.
Yanga inarejea kwa Fei baada ya kupata uhakika wa kumuuza kiungo wake Stephanie Aziz KI, anayetakiwa na FAR Rabat, pia Raja Athletic na Wydad Athletic ambazo nazo zinaendelea kupigania saini hiyo. Klabu zote hizo zinatoka Morocco.
Hesabu nyingine ni Yanga pia ina uhakika wa kutumia fedha ikiwa pia imepata uhakika wa kuvuna fedha nyingi kwenye hesabu za kumuuza mshambuliaji wake Clement Mzize.
Vinara hao wa ligi, wanataka Fei Toto arudi kuziba pengo la Aziz KI kwenye kikosi hicho kuungana na mastaa wengine.
Yanga wakati inamuuza Fei kwenda Azam, iliweka makubaliano rasmi na klabu hiyo kwamba endapo kiungo huyo atauzwa kwa timu yoyote ndani ya Tanzania, basi kwenye mauzo mabingwa hao wa soka nchini, watatakiwa kupata Sh1 bilioni, hatua ambayo inaifanya Azam kutakiwa kufanya biashara itakayohusisha fedha nyingi zaidi ya hizo ili kuona faida ya kuwa na kiungo huyo.
Azam kama itamuuza nje ya Tanzania kiungo huyo, kipengele hicho hakitafanya kazi lakini bado Yanga itapata fedha zake kwani kuna mgao wa asilimia itaupata kwenye dau la mauzo hayo.
Hata hivyo, kipengele hicho kinawapa urahisi Yanga, kwamba kama wao watahitaji kumnunua Fei Toto, watakwepa kutumikia kifungu hicho lakini kama watamuhitaji sasa watahitajika kulipa Dola 500,000 (Sh1.3 bilioni) ili kumpata kiungo huyo fundi.

WASAUZI WAMO
Klabu pekee iliyowasilisha ofa rasmi Azam ya kumtaka Fei Toto ni Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na kiungo huyo ndiye anayetamani kwenda kuungana na kocha wake wa zamani Nasreddine Nabi, ambaye waliwahi kufanya kazi wote wakiwa Yanga.
Fei Toto ana urafiki mkubwa na Nabi na anataka kwenda kuungana na kocha huyo Mtunisia lakini Mwanaspoti linafahamu wazi Kaizer maarufu kwa jina la Amakhosi, ndiyo klabu pekee iliyothubutu kukaa mezani na Azam kuomba kuuziwa kiungo huyo.
Kwenye ofa ya Amakhosi, imeweka dau mpaka kiasi cha zaidi ya Dola 300,000 (Sh 804 milioni) kununua mkataba wake pale Chamazi lakini kiasi hicho bado kimekataliwa.
MUDATHIR AZAM FC
Wakati taarifa za Fei Toto kudaiwa kuugomea mkataba mpya wa Azam, taarifa zaidi zinaeleza kuwa tayari mabosi wa klabu hiyo wameanza mazungumzo ya kumrejesha kikosi kiungo aliyewahi kuitumikia timu hiyo, Mudathir Yahya aliyepo Yanga kwa misimu miwili sasa.
Mudathir alijiunga na Yanga katika dirisha dogo la usajili akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Azam, kisha kukaa nusu msimu bila kucheza popote zaidi ya kufanya mazoezi na KMKM kabla ya Yanga kumuibukia visiwani humo na kumsajili.
Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa mchezaji huyo kimeliambia Mwanaspoti, Azam imerudi kufanya mazungumzo na kiungo huyo wakiweka dau nono la usajili ambalo hawezi kulikataa.
“Ni kweli Azam wameomba kuzungumza na Mudathir kwa ajili ya kumsainisha mkataba ambao ni wa miaka miwili wenye dau nono, nafikiri ni mara mbili ya pesa ambayo Yanga wanataka kumpa ili aweze kubaki,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Matajiri wa Dar es Salaam wapo tayari kufanya chochote ili kumrudisha Mudathir Chamazi na mambo yanaenda vizuri, kilichobaki ni Mudathir kukunjua nafsi kutokana na namna walivyoachana awali.”
Mwanaspoti lilimtafuta Mudathir, ili kufafanua juu ya taarifa hiyo, alithibitisha ni kweli mkataba alionao na Yanga unamalizika mwisho wa msimu huu, lakini hawezi kuzungumza mambo yoyote ambayo hayaihusu timu yake ya Yanga.
“Ni kweli mkataba wangu unamalizika mwisho wa msimu huu, lakini kwa sasa mimi bado ni mchezaji wa Yanga. Naomba kuulizwa kuhusu timu ambayo naitumikia sasa, juu ya timu hizo nyingine ni tetesi tu.”