Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wawakilishi waibana Serikali kilimo cha kisasa, viwanda, wakipitisha bajeti ofisi ya OMPR

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Hamza Hassan Juma (katikati), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Afya, Dk Saada Mkuya (kulia) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Talib Mwinyi Haji wakiandika baadhi ya hoja zinazotolewa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati wa mjadala wa hotuba ya makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Barazani Chukwani Unguja Zanzibar

Muktasari:

  • Wamesema sekta hizo zimeporomoka kwa kiwango kidogo mwaka 2025 kutokana na changamoto za pembejeo, teknolojia na mifumo. Serikali imeahidi kufanyia kazi hoja zilizotolewa, huku Baraza likipitisha bajeti ya Sh135.676 bilioni kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wameitaka Serikali kuongeza nguvu katika kilimo cha kisasa na ujenzi wa viwanda, ili kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi.

Wito huo umetolewa wakati wa kupitishwa kwa makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar (OMPR), ambapo wawakilishi hao wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha sekta za uzalishaji ili kuongeza tija ya uchumi wa Zanzibar.

Awali, akiwasilisha makadirio hayo jana, Jumatano Mei 6, 2026, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alisema kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar mwaka 2025 imefikia asilimia 7.0 ikilinganishwa na asilimia 7.1 mwaka 2024.

Alisema kupungua huko kwa asilimia 0.1 kumesababishwa na kushuka kwa ukuaji wa sekta ya kilimo, inayojumuisha mazao, mifugo, misitu na uvuvi, kutoka asilimia 24.3 mwaka 2024 hadi asilimia 23.5 mwaka 2025.

Aidha, alisema sekta ya viwanda nayo imepungua kutoka asilimia 20.2 mwaka 2024 hadi asilimia 19.3 mwaka 2025. Sekta hiyo inajumuisha uchimbaji wa mawe na mchanga, ujenzi, umeme na gesi, uzalishaji viwandani pamoja na usambazaji wa maji safi na udhibiti wa maji machafu.

Wakichangia mjadala wa bajeti hiyo leo, Alhamisi Mei 7, 2026, baadhi ya wawakilishi hao wa Baraza wameitaka Serikali kuongeza kasi ya kuimarisha sekta za kilimo na viwanda.

Mwakilishi Jaku Hashim Ayoub amesema Serikali inapaswa kusimamia kwa karibu upatikanaji wa mbolea na dawa za kilimo, akieleza kuwa pamoja na kilimo kutajwa kuwa mkombozi wa uchumi, bado hakijapewa kipaumbele kinachostahili.

“Masuala ya mbolea na dawa bado ni changamoto, hivyo tunapaswa kufikia hatua ya kuyaangalia kwa uzito zaidi,” amesema.

Kwa upande wake, Said Ali Mbarouk amesema Serikali lazima iweke mikakati imara kuhakikisha sekta ya kilimo inaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar.

Naye Abdulghan Ismail Zubeir amesema ni muhimu kwa Serikali kuwezesha matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kilimo badala ya kuendelea kutegemea kilimo cha kawaida.

Amesema matumizi ya teknolojia yataongeza uzalishaji wa chakula na kusaidia kupunguza gharama za bidhaa kupitia maendeleo ya viwanda.

“Nashauri Serikali iendelee kutoa ruzuku ili kupunguza gharama za bidhaa na kuongeza jitihada katika sekta ya utalii ili mapato yaongezeke,” amesema.

Akichangia mjadala huo, Mwakilishi Mohamed Ali Suleiman wa Chama cha ACT-Wazalendo amesema bajeti ya ofisi hiyo ina upungufu, hususan katika maoteo ya kifedha ambayo amesema hayana uwiano.

“Inashangaza kuona makadirio yaliyowekwa katika bajeti zilizopita yanatofautiana mara kwa mara. Unajiuliza sababu ni nini, ilhali Serikali ni moja,” amesema.

Ameongeza kuwa baadhi ya maeneo ya bajeti hayana viashiria vya utekelezaji, jambo alilosema ni dosari kubwa katika upangaji wa bajeti za kisasa.

Akijibu hoja hizo, Waziri wa Fedha na Mipango, Juma Malik Akil, amekiri kuwepo kwa changamoto hizo na kueleza kuwa zinatokana na matatizo ya mifumo, huku akiahidi kuwa Serikali itazifanyia kazi.

Kwa upande wake, Sulubu Kidongo Amour ameiomba Serikali kuchukua hatua dhidi ya Hospitali ya Kivunge na Hospitali ya Matemwe kwa madai ya kuwarejesha wagonjwa nyumbani kutokana na changamoto za mifumo ya huduma.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, na Kaimu Waziri wa Afya, Saada Mkuya, amekiri kuwepo kwa changamoto kwa baadhi ya watendaji, lakini akasisitiza kuwa si dhamira ya Serikali kuona wananchi wakikosa huduma.

“Kwa kweli hili halikubaliki. Kuwarejesha wagonjwa nyumbani kwa sababu ya mtandao si jambo linalopaswa kutokea. Tunakiri bado kuna changamoto kwa baadhi ya watendaji wetu, lakini tutalifanyia kazi,” amesema.

Kuhusu hoja ya ukuaji wa uchumi kutokuonekana moja kwa moja katika maisha ya wananchi, Dk Saada amesema wananchi wanapaswa pia kutumia fursa za kiuchumi zilizopo, ili kuongeza kipato chao.

Amesema bado kuna changamoto ya baadhi ya vijana wa Zanzibar kudharau kazi zinazopatikana katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa visiwani humo.

“Ili mwananchi afaidike na ukuaji wa uchumi, lazima naye ajishughulishe kutafuta kipato. Bado kuna kasumba kwa vijana wetu kudharau kazi, hivyo ni wajibu wetu kutoa elimu kwa wananchi,” amesema.

Akihitimisha mjadala huo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali itafanyia kazi hoja na ushauri wote uliotolewa na wajumbe wa Baraza, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda amani na utulivu nchini.

“Serikali itaendelea kulinda amani kwa gharama zote,” amesema.

Baraza hilo limeidhinisha jumla ya Sh135.676 bilioni kwa ajili ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Kati ya fedha hizo, Sh25 bilioni ni kwa mishahara, Sh59.867 bilioni kwa matumizi mengineyo na Sh40 bilioni kwa miradi ya maendeleo, huku makusanyo yakikadiriwa kufikia Sh60.132 milioni.