Miaka 2 ya Rais Samia Suluhu Hassan: Uhifadhi na Utalii wapaa TANAPA

Mitambo kwa ajili ya ujenzi barabara na viwanja vya ndege.

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ni taasisi ya Serikali iliyopewa dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yote yaliyoanzishwa kisheria kuwa Hifadhi za Taifa.

Shirika hili lilianzishwa mwaka 1959 kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura Na.282 (The National Park Act Cap.282) na kufanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kwa takribani miaka 64 sasa tangu kuanzishwa kwake, TANAPA imeendelea kupata mafanikio, tukianza na awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere.

Maroli kwa ajili ya ujenzi barabara na viwanja vya ndege.

Kipindi anatwaa madaraka kutoka kwa wakoloni mwaka 1961 kulikuwa na Hifadhi za Taifa tatu na wakati anang’atuka madarakani mwaka 1985 kulikuwa na ongezeko la hifadhi za taifa 11 zilizosheheni rasilimali nyingi.

Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika awamu tano zilizopita, kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kasi ya mafanikio imeongezeka kutokana na msukumo na hamasa aliyoiweka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuingia uwandani kuvitangaza vivutio tulivyonavyo ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Uboreshaji viwanja vya ndege Hifadhi ya Kilimanjaro.

Vivutio hivi vimetangazwa kupitia Filamu ya “Tanzania, the Royal Tour” aliyoiasisi Rais mwenyewe kwa kupita katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na Kilimanjaro, eneo la Ngorongoro, Zanzibar na maeneo mengine yenye vivutio vya utalii.

Sasa Tanzania imefunguka, na tunashuhudia mafuriko ya watalii kutoka mataifa mbalimbali wakipishana katika hifadhi zetu.

Akieleza mafanikio yaliyotokana na Filamu ya “The Royal Tour”, Kamishna wa Uhifadhi, William Mwakilema - TANAPA, anasema filamu ya Tanzania the Royal Tour imeleta mageuzi makubwa kwani tumeshuhudia ndege kubwa zikishusha watalii wengi katika viwanja vyetu vya ndege na hivi karibuni treni ya kitalii aina ya ROVOS RAIL kutoka Afrika ya Kusini imeleta watalii wengi kutembelea Hifadhi ya Taifa Nyerere. Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa treni hii ya kifahari kuleta wageni tangu mwaka huu 2023 uanze.

Tuzo ya World Travel Award ambayo Hifadhi ya Taifa Serengeti ilishinda 2022 kama hifadhi bora barani Afrika. Kwa kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia hifadhi hiyo imeshinda tuzo hiyo mara mbili mfululizo.

Anasema kuwa kuongezeka kwa watalii kutoka ndani na nje ya Tanzania katika Hifadhi za Taifa kunadhihirisha mchango mkubwa katika ongeza LA mapato kwa Serikali, huku Hifadhi ya Taifa Serengeti na Kilimanjaro zikionekana vinara wa kutembelewa na wageni wengi, hivyo mapato yanayotokana na utalii yanaendelea kuongeza kasi ya maendeleo katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali.

“Katika uongozi wa Dk Samia Suluhu Hassani, suala la uimarishwaji wa miundombinu pia halikuachwa nyuma. TANAPA ilipokea kiasi cha shilingi bilioni 46 karibia nusu ya fedha yote iliyotolewa na Rais kwa Wizara ya Maliasili na Utalii. Fedha hizo zimeelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya utalii na uhifadhi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, madaraja, viwanja vya ndege na malango ya kuingilia wageni,” anaongeza Kamishna Mwakilema.

Anafafanua kuwa malango ya kuingilia na kutokea wageni yamejengwa kisasa na kuwekewa mitambo ya Tehama ili kuzuia upotevu wa mapato wakati wa ukusanyaji.

Anataja Hifadhi zilizojenga malango hayo kuwa ni Hifadhi ya Taifa Mkomazi na Nyerere na kwamba Hifadhi ya Taifa Nyerere imepata malango mawili, moja eneo la Msolwa Kaskazini mwa hifadhi hiyo na lingine likiwa Kusini, eneo la Likuyu Sekamaganga.

Muonekano wa Bonde la Ihefu ambalo ni chanzo cha Mto Ruaha unavyovutia baada ya utatuzi wa mgogoro unaoendelea baina ya Serikali na wananchi wa Wilaya ya Mbarali.

Kamishna Mwakilema anasema kuwa lengo la kuweka malango maeneo hayo ni kuifungua Kusini kiutalii na kueleza kuwa mbali na ujenzi wa viwanja vya ndege katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi, Nyerere, Saadani na Tarangire. Fedha hizo pia zimetumika kununulia magari, mitambo na malori ili kurahisisha ukarabati na ujenzi wa barabara mpya. Fedha zote hizo zilitolewa na Rais kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO - 19.

Anakumbusha kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Dkt Samia Suluhu Hassani, Hifadhi ya Taifa Serengeti imeshinda tuzo ya kimataifa ya kuwa hifadhi bora barani Afrika mara mbili mfululizo.

“Hili ni la kujivunia sana kwani juhudi zake anazozifanya kuendeleza utalii ndio zimezaa matunda ya tuzo hii. Tuzo hii “The World Travel Award” hutolewa na taasisi ya kimataifa yenye makazi yake nchini Marekani,” anaeleza na kuongeza:

“Jambo jingine kubwa lililotekelezwa katika kipindi hiki ni utatuzi wa mgogoro kati ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi uliofanywa na Kamati ya Mawaziri nane (8) wa kisekta. Mgogoro wa Ihefu ulidumu kwa zaidi ya miaka 18 na kwa sasa unaelekea ukingoni kwani GN 28 iliyokuwa inalalamikiwa na wananchi wa Wilaya ya Mbarali inafanyiwa kazi na wataalamu wako uwandani kuweka mpaka mpya.”

Watalii wakiwasilia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Qatar.

Eneo la Ihefu ni chanzo cha Mto Ruaha Mkuu ambao ni muhimu kwa Ikolojia ya Hifadhi ya Taifa Ruaha. Maji yanayotiririka kutoka katika mto huu ni muhimu katika uzalishaji wa nishati ya umeme katika mabwawa ya Mtera, Kidatu na bwawa linaloendelea kujengwa la Nyerere. Hivyo utatuzi wa mgogoro huu ni muhimu kwa mustakabali wa Taifa.

“Kama tulivyoshuhudia mwaka jana kwa zaidi ya miezi mitatu mfululizo Mto Ruaha Mkuu ulikauka na kusababisha upungufu wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme. Sababu za tatizo hilo ni shughuli za kibinadamu zisizofuata sheria na taratibu zilizokuwa zikiendelea kwenye vyanzo vinavyoingiza maji ndani ya bonde la Ihefu.

“Timu ya Mawaziri hao 8 wa Kisekta imeweza pia kuleta utatuzi wa mgogoro katika ghuba ya Speke ambapo watu walikuwa wanaishi. Kwa sasa wanafanyiwa uthaminishaji wa mali zao ili walipwe fidia na kupisha uhifadhi wa wanyamapori na vyanzo vya maji vilivyokuwa hatarini kukauka,” aliongeza Mwakilema.

Anaeleza kuwa utatuzi wa migogoro hiyo miwili uliofanyika katika kipindi cha uongozi wa Samia Suluhu Hassani umepunguza uhasama kati ya wananchi na hifadhi, pia utasaidia kupunguza athari zilizokuwepo katika Bonde la Ihefu zilizokuwa zikikausha mto huo.

Anaendelea kufafanua kuwa kasi hiyo ya mafanikio ya miaka miwili ya uongozi wa Samia Suluhi imepunguza changamoto zilizokuwepo.

TANAPA pia imefanikiwa kuwafunga “collar” wanyama kama tembo ili kufuatilia mienendo yao wanapovamia maeneo ya makazi na kuwarudishana pia wanyama walio hatarini kutoweka kama Faru na mbwa mwitu. Vifaa hivi vimesaidia wanyama kama Faru kutouwawa na majangili kwa kipindi chote cha miaka miwili.