Kampeni yazinduliwa kumlinda mtoto dhidi ya mitandao Zanzibar
Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrik Ramadhan Soraga akizungumza kuhusu uzinduzi wa kampeni maalumu ya kumlinda mtoto dhidi ya mitandao Zanzibar
Muktasari:
- Watoto 200,000 wenye umri wa miaka 12 hadi 17 wameathirika na changamoto mbalimbali za kihalifu katika mitandao ikiwemo udhalilishaji na kurubuniwa.
Unguja. Wakati kasi ya matumizi ya mitandao na utandawazi vikiongezeka, Zanzibar imezindua kampeni ya kumlinda mtoto dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao.
Hatua hiyo inakuja wakati Serikali ikiwa haina sheria wala kanuni ambazo zimeweka udhibiti wa kumlinda mtoto kwenye mitandao, hivyo kampeni hiyo itasaidia kuchukua hatua mbalimbali za kufanya hivyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Julai 9, 2026, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrik Ramadhan Soraga amesema watoto ni kundi ambalo ni rahisi kushawishika katika nadharia mbalimbali, hivyo lazima wawekewe tahadhari na ulinzi.
“Kwa sasa kasi ya matumizi ya mitandao yamekuwa makubwa kwa watoto, wakiwa shule, nyumbani hata katika mazingira mengine na hakuna udhibiti kwa hiyo kampeni hii inakwenda kutoa elimu na namna wazazi na walezi wanaweza kuwalinda watoto dhidi ya mitandao,” amesema.
Kutokana na matumizi mabaya ya mitandao, amesema kuna mambo mengi ambayo yanaibuka katika jamii hususani mwenendo wa tabia za watoto hasa na kuporomoka kwa maadili.
“Hivi sasa matumizi ya mtandao yamekuwa makubwa na watoto wetu wanajua kila kitu juu ya masuala mbalimbali hivyo ni lazima kuweka ulinzi kabla halijawa janga la kitaifa,” amesema Soraga
Amesema zipo nchi duniani kama Australia na Uingereza ambazo zimeweka sheria ambapo matumizi ya mtandao kwa mtoto ni kuanzia umri wa 16 na kuendelea.
“Sisi hatuna sheria hizo mtoto wa miaka 10 hadi 12 ana simu na anatumia mtandao na hakuna kitu kinachomlinda,”
Naye Mtaalamu wa Usalama na Uchunguzi wa Makosa ya Kidijitali Tanzania, Yussuph Kileo, amesema kampeni hiyo kwa Tanzania bara wameshaanza tangu mwaka 2024 na wanakwenda vizuri.
Amesema zipo takwimu zinazolisukuma taifa kulichukulia jambo hilo kwa uzito kwani zinaonesha asilimia 87 ya mmomonyoko wa maadili unasababishwa na ukuaji mkubwa wa utandawazi na hali hiyo inasababisha watoto kubadilika tabia.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, yapo matukio ambayo watoto hawapaswi kuyaona katika mitandao lakini wanayaona na kusababisha athari kwa ubongo wa mtoto.
“Asilimia 67 ya watoto wa Tanzania wapo katika mitandao na watoto 200,000 wenye umri wa miaka 12 hadi 17 wameathirika na changamoto mbalimbali za kihalifu katika mitandao, ikiwemo udhalilishaji na kurubuniwa,” amesema Kileo
Kutokana na hali hiyo, Kileo amesema ni muhimu taifa kuona namna gani watoto watajilinda na mitandao na kutoa taarifa pale wanapokutana na changamoto za kimtandao.
Mtaalamu huyo ameshauri ni vyema sheria, kanuni na taratibu zilizopo ziweze kupitiwa vizuri ili kuhakikisha zinakuwa na ulinzi wa watoto.
Katika kulitafutia ufumbuzi na kupunguza athari hizo, Kileo amesema kwa sasa Tanzania Bara kuna mjadala unaoendelea ili kuja na simcard maalumu kwa ajili ya watoto, ambazo zitakuwa hazina maudhui ambayo hayaendani na watoto.
“Tutashirikiana pande zote mbili kuhakikisha watoto wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa bara na Zanzibar wanalindwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zitakazokuwepo,” alisisitiza.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Serensic Afrika, Ester Mengi amesema kampeni hiyo ni muhimu kwani watoto wengi wanaathirika kwa kiasi kikubwa mitandaoni.
Kampeni hiyo ambayo haina muda maalumu, inakwenda sambamba na ujumbe maalumu unaosema “Ulinzi wa watoto mtandaoni ni jukumu letu sote chukua hatua”.
Mkurugenzi wa Usalama wa Mitandao na Ulinzi wa taarifa, Khalfan Mohamed Othman, amesema kampeni hiyo itakwenda wilaya na mikoa yote Unguja na Pemba kupitia shule na vyuo vya Qur-an ili kupata kundi kubwa la watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ili elimu iliyokusudiwa iwafikie wote.