Watoto 374 wafanyiwa ukatili Zanzibar

Muktasari:

  • Takwimu za ukatili wa kijinsia na udhalilishaji Zanzibar zinaonyesha asilimia zaidi ya 80 ya matukio yaliyoripotiwa kati ya Februari hadi Aprili 2024 yalikuwa dhidi ya watoto

Dar es Salaam.  Watoto 374 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia na udhalilishaji visiwani Zanzibar ndani ya miezi mitatu huku usiri na kumalizana kindugu ukitajwa kuwa sababu ya kuchochea matukio hayo. 

Hiyo ni kutokana na watekelezaji wa vitendo hiyo kutochukuliwa hatua za kisheria jambo linalowafanya kuendelea kutekeleza vitendo hivyo sehemu nyingine. 

Takwimu za ukatili wa kijinsia na udhalilishaji Zanzibar zinaonyesha asilimia zaidi ya 80 ya matukio yaliyoripotiwa kati ya Februari hadi Aprili 2024 yalikuwa dhidi ya watoto huku ubakaji ukiendelea kuwa kinara. 

Takwimu hizo zilizotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar (OCGS) zinaonyesha jumla ya matukio 148 yaliripotiwa Aprili, 2024  waathirika 128 walikuwa watoto sawa na asilimia 86.5. 

Katika matukio hayo wanawake walikuwa 16 na wanaume walikuwa wanne. Kati ya watoto walioathirika wasichana walikuwa 108 na wavulana 20. 

Machi mwaka huu haikuwa nzuri kwa watoto kwa kuwa katika matukio 125 ya yaliyoripotiwa asilimia 81.6 ya waathirika walikuwa ni watoto, wanawake asilimia 13.6 na wanaume asilimia 4.8.

Katika watoto walioathiriwa, wasichana walikuwa 84 na wavulana walikuwa 18. 

Kadharika Februari, jumla ya matukio 175 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yaliripotiwa yakiwa na waathirika 176 na asilimia 83 wakiwa ni watoto. 

Wanawake walikuwa asilimia 13 na wanaume asilimia 4. Katika watoto hao wasichana walikuwa 123 na wavulana 23. 

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mkurugenzi wa Tasisi ya Zanzibar Women Recognition Awards, Hadia Abdallah Othman amesema licha ya jitihada kubwa zinazofanyika katika kumaliza suala hilo, matunda hayaonekani kwa sababu wanaofanya vitendo hivyo ni watu wa karibu na familia. 

Amesema mtu karibu na familia akitekeleza ukatili wa kijinsia inakuwa ngumu kwa wazazi kuripoti tukio hilo na kutoa ushirikiano kwa kile alichokieleza kuwa, wakati mwingine ni kuepusha aibu kwa familia. 

“Mtu anaona aibu kuwa mtoto kabakwa na kaka yangu, kabakwa na mjomba wangu, anaona aibu, inafichwa bila kujua mtoto ndiyo anaathirika zaidi kwa kukosa haki,” amesema Hadia. 

Amesema hali hiyo imefanya kuendelea kuwapo kwa vitendo hivyo kwani wanaotekeleza jambo hilo ni walewale na hawaripotiwi.

“Hii ndiyo inafanya kadri yanavyopigwa vita ndiyo yanaongezeka,” amesema Hadia. 

Mkurugenzi Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ofisi ya Zanzibar, Dk Mzuri Issa amesema wakati mwingine kuwapo kwa ongezeko la matukio yanayoripotiwa kunatokana na elimu iliyotolewa. 

“Zamani yalikuwa hayaripotiwi tofauti na sasa na watu wamezoea kuyafanya mambo haya bila kuripotiwa na kujenga ile dhana kuwa naweza kufanya hivi na nikatoka,” amesema Dk Mzuri.

Amesema miongoni mwa vitu vinavyochangia watoto kuathiriwa na matukio hayo ni kutojua namna ya kujilinda huku utawandawazi na matumizi ya mitandao ikiwafanya kuangukia katika kuangalia picha zisizofaa.


Matukio yanayoongoza

Wakati watoto wakiwa waathirika wakubwa, ubakaji ndiyo unaongoza kwa kuripotiwa kwa kaiasi kikubwa dhidi ya matukio mengine. 

Katika matukio yaliyoripotiwa Aprili mwaka huu kubaka yalikuwa 77 huku waathirika 70 wakiwa wasichana na saba 7 wanawake. Matukio ya kulawiti yalikuwa 13 na waathirika 12 walikuwa wavulana na mmoja ni mwanamume. 

Matukio ya kuingiliwa kinyume na maumbile manne waathirika wote wakiwa wasichana. 

Matukio mengine ya kutorosha ni saba, shambulio la aibu/kukashifu 19 na shambulio 28. 

Maeneo yanayoongoza

Kwa mujibu wa OCGS Wilaya ya Magharibi “A” imeripotiwa kuwa na matukio mengi ikilinganisha na wilaya nyingine, matukio 40 yalirekodiwa ikifuatia wilaya ya Mjini ambapo yameripotiwa matukio 34. 

Wilaya ya Kusini imeripotiwa kuwa na idadi ndogo ya matukio, tukio moja, ikilinganishwa na wilaya nyingine. 

Hata hivyo, idadi ya matukio yaliyoripotiwa Aprili mwaka huu ni ongezeko kwa asilimia 18.4 ikilinganishwa na matukio 125 yaliyokuwapo Machi, 2024. 

Aidha, matukio yote yameripotiwa kuongezeka isipokuwa matukio ya kuingilia kinyume na maumbile na shambulio la aibu. 

Tunatokaje

Hadia amesema moja ya njia inayoweza kusaidia kutokomeza hali hiyo ni kuielimisha jamii ili waweze kuripoti matukio hayo yanapotokea ili haki itendeke. 

Dk Mzuri amesema miongoni mwa njia za kukomesha tabia hizo ni kudhibiti mianya ya rushwa na kuweka mifumo mizuri inayowezesha baadhi ya watu kesi zao kushindwa kushughulikiwa kwa wakati na wengine kutojua wataripoti wapi. 

“Pia, kulea watoto vizuri kuwafundisha kutumia mitandao vizuri, kutoa elimu kwa wazee juu ya malezi, kuangalia mifumo ya waganga wa kienyeji ili waweze kufanye kazi kwa taaluma na si kupotosha watu kwa masuala mbalimbali,” amesema Dk Mzuri.

Serikali

Alipozungumza na Mwananchi Digital, Machi mwaka huu, Mkuu wa Divisheni ya Watoto, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Zanzibar, Mohammed Jabir amesema jukumu kubwa linalofanyika ni kuhakikisha uwajibikaji unaangaliwa kwa jumla kuanzia ngazi ya familia, jamii na kila mtu afanye analopaswa kuwajibika nalo.

Amesema kwa upande wa jamii na familia wanapokumbana na tatizo hilo jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wanatoa taarifa katika vyombo vya sheria na kutoa ushirikiano kwa vyombo hivyo.

“Vyombo vya sheria havina miujiza, vyombo vipo hivyo ni jukumu la wanafamilia kuvitumia kuonyesha kwa namna gani wanapambana na vitendo hivyo,” amesema Jabir. 

Kuendelea kutolewa kwa elimu kwa umma juu ya madhara ya vitendo hivyo imetajwa kuwa njia moja wapo ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji. 

“Wakati mwingine inaweza kuwa ngumu mtu kuja kuripoti tukio lake na kuhitaji faragha zaidi, wanaweza kutumia namba 116 inakupa nafasi ya kutoa taarifa yako,” amesema Jabir.