Mastaa KenGold wapewa mchongo

Muktasari:
- KenGold ipo mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 16, ikitokea ikashinda mechi tatu dhidi ya Pamba Jiji, Simba na Namungo itafikisha pointi 25 ambazo haziwezi kubadilisha uhalisia wa kushuka daraja.
KOCHA wa KenGold, Omary Kapilima amesema ingawa hakuna kitu kitakachobadilika katika mechi tatu zilizosalia kumaliza msimu huu, lakini ni fursa kwa wachezaji kuonyesha viwango bora.
KenGold ipo mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 16, ikitokea ikashinda mechi tatu dhidi ya Pamba Jiji, Simba na Namungo itafikisha pointi 25 ambazo haziwezi kubadilisha uhalisia wa kushuka daraja.
Kapilima alisema: “Kushuka kwa timu siyo kushuka kwa viwango vya wachezaji. Soka ni kazi yao wanapaswa kupambana hadi dakika ya mwisho bila kujali watavuna kitu gani.
“Kazi ya mchezaji ni kucheza haijalishi KenGold imeshuka, bado kazi yao itabaki palepale. Nafahamu namna inavyoumiza kupata matokeo kama hayo ila hatuna budi kuyapokea na kuendelea kusonga mbele,” alisema Kapilima.
Alisema anafanya kazi kubwa ya kuwajenga kisaikolojia ili morali zao zisishuke, akiamini kuna nyakati watapata muda wa kufurahia kama ilivyo kwa timu nyingine zilizofanya vizuri msimu huu. “Ni kweli ni ngumu kwa mchezaji timu imeshuka halafu bado wana mechi mbele yao, lakini inatakiwa kuwajenga na kuwasisitiza kucheza kwa kiwango cha juu kwani hiyo ni kazi yao lazima wakabiliane na changamoto kama hizo,” alisema.
Kapilima alipewa jukumu la kuinoa timu hiyo Oktoba 22, 2024 akiziba nafasi ya Fikiri Elias aliyeondoka Septamba 17, 2024.