Mali za bima, ada zafikia Sh3.4 trilioni, Dk Mwinyi ataka ubunifu zaidi

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza baada ya kupokea taarifa ya utendaji wa soko la bima Tanzania hafla iliyofanyika Unguja
Muktasari:
- Katika kipindi cha mwaka 2022, mchango wa sekta ya bima katika pato la taifa ulikuwa kwa asilimia 1.99 na mwaka 2023 umekua hadi asilimia 2.01.
Wakati Mamlaka ya Bima Tanzania (Tira) ikiongeza undikishaji wa ada za bima kwa asilimia 7.4 kutoka Sh1.1 trilioni mwaka 2022 hadi kufikia Sh1.2 trilioni mwaka 2023, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametaka sekta hiyo kuongeza ubunifu na matumizi ya teknolojia ili kuendana na kasi ya serikali zote mbili ambazo zimejikita kuvutia wawekezaji wengi nchini.
Katika kipindi hicho, mchango wa sekta ya bima katika pato la taifa ulikuwa kwa asilimia 1.99 na mwaka 2023 umekua hadi asilimia 2.01.
Pia, mali za bima zimeongezeka kwa asilimia 26, kutoka Sh1.7 trilioni hadi kufikia Sh2.2 trilioni mwaka 2023 huku mali za uwekezaji zimeongezeka kwa asilimi 9.3 kutoka Sh1.1 trilioni hadi Sh1.28 trilioni mwaka 2023 kwa watu wengi kuendelea kuwekeza katika sekta hiyo.
Hayo yamebainika leo Februari 20, 2025 wakati wa kutoa ripoti ya soko la bima kwa mwaka 2023/24 kisiwani Unguja ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Mwinyi.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Kamishna wa Bima Tanzania, Dk Baghayo Saqware amesema kwa upande wa madai ya bima (malipo ya bima) yameongezeka kwa asilimia 25 kutoka Sh389 bilioni hadi Sh488 bilioni na kati ya madai hayo yaliyolipwa, kampuni za bima za kawaida zimelipa Sh408 bilioni na kampuni za bima za maisha zimelipa Sh79 bilioni.
“Bima za kawaida bado zinaoongoza kwa hiyo bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha bima za maisha nazo zinaongezeka,” amesema.
Katika eneo la ubakizaji wa ada za bima nchini, Dk Saqware amesema umeonesha mwenendo tofauti kati ya bima za kawaida na bima za maisha, wakati kiwango cha ubakizaji kwa bima za kawaida kikiongezeka kutoka asilimia 49.4 hadi kufikia asilimia 55.5, kiwango cha ubakizaji bima za maisha kimepungua kutoka asilimia 85.7 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 83.2 mwaka 2023.
Licha ya kiwango hicho kushuka, Dk Saqware amesema bado kinakubalika kwani wamejiwekea isipingue asilimia 80.
Hata hivyo, kwa upande wa bima ya kawaida amesema lengo lao kuhakikisha wanafikia asilimia 70 katika miaka ijayo.
“Ubakizaji unavyoongezeka ndipo na soko linatanuka na fedha nyingi zinakuwa kwenye mabenki na kuchangia uchumi na hali hiyo inaonesha kampuni za bima zinaweza kuhimili viwango hatarishi na kupunguza utegemezi kampuni za nje,” amesema.
Pia, amesema watoa huduma za bima wameongezeka kwa asilimia 33 kutoka watoa huduma 1,165 mwaka 2022 hadi kufikia watoa huduma 1,549 mwaka 2023 ambo wametoa ajira rasmi katika sekta hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 34.1 kutoka 4,000 mpaka 5,595.
Baada ya kupokea ripoti hiyo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema serikali zote mbili (SMT) na SMZ pamoja zina dhamira ya dhati kuleta maendeleo kwa wananchi kutokana na mageuzi makubwa yanayoendelea kufanywa katika sekta zote za uchumi nchini.
“Tumedhamiria kuvutia wawekezaji kwa kuweka mazingira wezeshi na taratibu bora za kiuwekezaji, kwa mantiki hiyo, ni lazima sekta ya bima iendane na kasi ya Serikali zetu kwa kujikita kwenye ubunifu na matumizi ya teknolojia,” amesema.
Ametumia fursa hiyo kuwataka watoa huduma za bima na wadau wote wa bima kufanya kazi kwa weledi na kwa ushirikiano.
“Kwa lengo la kuzidi kupiga hatua ya maendeleo katika uimarishaji wa sekta ya bima nchini ni vyema tukawa na mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hii kwa kuyaimarisha maeneo maalumu,”
Ameyataja maeneo hayo ni pamoja na mchakato wa kuwa na Sera ya Taifa ya Bima ukamilishwe kwa haraka ili kutoa dira ya taifa kwa kila sekta kuhusu matumizi ya Bima nchini.
Pia, mchakato wa kuwa na bodi ya wataalamu wa bima, hifadhi ya jamii nao ukamilishwe haraka ili kuwa na bodi itakayosimamia wataalamu wa sekta hiyo huku jitihada ziongezwe zaidi katika matumizi ya teknolojia, ubunifu wa bidhaa za bima, na utoaji wa elimu ya bima kwa wananchi.
Balozi wa Bima ambaye pia ni Katibu Mkuu kiongozi, Zena Said amesema ipo haja kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu bima ya tafakuli (bima inayofuata misingi ya kiislamu) kwani watu wengi bado hawana uelewa na bima hiyo.