Tanapa, Carbon Tanzania kushirikiana katika mradi mkubwa wa kaboni Afrika Mashariki

Msitu wa hifadhi ya Ntakata

Muktasari:

  • Hekta milioni 1.8 za Hifadhi za Taifa zitajumuishwa katika mradi wa kaboni unaotekelezwa na TANAPA na Carbon Tanzania
  • Ushirikiano huu utawezesha kuanzishwa kwa mradi wa kaboni unaotambulika kimataifa - ukifungua njia kwa uwekezaji endelevu wa uhifadhi.
  • Carbon Tanzania wanashiriki COP28 kukuza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuharakisha hatua za msingi za asili kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Dar es Salaam. Shirika la Hifadhi za Taifa za Tanzania (TANAPA) na Carbon Tanzania (CT) wamesaini Hati ya Makubaliano (MoU) ya kihistoria yenye lengo la kutekeleza mradi wa kaboni katika hifadhi sita za Taifa.

Hifadhi za Taifa zilizojumuishwa katika mradi huo ni; Burigi-Chato, Katavi Plains, Ugalla River, Mkomazi, Gombe Stream, na Hifadhi ya Milima ya Mahale.

Hifadhi hizi zina eneo la jumla la hekta 1.8 milioni, ikifanya huu kuwa mradi mkubwa zaidi wa kaboni Afrika Mashariki. Mradi huu utazingatia ulinzi, uhifadhi na usimamizi bora wa maeneo haya ya hifadhi za Taifa, kulinda mfumo wake wa asilia na rasilimali muhimu za wanyamapori.

Ikiwa hifadhi mashuhuri kama Serengeti na Kilimanjaro ziko chini ya uangalizi wake, TANAPA ni moja ya mashirika ya uhifadhi yanayoongoza Barani Afrika na lina nafasi nzuri ya kushirikiana katika mradi huu.

Mradi huu utaanza na upembuzi yakinifu, ambapo TANAPA na Carbon Tanzania wanakusudia kubaini ili kuhaini kiwango cha hewa ya kaboni kinachoweza kuzalishwa katika kila eneo na kutengeneza mfumo imara wa biashara na mpango wa usimamizi ili kuhakikisha upatikanaji wa fedha na uendelevu wa mradi huo kwa muda mrefu. Hii itakuwa mfano mzuri kwa uwekezaji zaidi katika Hifadhi za Taifa nchini.

Marc Baker, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Carbon Tanzania amesema: “Njia yetu ya ubunifu na mfumo wa kipekee wa biashara umejidhatiti katika kuhifadhi rasilimali za asili. Tunao uzoefu mkubwa wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika ngazi mbalimbali, kuanzia vijiji hadi wilaya na ngazi ya kitaifa. Carbon Tanzania ni kampuni ya kwanza na pekee Tanzania kutekeleza miradi ya kaboni kwa msingi wa uhifadhi wa misitu na kufanikiwa kuelekeza mapato kwa jamii katika Wilaya za Karatu, Mbulu, Tanganyika, Namtumbo, Tunduru na Kiteto kupitia miradi mitatu inayoitekeleza kwa sasa.”

Carbon Tanzania itatumia mtandao wake wa uwekezaji wa kimataifa kutoa fursa kwa TANAPA kupata mapato ya ziada, kuimarisha uwezo wake wa kusimamia maeneo ya hifadhi ambayo idadi yake imekuwa ikiongezeka.

Viongozi wa kampuni pamoja na wawakilishi wa jamii za asili wanahudhuria COP28 kwa mwaliko wa Serikali ya Tanzania. Watakuwa wakihamasisha njia za masoko zinazosimamiwa na jamii kwa uhifadhi na umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma ili kuongeza kiwango cha suluhu za kimazingira kwa mabadiliko ya tabianchi.

Mwakilishi wa jamii ya asilia amealikwa kuwa sehemu ya ujumbe huo ili kuongeza uzito wa jukumu muhimu ambalo watu wa jamii za asili wanafanya katika kulinda mazingira na kupunguza changamoto za mabadiliko ya tabianchi duniani.

Waanzilishi wa Carbon Tanzania wana uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika Soko la Hiari la Kaboni la Kimataifa (VCM), wakianzisha mtandao mkubwa wa washirika wenye ujuzi katika masuala ya fedha, sheria na njia za kiufundi. Mtandao huu utaleta urahisi katika maendeleo ya mradi huu mkubwa wa kaboni, ukiendana na masharti ya Mkataba wa Paris kuhusu ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma ili kukidhi Ahadi Zilizoridhiwa na Taifa (NDCs) katika mkataba huo.

Uwekezaji wa ziada katika mradi utatoka kwa kampuni ya Kitanzania, Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), kampuni ya kilimo, uzalishaji, na biashara iliyoanzishwa miaka ya 1970 na uwepo wa kikanda katika nchi sita za Afrika Mashariki.

Uzoefu wa MeTL katika biashara kwa kiwango kikubwa Barani Afrika utaimarisha utekelezaji wa mradi huu. Mohammed Dewji, Afisa Mtendaji Mkuu wa MeTL, amesema, “Tunafurahi kushirikiana na Carbon Tanzania ambayo njia yake ya uhifadhi inaleta mafanikio kwa jamii za asili za Tanzania, wakati ikilinda mazingira.

Marc anahitimisha: “Kusainiwa kwa mkataba huu ni hatua muhimu kuelekea mustakabali wa kijani na endelevu zaidi kwa Hifadhi za Taifa Tanzania. TANAPA na Carbon Tanzania wamejidhatiti kukuza ushirikiano wenye manufaa ambao hautalinda tu urithi wa asili wa Tanzania lakini pia utachangia kwa kiasi kikubwa katika hatua za kimataifa za mabadiliko ya tabianchi.”

Kwa kufuata mbinu ya kushirikiana na jamii ya Carbon Tanzania, utaratibu wa kanuni za Free Prior and Informed Consent (FPIC) umefuatwa kikamilifu na umesaidia katika kukamalisha kwa mafanikio zoezi la upembuzi yakinifu. Matokeo yanayotarajiwa kutoka katika upembuzi huo yatawezesha uundaji wa mradi wa kaboni uliothibitishwa kimataifa, ukionyesha hatua muhimu katika juhudi za uhifadhi endelevu.

Baada ya mradi huo kuanzishwa, mapato yanayotokana na mauzo ya fidia ya kaboni yatagawanywa kulingana na kanuni za biashara ya kaboni zilizochapishwa hivi karibuni. Kama Mamlaka ya Usimamizi, TANAPA inaendelea kuwa na mamlaka kamili juu ya utawala na maendeleo ya rasilimali zake, hivyo kutaiwezesha kupata asilimia 61 ya mapato ya jumla ya mauzo.

Katika sehemu hii, kanuni zinatoa mwongozo kwa TANAPA kushirikiana kwa pamoja na jamii zinazopakana na Hifadhi za Taifa ili kuhakikisha kuwa mapato yaliyopatikana yanatoa faida za kijamii na kiuchumi kwa watu wa eneo hilo.

Hii ni muhimu hasa kwani mara nyingi jamii hizi hulipa gharama moja kwa moja za uhifadhi kupitia migogoro ya binadamu na wanyamapori. Kwa kufuata mwongozo uliowekwa, TANAPA inaweza kukuza athari chanya kwa jamii na kuboresha maendeleo endelevu katika eneo hilo.


Kuhusu Shirika la Hifadhi za Taifa za Tanzania (TANAPA)

TANAPA ni shirika kubwa la uhifadhi barani Afrika, lililokabidhiwa jukumu la kulinda na kusimamia Hifadhi za Taifa Tanzania. Kwa mkusanyiko wa hifadhi za kipekee na azimio linaloendelea kwa uhifadhi, TANAPA inatekeleza jukumu muhimu katika kuhifadhi urithi wa asili wa nchi kwa vizazi vijavyo.


Kuhusu Carbon Tanzania

Carbon Tanzania ni shirika la kijamii linaloleta thamani ya kiuchumi kwa watu wa asili kupitia usimamizi endelevu wa misitu na bioanuai. Carbon Tanzania inazalisha mapato ya fidia ya kaboni kutokana na misitu inayowezesha wamiliki wa rasilimali za asili wa Tanzania kupata mapato kutokana na ulinzi wa rasilimali zao za asili.

Upunguzaji wa uzalishaji uliothibitishwa wa kaboni unaruhusu biashara zenye mikakati thabiti ya kuondoa kaboni kuwekeza katika suluhisho la msingi linalolinda hali ya hewa, jamii za asili, wanyamapori na kuchangia kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu.


Kuhusu Mohammed Enterprises Tanzania Limited

MeTL Group ni kampuni ya Kitanzania inayozalisha, kutengeneza na kufanya biashara ya bidhaa za kilimo, viwanda na bidhaa za watumiaji.

Biashara kuu za kampuni hiyo zinalenga kutoa bidhaa na huduma zenye thamani iliyotengenezwa ndani na zinazokidhi mahitaji ya kila siku ya Waafrika. Na uwepo wa kikanda katika nchi sita za Afrika Mashariki, MeTL Group imeajiri zaidi ya watu 30,000 Afrika Mashariki.