WaterAid Tanzania: Huduma za maji safi, usafi wa mazingira katika vituo vya afya suluhisho la afya na ustawi bora wa watu
Kuelekea katika Mkutano wa Zama Zijazo unaotaraji wa kufanyika kwa siku mbili (Septemba 22-23, 2024), ambao ni kikao cha ngazi ya juu cha Umoja wa Mataifa, nchi wanachama walikubali ana kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu kwenye Mkutano Mkuu wa Kisiasa uliofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, July 8-18, 2024.
“Lazima tuendelee kutafuta masuluhisho yatakayowezesha kuboresha utekelezaji na mafanikio ya Malengo ya Maendeleo Endelevu,” amesema Rais wa Baraza la Uchumi na Jamii la Umoja wa Mataifa, Paula Narváez.
Kwa kuwa ajenda ya huduma za maji safi na usafi wa mazingira ni sehemu ya malengo ya maendeleo endelevu, ndiyo kusema Taasisi ya WaterAid Tanzania, ambayo imejipambanua kwa kusimamia upatikanaji wa huduma hizo kwa jamii za Kitanzania, inayo dhima ya kubwa ya katika uharakishaji wa utekelezaji wa malengo hayo.
Na wito huo wa Paula Narváez hauna ugumu wowote katika utekelezaji wake kwa kuwa tayari WaterAid Tanzania imeshadhihirisha hayo miaka 40 iliyopita namna gani imejidhatiti katika eneo hilo.
Nyuma ya mafanikio ya taasisi hiyo, upo mpango wake wa miaka mitano (2023-2028) ambao ulibuniwa kwa kuzingatia malengo ya maendeleo endelevu, hususan lengo namba 6 ambalo linasisitiza hitaji la kuhakikisha huduma za maji safi na usafi wa mazingira zinafikiwa na watu wote.
Kwa upande wa matokeo, katika kipindi chote cha WaterAid Tanzania imeweza kusaidia watu milioni 1.8 kupata maji safi na salama, huku kaya 800,000 zikipatiwa vyoo vyenye staha na watu milioni 26 wamehimizwa kutumia mbinu za usafi binafsi.
Huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika vituo vya afya zinavyochochea uboreshaji afya na ustawi wa watu
Ili kuchangia uboreshaji afya na ustawi wa watu kupitia uimarishaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika vituo vya kutolea huduma za afya, taasisi hiyo imehakikisha kuwa mkakati wake unatekeleza kikamilifu malengo ya kitaifa na kidunia yaliyojikita kuimarisha afya ya umma.
Kwa kupitia kufungamanisha mkakati wake wa miaka mitano na ule mpango wa WSDP-III, WAT imeweza kuweka mifumo ya huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika vituo vya kutolea huduma za afya 35 ili kuhakikisha huduma hiyo inatolewa katika utaratibu unaozingatia utu.
Hili linaenda sambamba na ufungaji wa miundombinu ya kunawia katika vituo vya kutolea huduma za afya na maeneo ya umma ili kuboresha usafi wa mikono, hatua inayolenga kukabiliana na magonjwa ya milipuko.
Nini kilitokea? vituo vya kutolea huduma za afya nchini vilipatiwa huduma za uhakika za maji safi na usafi wa mazingira. Na watu milioni 8.5 walifikishiwa huduma za maji safi na usafi wa mazingira. Jitihada ambazo zinatakiwa kuwa endelevu kufikia malengo ya uboreshaji afya na ustawi wa watu.
Kupitia mageuzi hayo ya huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika sekta ya afya, ni wazi taasisi hiyo imefanikiwa kuharakisha utekelezaji wa malengo namba 6 na 3 yanayohusiana moja kwa moja katika kuleta ustawi na kuimairisha afya za watu.
WaterAid Tanzania inatekeleza jukumu muhimu katika kusimamia uhusiano thabiti kati ya utekelezaji wa malengo namba (SDG 3) na utekelezaji wa malengo namba (SDG 6) kwa kuonyesha athari chanya za moja kwa moja ambazo huduma bora za maji na usafi wa mazingira katika vituo vya afya zinazo kwenye kuboresha matokeo ya kiafya.
Kuelekea katika mkutano huo wa siku zijazo, kama nchi, bado tunahitaji kuona lengo namba 6 linakuwa sehemu ya ajenda za msingi za mjadala utakaochagiza ufikiwaji wa lengo namba 3 linalohakikisha huduma za maji safi na usafi wa mazingira zinachangia uboreshaji afya na ustawi wa watu.
Huduma hizo ni msingi wa hatua za udhibiti wa ueneaji wa magonjwa, uimarishaji afya ya mama na mtoto sambamba na kulinda utu na usalama wa wagonjwa na wahudumu wa afya katika vituo vya kutolea vya afya.
Huduma za maji safi na usafi wa mazingira unavyodhibiti usugu wa vijidudu dhidi ya dawa
Usugu wa vijidudu dhidi ya dawa ni moja ya mada kuu zilizojadiliwa katika Mkutano huo wa kisera na kuonekana kama tishio jipya katika sekta ya afya duniani.
Zaidi ya vifo 750,000 vitokanavyo na usugu wa vijidudu dhidi ya dawa kila mwaka huripotiwa katika nchi za uchumi wa chini na kati pekee, na vifo hivi vinaweza kuzuilika endapo tutaamua kuboresha mifumo ya udhibiti na kinga dhidi ya maambukizi.
Huduma za maji safi na usafi wa mazingira zinatazamwa kama silaha muhimu katika mapambano dhidi ya usugu wa vijidudu dhidi ya dawa. Huduma hizi zinaweza kutumika kuzuia uibukaji, kujirudiarudia na ueneaji wa usugu wa vijidudu.
Wakati tunapiga mahesabu hayo, tusisahau kuwa ni asilimia 22 pekee ya vituo vya kutolea huduma za afya duniani vinakosa huduma ya maji na walau nusu yake vinakosa huduma za usafi wa mazingira.
“Usogezaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya sio tu ni kipaumbele chetu bali ni jambo muhimu. Ni msingi ambao tunaotegemea kujengea jamii ya Kitanzania yenye afya njema na himilivu zaidi. Kwa kuzipa kipaumbele huduma hizi, tutaweza kulinda afya za mama na mtoto, kuimarisha afya ya umma na kukabiliana na tishio la kiafya linaloshika kasi zaidi la usugu wa vijidudu dhidi ya dawa,” amesema Mbunge wa Nzega na Mwenyekiti wa Muungano wa Wabunge wanaopambana na Usugu wa Vijidudu dhidi ya Dawa, Mhe. Dk Hamis Kigwangala.
Utafutaji fedha kwa ajili ya miradi huduma za maji safi na usafi wa mazingira
Kutokana na ufinyu wa bajeti za nchi zinazoendelea katika kuimarisha uwezo wao wa kusimamia huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika vituo vya kutolea huduma za afya, kuna dhamira mahususi ya kuongeza ushirikiano wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na utafutaji rasilimali fedha kupitia ushirikiano wa nchi mbili na ule wa mataifa mbalimbali.
“Tunazihitaji Wizara ya Afya, Wizara ya Maji na wahisani kutimiza ahadi zao ili kufikia bajeti ya Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji (WSDP III) ya Dola za Marekani 49 milioni inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini ifikapo 2026,” ameeleza Christina Mhando, Mkuu wa Sera, Utetezi na Ushawishi wa WaterAid Tanzania.
Kuzifikia taasisi kubwa za kifedha kama vile Global Fund, Gavi, na Benki ya Dunia kunaweza kurahisisha uboreshaji wa mikakati hiyo ya huduma za maji safi na usafi wa mazingira kwaajili ya kuzuia Usugu wa vijidudu dhidi ya dawa (AMR).
“Huduma za maji safi na usafi wa mazingira lazima zipewe kipaumbele ikiwa tunataka kumaliza mlipuko wa magonjwa. Vyoo vyenye staha, maji safi na usafi wa mikono vinaweza kukomesha maambukizi kabla hayajaanza, jambo ambalo hupunguza hitaji la viuavijasumu na kupunguza usugu wa vijidudu dhidi ya dawa.
Hili ni suala la usalama wa Kitaifa na Ulimwengu wote, sio la kiafya pekee,” amehitimisha Anna Mzinga, Mkurugenzi wa Shirika la WaterAid Tanzania nchini.