90 warejeshewa tabasamu kwa kupewa miguu bandia
Baadhi ya wananchi waliopewa miguu bandia bure wakifanya mazoezi ya kutembea katika hospitali ya Wilaya Mbuzini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Wataalamu kutoka Bangladesh na Nepal wamewapa miguu bandia na kuwawafundisha wataalamu wa ndani ambao wataendeleza huduma hiyo na kuwaunganishia watu wengine wenye uhitaji.
Unguja. Baada ya kupitia changamoto na kuwa tegemezi kwa muda mrefu kutokana na kukosa miguu, wananchi 90 wameeleza matumaini yao katika safari mpya ya maisha baada ya kupewa miguu bandia.
Faraja hiyo inakuja kupitia mradi wa Zanzibar 100 Limb Project, ambao ni matokeo ya ushirikiano kati ya Taasisi ya Naya Qadam Trust ya Uingereza na Zanzibar Global Health and Education Foundation (ZGHEF).
Kazi ya kuwapima na kuwapatia huduma hiyo imedumu kwa takribani mwezi mmoja, kuanzia Juni 1 hadi Julai 10, katika Hospitali ya Wilaya ya Mbuzini, Unguja.
Wakizungumza baada ya kupewa miguu hiyo leo Julai 10, 2026, baadhi ya wanufaika hao wameeleza namna walivyokuwa wakihangaika, huku wengine shughuli zao zikikwama, lakini sasa wamepata matumaini mapya baada ya kupatiwa miguu bandia.
Sehemu ya wananchi 90 waliopewa miguu bandia bure wakiwa wamekaa baada ya kumaliza kuunganishwa katika Hospitali ya Wilaya Mbuzini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja. Picha na Jesse Mikofu
Hashim Haji, mkazi wa Bububu amesema alipata ajali na kukatika miguu, hali iliyomfanya ashindwe kuendelea na shughuli zake za uzalishaji na kubaki kuwa tegemezi.
Amesema baada ya kupewa miguu bandia anaamini ataweza kujiendeleza kupitia shughuli za kiuchumi.
Naye Fatma Abdalla Juma, mwanafunzi wa kidato cha pili kutoka Pemba, amesema alipata tatizo la mguu lililosababisha ukatwe akiwa kidato cha pili, jambo lililomfanya ashindwe kuhudhuria vizuri masomo yake.
“Kupata mguu utanisaidia kwenda shule, chuoni na kufanya shughuli nyingine mbalimbali kwani nilipokatwa mguu ilikuwa changamoto kubwa,” amesema Fatma.
Akisimulia kilichosababisha mguu wake kukatwa, mwanafunzi huyo amesema alianguka akiwa shuleni, kisha akaanza kukandwa nyumbani, hali iliyosababisha maumivu kuongezeka.
Baadaye alipopelekwa Hospitali ya Micheweni aliambiwa mfupa umeharibika na alihitaji kukatwa mguu.
Naye Saleh Salim Khamis amesema baada ya kukatwa miguu yake alibaki kuwa mtu wa kuhudumiwa nyumbani, lakini baada ya kupatiwa miguu bandia sasa anaweza kutembea mwenyewe na kufanya shughuli za kujipatia kipato.
Akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mradi huo, Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu, Ali Omar, amesema watu wenye ulemavu hukumbana na changamoto nyingi, ikiwemo gharama kubwa za kupata miguu bandia.
“Kutokana na gharama hizo, watu wengi wenye ulemavu wameshindwa kumudu kupata miguu bandia, kwa hiyo hii ni faraja kubwa sana,” amesema.
Saleh Salim Khamis mkazi wa Bumbwini akionesha uwezo wake wa kupanda ngazi baada ya kupewa mguu bandia katika hospitali ya Mbuzini Mkoa Mjini Magharibi Unguja Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu
Mbali na gharama za miguu bandia, amesema bado kuna gharama za kufuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam.
“Hali hii imesababisha watu wenye ulemavu kuishi kwa kukata tamaa na kujiona kama mzigo kwa jamii, lakini leo mradi huu umeleta matumaini mapya leo ndugu zetu 90 wanaweza kusimama na kutembea kwa ujasiri,” amesema Omar.
Amesema ni faraja kwa wote kwani mradi huo haujaleta miguu tu, bali umerudisha utu, furaha, ujumuishi na uwezo wa kujumuika na jamii pamoja na kufanya kazi za kujitegemea.
Katibu wa ZGHEF, El'Jabir Shao amesema safari ya kutekeleza mradi huo ilikuwa ndefu, lakini wanashukuru kuona umefanikiwa licha ya kutofikia lengo la kuwapatia miguu bandia watu 100.
Hata hivyo, amesema bado kuna mwamko mdogo miongoni mwa watu wenye ulemavu wa kupambania haki zao.
“Haikuwa rahisi na haijawahi kufanyika, lakini tunamshukuru Mungu tumefanikiwa,” amesema.
Naye mratibu wa mradi huo, Zarina Jafferji, mzaliwa wa Zanzibar anayeishi nje ya nchi, amesema Wazanzibari wenye changamoto hiyo sasa watapata fursa ya kurejea katika hali zao za kawaida.
Wataalamu hao kutoka Bangladesh na Nepal, mbali na kuwapatia walengwa miguu bandia, pia wamewafundisha wataalamu wa ndani ili waendelee kutoa huduma hiyo kwa wengine zaidi.