Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SMZ yajibu hoja za ACT-Wazalendo ujenzi Uwanja wa Ndege Pemba

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Muhamed akizungumza wakati wa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya tuhuma za ujenzi wa miradi inayotekelezwa na wizara hiyo. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi imesema hoja zinazotolewa zinalenga kuichonganisha Serikali na wananchi.

Unguja.  Wakati Chama cha ACT-Wazalendo kikirusha shutuma kwa Serikali kuhusu ubadhirifu wa miradi ya barabara na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Pemba, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi imejibu tuhuma hizo ikisema wanaotoa taarifa hizo wana lengo la kuichonganisha Serikali na wananchi.

Kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara inayofanywa na chama hicho Unguja na Pemba, viongozi wake wamekuwa wakitoa tuhuma kuhusu kuhujumiwa kwa miradi hiyo.

Makamu Mwenyekiti ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa alitaja kukwama kwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege Pemba ni kutokana na uingiliaji wa kisiasa wa mikataba kati ya kampuni zinazoshughulikia mradi huo.

Juni 2023, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) iliingia mkataba wa Dola 428 milioni za Marekani (Sh1.01 trilioni) na UK Export Financing kupanua Uwanja wa Ndege wa Pemba na kujenga mitandao ya barabara Unguja na Pemba.

Hata hivyo, Januari 10, 2024 Mahakama Kuu ya Zanzibar ilitoa amri za muda kusimamisha maendeleo ya mradi kusubiri utatuzi wa mgogoro wa kisheria kati ya kampuni hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 8, 2024 ofisini kwake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed ametoa ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo akiwataka wananchi kupuuza upotoshaji aliouita wa kisiasa.


Wete -Chake Chake

Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Wete – Chake Chake amesema ni miongoni mwa barabara tatu zilizopangwa kujengwa kwa kiwango cha lami kupitia mkopo nafuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Saudi Arabia na Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Uchumi Afrika (Badea).

Awamu ya kwanza ya utekelezaji wake ilihusisha ujenzi wa barabara ya Wete - Gando (kilomita 11) na barabara ya Wete - Konde (kilomita 15).

Ujenzi wa barabara hizo amesema ulitekelezwa kupitia mkandarasi Kampuni ya Mecco na ulikamilika mwaka 2013. Awamu ya pili ya mradi huo amesema ni ujenzi wa barabara ya Chake Chake - Wete yenye urefu wa kilomita 22.1.

“Mkataba wa mkopo kwa barabara hii ya Chake –Wete ulisainiwa Saudi Fund Aprili 19, 2020. Kiutaratibu, utekelezaji wa mradi huanza baada ya kukamilika kwa masharti ya awali ya kuanza kwa matumizi ya fedha za mkopo,” amesema.

Amesema Wizara ya Miundombinu, Mawasiliano na Usafirishaji kwa wakati huo iliingia mkataba na Kampuni ya Mecco Februari 14, 2022 baada ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kutimiza masharti ya awali.

“Mkataba wa Mkandarasi Mecco ni wa muda wa miezi 30 na unatarajiwa kumalizika ifikapo Agosti 14, 2024,” amesema.

Amesema hadi muda wa utekelezaji wa mkataba wa mradi huo unakamilika, utekelezaji halisi (physical progress) hadi kufikia Juni, 2024 ni chini ya asilimia 30.

Miongoni mwa changamoto zilizoonekana katika utekelezaji wa mradi huo amesema ni uchache na uchakavu wa vifaa na uhaba wa wafanyakazi na wataalamu wa mkandarasi.

Amesema tuhuma zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa hazina msingi na ukweli wowote, kwani hata wananchi wanaoishi na kutumia barabara hiyo wanaziona changamoto za mkandarasi huyo.

“Madai kwamba mkandarasi huyu alikataliwa asipewe kazi kwa sababu kuna watu walitaka wapewe chao ni ya upotoshaji, uzushi na yenye nia ya kuchafua na kuwagombanisha wananchi na Serikali yao,” amesema Dk Khalid.


Kucheleweshwa malipo

“Tunaomba ifahamike kwamba, taratibu za malipo kimkataba kwa mkandarasi huanza kwa kulipwa malipo ya awali,” amesema.

Amesema malipo hayo yalifanyika kikamilifu kwa mujibu wa mkataba, na madhumuni yake ni kumwezesha mkandarasi kuanza maandalizi ya awali ya utekelezaji wa mradi ikiwamo uletaji wa vifaa na wataalamu.

Amesema hadi muda wa utekelezaji wa mradi huo unamalizika mkandarasi ameshindwa kukamilisha utekelezaji wa kipengele hicho na bado aliendelea kulipwa malipo ya pili.

Hivi karibuni akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi kisiwani Pemba, Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla alitembelea mradi huo huku mkandarasi akieleza ucheleweshaji wa malipo ni miongoni mwa changamoto.

Hemed alitoa onyo kwa mkandarasi huyo iwapo akishindwa kwenda na matakwa ya mkataba atakuwa amejifukuzisha kupata zabuni Zanzibar.

Waziri Khalid amesema malipo ya tatu yalichelewa kulipwa kwa siku 160 baada ya Saudi Fund na Badea kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi.

“Hivyo, Serikali inapenda ieleweke kwamba ucheleweshaji huu haukutokana na Serikali bali ulitokana na mlipaji kutoridhishwa na utendaji wa mkandarasi,” amesema.

Waziri Khalid amesema malipo ya tatu yalifanyika baada ya ujumbe kutoka Saud Fund na Badea kufika Zanzibar Desemba, 2023 kutembelea eneo la mradi na kufanya mkutano na menejimenti ya wizara na hatimaye kufikia makubaliano ya kimaandishi ya kurekebisha kasoro zilizobainika.

Amesema malipo ya tatu yalifanyika kati ya Januari na Februari, 2024, akieleza yaliyosalia ni malopo ya nne.


Malipo ya fidia

Kuhusu malipo ya fidia kwa vipando na nyumba za wananchi, amesema si tatizo kwani asilimia 95 ya wananchi wote wanaostahiki kulipwa fidia wameshalipwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za malipo ya fidia.

Amesema eneo la mradi ambalo limeshalipwa fidia linatosha kwa mkandarasi kulifanyia kazi kwa zaidi ya asilimia 90.

Kuhusu uwanja wa ndege, Dk Khalid na wabia wamekubaliana kuweka tofauti zao kando na kukubaliana ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Pemba ufanywe na Kampuni ya PROPAV kupitia makubaliano yao ya Aprili 18, 2024 yaliyoshuhudiwa na Wizara za Fedha za SMT na SMZ na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi SMZ.

Amesema kinachoendelea ni kukamilisha taratibu za mwisho ili ujenzi wa mradi uanze.

Akizungumzia Barabara ya Tunguu – Makunduchi na ya  Mkoani – Chake Chake, amesema hizo pamoja na ya Fumba – Kisauni (kilomita 12) ziliombewa mkopo kutoka UKEF kupitia dhamana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema zilikuwa zijengwe kwa ubia baina ya Kampuni ya PROPAV na Mecco lakini kutokana na kutoelewana kwa wabia hao walikubaliana Mecco wajenge Barabara ya Tunguu – Makunduchi na Barabara ya Fumba – Kisauni.

Amesema PROPAV kwa vile watakuwa Pemba kwa ujenzi wa uwanja wa ndege pia wajenge Barabara ya Mkoani – Chake Chake.

Amesema fedha za malipo ya awali kwa ujenzi wa barabara hizo zilikwishalipwa kwenye akaunti ya ubia iliyopo Benki ya CRDB.

“Napenda kuwahakikishia kwamba, miradi yote miwili Uwanja wa Ndege Pemba na barabara itatekelezwa kama ilivyopangwa na hakuna taarifa yeyote ya kusitishwa utekelezaji wa miradi hii,” amesema.