Mugalla: Upatikanaji wa haki za kijamii ni kazi endelevu

Caroline Mugalla, Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Ukanda wa Afrika Mashariki kwa nchi za Tanzania, Burundi, Uganda, Rwanda na Kenya.

Ukurasa mpya umefunguliwa kwa ukanda wa Afrika Mashariki baada ya kumpata Mkurugenzi Mkaazi mpya wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bi Caroline Khamati Mugalla ambaye atakuwa akisimamia shughuli za shirika hilo kwa nchi za Tanzania, Burundi, Uganda, Rwanda na Kenya.

Hatua hii inakuja baada ya aliyekuwa mkurugenzi mkazi wa ILO kwa ukanda huo, Bw Wellington Chibebe kumaliza muda wake na kupisha sura mpya ikiwa ni utaratibu wa mashirika hayo yaliyo chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa (UN) kubadili wakuu wa taasisi hizo ndani ya muda mfupi.

Licha ya asili ya mkurugenzi huyo kuwa ni Kenya, Bi Mugalla anakuja na uzoefu, maarifa na ujuzi mkubwa wa kufanya kazi katika kada ya utetezi wa haki za wafanyakazi na masuala ya uratibu wa sera zinazofaa za mazingira ya kazi na haki ya jamii kwa ujumla.

Amefanya kazi na taasisi ya EATUC kwa miaka 10 tangu 2013, kama katibu mkuu kabla ya uteuzi wake huu wa sasa, huku akihudumu katika ofisi nyingine kubwa za masuala ya ulinzi wa ustawi wa jamii na kazi kabla ya hapo kwa mafanikio makubwa.

“Kufanya kazi na ILO ndani ya ukanda huu ni sawa na kurudisha fadhila kwa sehemu iliyokulea. Safari yangu ya utetezi wa haki za wafanyakazi imeonekana katika ukanda huu na nadhani ni wakati sahihi wa kushukuru,” alisema na kuongeza: “Pia nimekuwa sehemu ya mafanikio makubwa katika kuufanya ukanda huu kuwa eneo bora la watu kutamani kufanya kazi, kwa kushirikiana na wadau wengine.”

Kama mkurugenzi mkaazi mpya katika ukanda huu, kazi ambayo iko mbele yake ni kuendelea pale ambapo mtangulizi wake aliishia. Bi Mugalla anasema kuwa, Chibebe alifanya kazi nzuri katika eneo hilo katika kufanya tathmini na kuunda sera ya pamoja kuhusu sheria za uhamiaji wa wafanyakazi kutoka eneo moja kwenda lingine ikiwa ni sehemu kubwa ya ajenda kuu ya haki za kijamii.

Akiwa na dhamira ya dhati ya kuendeleza jitihada za upatikanaji wa haki za kijamii kwenye mipaka ya Afrika Mashariki, mkurugenzi huyo hivi sasa anafanyia kazi rasimu ya itifaki ya soko la pamoja la ukanda huo katika masuala ya kuruhusu uhamiaji huru wa wafanyakazi kutoka eneo moja kwenda lingine ndani ya ukanda huo.

“Moja ya juhudi ambazo nimechukua kwa mwezi mmoja tu tangu nilipoteuliwa ni kupendekeza na kuharakisha tifaki ya soko la pamoja ambayo inadai uhuru wa wafanyakazi katika eneo hilo lote,” alieleza zaidi.

Amesema kuwa ukanda huo unakabiliwa na changamoto zinazofanana katika safari hii ya kusimamia upatikanaji wa haki za kijamii, licha ya ukweli kwamba bado ana imani kuwa mambo yatakaa sawa na wataweza kutatua changamoto hizo.

“Kama kuna jambo lolote ningependa kulisema, ni kuzishukuru Serikali wanachama kwa kuanzisha mazungumzo yahusuyo haki za kijamii ikiwa ni mwanzo wa hatua za mabadiliko.

Na sisi, ILO tutaendelea kuhimiza wadau wetu wote watatu (Serikali, vyama vya wafanyakazi na waajiri) kuendelea na mazungumzo haya kwa ajili ya kuchagiza ukuaji wa uchumi jumuishi na kutafuta suluhu kwa pamoja zinazotatua changamoto zinazokabili ukanda wetu,” alieleza Bi Mugalla.

Akipongeza dhamira ya dhati ya Tanzania katika kuridhia mikataba ya kimataifa ya usalama na afya mahala pa kazi na ile inayohusu usawa wa jinsia, anasema ni jambo la kupigiwa mfano kwa namna nchi hiyo inavyosisitiza uwezeshaji wa wanawake na vijana ambao ndiyo sehemu kubwa ya idadi ya watu nchini.

“Jambo moja ninalolipenda kuhusu Tanzania ni kwamba inapenda sana kuridhiwa kwa baadhi ya mikataba iliyowasilishwa mezani kuhusu mambo mbalimbali iwe ya afya, usalama kazini au jinsia.

Haitakimbilia chochote kwa ajili yake na inapofanya hivyo, inatii moja kwa moja.” Kuhusu nafasi ya vyama vya wafanyakazi na waajiri, Mkurugenzi huyo ambaye pia aliongeza kuwa vyama vya wafanyakazi vimekuwa macho kila mara na kuendeleza mazungumzo, hivyo ni wajibu wa Serikali kusikiliza sauti za waajiri na waajiriwa kupitia miongozo iliyopo.

Pia, amegusia kuhusu programu ya uanagenzi kama njia mojawapo ya kuwarasimisha wafanyakazi walio nje ya mfumo rasmi wa ajira.“Kama nakumbuka, ILO ilianzisha programu za uanagenzi miaka kadhaa iliyopita kama mkakati kuelekea kuunganisha wafanyakazi wasio katika sekta rasmi katika soko rasmi la ajira.

” Siri kuu ya mafanikio yake ya uongozi, kulingana na Mkurugenzi huyo ni kujitolea, kutokusikiliza miruzi kutoka nje, kuongeza ujuzi na kugeuza changamoto kuwa fursa kwa ajili ya maboresho zaidi. “Imekuwa utamaduni wangu kujitolea kwa asilimia mia na ishirini kwa kazi yangu na sitaangalia nyuma,” alidokeza.

Akiwa mwanamke wa kwanza barani Afrika kuongoza taasisi ya utetezi wa haki za wafanyakazi, EATUC, kwa kufanya hivyo, amechonga barabara ili wanawake wengine wapite, akipata msukumo mkubwa kutoka kwa baba yake mzazi, aliyekuwa mwanaharakati wa utetezi wa haki za wafanyakazi.

Safari yake ya kuacha kusomea fani ya bayokemia hadi kuwa mwanamke wa kupigiwa mfano katika utetezi wa haki za wafanyakazi na uratibu wa sera barani Afrika, unaonyesha utayari wake wa kusimamia upatikanaji wa haki za kijamii.

“Nimetoka katika familia yenye historia kubwa ya utetezi wa haki za kijamii. Mimi ni mtoto wa kumi katika familia ya watoto 11 na ndiye pekee niliyechagua kutetea haki za wafanyakazi na kuachana na taaluma ya ndoto yangu.

Nimekua katika msingi wa uanaharakati wa haki za wafanyakazi na kushiriki katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani na shughuli zifananazo na hizo, kwa muda mrefu.”

Baba yake alikuwa mtu mashuhuri katika kupigania haki za wafanyakazi huko Kenya ambapo alihudumu kama Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (COTU) nchini humo.

ILO ni shirika la Umoja wa Mataifa linaloundwa na pande tatu; ikijumuisha Serikali, vyama vya wafanyakazi na waajiri wanaofanya kazi kwa maslahi ya vyama vyao katika masuala yote yanayohusiana na kazi.