Jinsi siku 1000 zinavyomsaidia mtoto kumkinga na maradhi 13
![](/resource/image/4916816/landscape_ratio2x1/320/160/fd4ed51efd98b34d4d4c187c71b6ef06/Cv/maradhi-pic.jpg)
Ofisa Programu wa mpango wa Taifa wa chanjo Tanzania, Lotalis Gadau akitoa taarifa za chanjo wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu chanjo kisiwani Zanzibar.
Muktasari:
- Mpango wa Taifa wa chanjo kwa upande wa Zanzibar ulianza mwaka 1985 kwa lengo la kuwakinga watoto, mama na jamii kwa ujumla dhidi ya maradhi yanayozuilika kwa chanjo ambapo hadi sasa maradhi 13 yanayozuilika yapo katika mpango huo ikiwemo polio, surua, rubella, pepopunda na dondakoo.
Unguja. Iwapo wazazi watazingatia malezi kwa siku 1000 za kwanza zitasaidia kumkinga mtoto na maradhi 13 ikiwamo kupunguza vifo vya mama na mtoto kisiwani Zanzibar. Imeelezwa
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar, Dk Salim Slim ambapo amesema siku hizo ni muhimu kwa makuzi ya mtoto, lakini wazazi wengi wanazipuuzia hivyo kusababisha athari kwa watoto.
Bila kutaja takwimu Dk Slim amesema Zanzibar ndio kitu kinachotokea wanawake wanazaa mara mbili kwa mwaka mmoja na ndio miongoni mwa sababu za vifo vya uzazi, ukondefu na lishe duni.
Bila mesema siku hizo ni kuanzia siku mama na baba walipoingiliana mpaka mtoto anafika miaka miwili.
Hata hivyo, amesema Wazanzibari wengi hawazingatii mpangilio huo na ndio maana wanazaa kila baada ya muda mchache.
"Moja kati ya vitu vinapelekea vifo ni hilo, kwa sababu hilo linaandaa uzazi wa mpango na uzazi wa mpango kwa Zanzibar haufuatiliwi, yaani hapa watu wanazaa kati ya Januari na Desemba mwaka huohuo,"
Amesema "Mtu akirudi kutoka siku za uzazi 40 anabeba mimba nyingine, sasa huo muda wa kujipanga na kumlea mtoto unatoka wapi, kwa hiyo ndio maana tunasema hivyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya afya na lishe ya mwaka 2022, asilimia 58 ya watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 19 wana utapiamlo.
Kwa mujibu wa mtaalamu hiyo, iwapo mtoto akilelewa kwa siku hizo, itamfanya mama ajielekeze zaidi katika malezi yake na kumpa huduma zote zinazotakiwa ikiwemo lishe na chanjo za kumlinda na maradhi kama surua, rubella na polio.
“Muhimu ni kuzingatia mtoto alelewe siku 1000 kuazia siku ya kupata ujauzito hadi miaka miwili bila mama kuzaa mtoto mwingine,” amesema Dk Slim Janauri 6, 2025 wakati wa semina ya siku mbili kwa waandishi wa habari kuhusu masuala ya chanjo.
“Kama tutafuata utaratibu huu hata tatizo la lishe, kuzaa watoto wadumavu na vifo vya mama na mtoto vitapungua, sababu moja ya kuwakosesha watoto chanjo ni kuzibeza siku 1000, endapo mama atabeba mimba ndani ya siku hizo matunzo yote yataelekezwa kwenye ujauzito na kupunguza huduma kwa mtoto alietangulia,” amesema.
Dk Slim amesema wazazi wengi hawapeleki watoto wao wakapata chanjo na wengine huwapeleka katika hatua za awali jambo linaloleta makuzi mabaya kwa watoto na wengine kupata magonjwa yanayozuirika.
Amesema katika mwaka 2022 Zanzibar ilipata mlipuko wa surua na kusbabisha vijana 16 kupoteza maisha na wengi wao wlaibainika hawakuwa wamechanjwa huku wengine walipata chanjo moja na wazazi kupuuza chanjo zingine.
Huduma za chanjo zinawalinda watoto na maradhi ya surua, rubella, polio na pepopunda huku zikileta nafuu na kupunguza gharama za matibabu na kupunguza vifo vya mama na watoto.
Dk Slim amesisitiza kwamba mitazamo potofu kuhusu chanjo, kama ilivyokuwa baada ya janga la Uviko-19, inachangia kutoelewa na kukubaliana na umuhimu wa chanjo.
Kutokana na hali hiyo Dk Slim amesema wakati wowote janga hilo linaweza kujirudia endapo jamii haitoachana na kupuuza dhana potofu dhidi ya chanjo kwa watoto wao.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, Serikali imewekeza kwenye sekta ya afya hasa katika masuala ya mama na mtoto kutokana na kuwa kundi hilo ndio linotengeneza rasilimali watu ya baadaye na kusisitiza kuwa ipo haja ya wananchi kuungana na Serikali ili kutimiza malengo.
“Tuna vituo 160 vyote vinatoa huduma za chanjo na kila mwezi tunaweka mabonanza ya kuhamasisha chanjo mara mbili wilaya zote ili kuwasogezea huduma wananchi.” Alisema Dk Slim.
Amesema Serikali imeandaa mifumo na mikakati ya kukabiliana na hali hiyo lakini kama jamii haitabadili mitazamo na mfumo wa maisha juhudi hizo hazitasaidia na kuwataka waandishi kutumia taaluma zao kubadilisha mitazamo na tabia za wananchi kwani nguvu yao ni kubwa na yenye kuleta mabadiliko chanya kwa haraka zaidi.
Ofisa Programu wa mpango wa Taifa wa chanjo Zanzibar, Ruzuna Abrahman amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa na kupata uwezo wa kuelimisha na kuhamasisha jamii katika kulipa umuhimu suala la chanjo ili kuimarisha mfumo wa afya na kukanusha upotoshaji unaojitokeza kutokana na chanjo katika jamii.
Amesema kwamba miongozo ya kuwashirikisha kina baba kushiriki katika malezi ya mimba na mtoto hadi ukuaji wake imeshaandaliwa na kuwataka waandishi kwa kutumia taaluma zao kuondoa dhana potofu dhidi ya chanjo zilizoibuka baada ya kuja ugonjwa wa korona.
Pia, amewashauri kina mama kuwahi kwenda kliniki wanapojibaini kuwa na ujauzito wakiongozana na wenza wao ili nao wapate elimu ya uzazi na ulezi pamoja na kufahamu umuhimu wa chanjo.
Mbali na hayo alihimiza kuwapeleka wasichana waliofikia umri wa miaka tisa kupata chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi ambayo imechukua nafasi ya juu ya magonjwa yanayozuiliwa na chanjo.
Akitoa taarifa ya chanjo kwa mwaka 2024, Ofisa Programu wa mpango wa Taifa wa chanjo Tanzania, Lotalis Gadau amesema wilaya tisa za Zanzibar zimefikia lengo la kitaifa la zaidi ya asilimia 95 isipokua Wilaya ya Magharibi B ambayo ina asilimia 94 na Mkoani yenye asilimia 90.
Amesema kumekua na changamoto nyingi wakati wa utoaji wa chanjo hiyo kutokana na walengwa kuamini taarifa potofu na uzushi zinazosambazwa na baadhi ya wanajamii kuhusu huduma za chanjo ikiwemo za watoto na kupelekea baadhi yao kususia na kuasi hata chanjo ya saratani ya kizazi.
Mbali na changamoto hizo, kupitia mpango huo wamefanikiwa kusambaza vifaa na chanjo kila wilaya, kufanya kampeni ya chanjo ya polio, surua, rubella kitaifa iliyofanyika kwa asilimia 95 na kupunguza magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Naye Meneja kitengo cha elimu ya afya, Hamad Bakari Magarawe amesema kuna baadhi ya maeneo kuna changamoto ya vituo vya afya lakini wengine wanashindwa kuchanja kwasababu ya kiimani hivyo inahitajika elimu kubwa kuhamasisha jamii.
Bila kutaja takwimu mtaalamu huyo amesema “vifo vingi tumevifuatilia tumegundua ni wale wanaochelewa kwenda kiliniki, Zanzibar ni ksiwa kidogo lakini bado maeneo mengi kiafya hayajakaa vizuri.”
Kwa mujibu wa Wizara ya afya, vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 542 mwaka 2021 hadi 421 mwaka 2022.