Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Petroli yapanda, dizeli ikishuka Zanzibar

Muktasari:

  • Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura) imetangaza bei za mafuta ya dizeli na petrol ambazo zitaanza kutumika kesho Jumatatu, Septemba 9, 2024.

Unguja. Bei ya mafuta ya petroli imepanda huku dizeli ikishuka kisiwani Zanzibar sababu zikitajwa ni kuongezeka na kupungua kwa gharama katika soko la dunia.

Bei ya petroli imepanda kutoka Sh3,062 kwa lita moja hadi kufikia Sh3,164 ikiwa ni tofauti ya Sh102 sawa na asilimia 0.75.

Dizeli kwa Septemba 2024 itauzwa kwa Sh3,247 kutoka Sh3,259  ikiwa ni tofauti ya Sh12 sawa na asilimia 0.37. Bei hizi zinaanza kutumika kesho Jumatatu, Septemba 9, 2024.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), mafuta ya ndege nayo yamepungua bei ambapo yatauzwa Sh2,837 ikilinganishwa na Sh2,843 ya Agosti 2024 ikiwa ni tofauti ya Sh6 sawa na asilimia 0.21, huku mafuta ya taa yatauzwa kwa bei ileile ya Sh3,200.

Akitangaza bei hizo leo Jumapili Septemba 8, 2024, Meneja Kitengo cha Uhusiano Zura, Mbaraka Haji ametaja sababu za kupungua na kuongezeka kwa bei hizo ni kutokana na gharama za mafuta katika soko la dunia, za uingizaji wa mafuta pamoja na mabadiliko ya fedha za kigeni.

“Sababu nyingine ni gharama za usafiri, bima na premium hadi Zanzibar, kodi, tozo za Serikali na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja,” amesema Mbaraka.

Kwa sasa Zanzibar inapokea mafuta kupitia Bandari ya Tanga na Dar es Salaam kuhifadhi katika bohari ya Maruhubi iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi yenye  uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 21.

Wakati bohari hiyo ikiwa na uwezo huo, matumizi ya mafuta Zanzibar ni kati ya lita za ujazo milioni 30 hadi 40 kwa mwezi, huku kukiwa na vituo vya mafuta zaidi ya 100.

Baadhi ya watumiaji wa nishati hiyo wamesema punguzo hilo sio dogo lakini ni vyema kukawa na mipango mathubuti ya kuwa na vituo vya kuhifadhi mafuta mengi.

“Tukiwa na mafuta angalau ya miezi sita itapunguza hili la kuwa inabadilika kila mara kwani watu watahifadhi na pindi bei zitakapokuwa zinabadilika kwenye soko la dunia,  huku tunakuwa na ziada ambayo itatupa unafuu,” amesema Abdulla Ameir mkazi wa Magogoni.

Hata hivyo, Mbaraka amesema wanapanga bei kila mwezi kwa sababu zabuni hiyo inanunuliwa kimataifa inayotangazwa kwa Tanzania nzima na nchi jirani ambayo huletwa kila mwezi.

“Mafuta yetu Zanzibar yapo katika Zabuni hiyo kwa sababu ya kupunguza gharama na ndio tunapata unafuu wa bei,” amesema.