Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miradi mikubwa ya barabara inavyoifungua Zanzibar

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Maziwang’ombe Wilaya ya Micheweni alipotembelea eneo la uwekezaji na kuona utekelezaji wa agizo lake la ujenzi wa barabara katika eneo hilo Mkoa wa Kaskazini Pemba, Agosti 31, 2021. Picha na Maktaba

Unguja. Pamoja na viashiria vingine, kiwango cha maendeleo ya taifa lolote kinapimwa kwa kuzingatia miundombinu yake hususani barabara na kushamiri kwa majengo ya makazi na biashara.

Mtandao mkubwa wa barabara hurahisisha shughuli nyingi kwa kuunganisha mifumo mingine na hivyo kukuza uchumi na maendeleo ya kijamii.

Kwa eneo kama Zanzibar ambako utalii ni miongoni mwa shughuli kubwa za kiuchumi, miundombinu imara husaidia kukuza sekta hiyo. Wageni wanaotembelea nchi hiyo hujisikia huru zaidi pindi wanapokutana na miundombinu isiyochosha.

“Zanzibar inategemea zaidi watalii, lakini kama hakuna miundombinu mizuri na wenyewe hupungua. Kawaida mtalii anapenda kustarehe, hivyo huwezi kumzungusha kwenye gari kutwa nzima kutokana na ubovu wa barabara,” alisema Hashim Ali, dereva visiwani Zanzibar.

Ali ambaye pia ni mdau wa utalii, alisema kuna uhusiano mkubwa kati ya utalii na miundombinu imara kwa sababu mgeni anapofika uwanja wa ndege anaanza kutumia magari, si tu kwa ajili ya kutalii, bali hata kwenda sehemu ya kulala na hoteli nyingi za kitalii zipo pembezoni mwa mji, bila miundombinu imara hata sekta hiyo itakwama.

Mbali na kuunganisha sekta ya utalii, barabara nzuri zinaunganisha wavuvi na masoko na kurahisisha au kuharakisha ufikishaji sokoni bidhaa za kilimo.
Kwa kipindi kilichopita, ilikuwa nadra Zanzibar kuona vitu hivyo. Barabara za mji huo zilikuwa chakavu zenye mashimo na kutuamisha maji kipindi mvua zinaponyesha.

Hata hivyo, ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi miundombinu hiyo imebadilika, barabara za mjini na vijijini zimeanza kufumuliwa kufanyiwa matengenezo na nyingine mpya zikijengwa kwa kasi

 

Mtandao wa barabara

Zanzibar, ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 1, 344 ndani ya Unguja na Pemba. Takribani asilimia 60 za barabara hizo ni za viwango vya lami hata kama baadhi zimechakaa na asilimia 40 ni changarawe/kifusi.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, Dk Khalid Salum Muhamed akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu alisema katika kipindi cha miaka mitatu, Rais Mwinyi ameweka mkazo katika ujenzi wa barabara na zaidi ya kilometa 854 ziko katika ujenzi, kwenye hatua mbalimbali.

Kwa mujibu wa Dk Khalid, tayari zimeshatambuliwa kilomita zingine 208 ambazo zinatafutiwa fedha za ujenzi kwenye barabara zilizokuwa za lami lakini sasa zimechakaa.
Anazitaja barabara hizo kuwa ni inayoanzia Mwera kupitia Kizimbani, Mfenesini hadi Kwanyanya na inayoanzia Kidimni, Kiboje hadi Kitope.

“Ndani ya kipindi hiki cha Dk Mwinyi kuna mpango wa kujenga mtandao wa barabara zenye urefu wa zaidi ya kilomita 1000,” alisema

Kwa upande wa barabara za ndani zinajengwa kilomita 275.9, kati ya hizo, takribani ya kilomita 234 ni za Pemba ambazo zinajengwa na kampuni ya Iris kwa gharama ya Dola za Marekani 89.3 milioni (Sh223.7 bilioni).

Vilevile kuna mtandao wa barabara za mjini Unguja kilomita 100.9 ambazo gharama yake ni Dola za Marekani 116.131 milioni (Sh290.9 bilioni).
Katika ujenzi wa barabara hizo za Unguja ambazo mkandarasi anaendelea na kazi, zitahusisha ujenzi wa madaraja mawili ya juu katika mzunguko wa Mwanakwerekwe na mzunguko wa Amani.

Pia zitakuwa na taa za barabarani na vituo vya daladala ambavyo havikuwapo awali, badala yake magari hayo ya abiria yalikuwa yanashusha na kupandisha abiria katikati ya barabara na kusababisha usumbufu.

Pia kuna barabara ya Chake Chake hadi Wete, Pemba yenye urefu wa kilomita 22.1 nayo inajengwa kwa gharama ya Sh23 bilioni kwa kutumia Kampuni ya Meco Mwananchi.
Ukiachilia mbali barabara hizo, kuna zinazojengwa katika Bandari ya Mangapwani na kampuni ya Orkur ya Uturuki kwa Dola za Marekani 33 milioni ambayo ina urefu wa kilometa 12.
Kutokna na mazingira ya bandari, viwango vya ujenzi vya barabra hii vinakuwa juu zaidi ikilinganishwa na nyingine za kawaida.

Pia kampuni hiyo ya Uturuki inajenga barabara kutoka daraja la Dk Shein hadi Tunguu kilomita 23.2 kwa gharama ya Sh27 bilioni.

Kuna barabara nyingine ambazo mikataba yake imetiwa saini kama Tunguu hadi Makunduchi urefu wa kilomita 48, Fumba hadi Kisauni yenye urefu wa kilomita 12 na Mkoani hadi Chakechake Pemba yenye urefu wa kilomita 43 ambazo kwa pamoja zinajengwa kwa gharama ya Euro 230 milioni (607.24 bilioni).

Waziri Khalid alisema kuna barabara nyingine kilomita 277.7 zitajengwa na kampuni ya CCECC ya China kwa awamu ambapo awamu ya kwanza itajengwa kilomita 136 na itakuwa na Dola 126 milioni (Sh315.63 bilioni) wakati wowote ujenzi unaanza na awamu ya pili itafanyika baadaye.

Kuhusu maendeleo hayo ya barabara, Waziri Khalid alisema uchumi wa nchi yoyote ile unategemea miundombinu imara japo kuna baadhi ya watu wanabeza na kutoona umuhimu wake.

“Watu wengine hawafahamu na kusema yasiyo na maana, hivyo unapokuwa na muunganiko mzuri wa barabara unainua na sekta zingine za kijamii na kiuchumi. Kwa hiyo Zanzibar kama kisiwa, lazima tunganike na baada ya barabara hizi kukamilika Zanzibar itakuwa na sura nyingine tofauti,” alisema Dk Khalid.

Baada ya kuona jinsi barabara zinavyoifungua zanzibar, kesho Mwananchi litaendelea na kuiangazia safari ya siku 1,096 Dk Mwingi, usikose kufuatilia makala yanayofuata ili kufahamu mengi zaidi.