Carbon Tanzania yasherehekea Siku ya Mazingira Duniani kwa kukabidhi hundi ya Sh14.25 bilioni, mapato ya hewa ukaa kwa jamii za Tanganyika
Muktasari:
- Jamii ya vijiji 8 zilizoko ndani ya Wilaya ya Tanganyika zimepokea mapato ya awamu ya nane na tisa ya fidia ya hewa ukaa ya mwaka 2023 kiasi cha Sh 14.25 bilioni, na kupelekea kuwa jumla ya kiasi cha Tsh 22.51 bilioni kuanzia kuanzishwa kwa mradi wa milima ya Ntakata
- Mapato hayo yanatokana na mkataba na mwekezaji (Carbon Tanzania) kutokana na shughuli za ulinzi wa misitu ya asili
Vijiji vinane na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika zimepokea mfano wa hundi yenye thamani ya Sh14.25 bilioni za Kitanzania.
Mapato hayo yametokana na uuzaji wa vyeti vya fidia ya hewa ukaa yenye ubora wa hali ya juu, iliyoidhinishwa kimataifa kwenye soko huria la kaboni ambayo yamepatikana kutokana na ulinzi wa Hifadhi ya Misitu kwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya Ardhi ulioandaliwa na vijiji.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Phillip Mpango alipokea mfano wa hundi ya fedha hiyo kwa niaba ya wanajamii katika siku ya kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Juni 5, 2024.
Mwaka 2017 Serikali za Vijiji ziliingia mkataba na mwekezaji mkubwa wa misitu ya asili barani Afrika, Carbon Tanzania, kutekeleza mchakato ambao juhudi za ulinzi wa misitu zinatambuliwa kwa kupimwa na kulipwa fidia za kifedha.
Kwa kuzuia ukataji miti katika hifadhi zao za misitu, jamii zinachangia katika mapambano ya kimataifa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Misitu inapokatwa, hewa ukaa husambaa kwenye angahewa na kuleta athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Hili linapozuiwa kutokea na kusababisha upunguzaji wa hewa ukaa, hutambuliwa kama utunzaji wa hewa ukaa iliyookolewa kutoka kwenye ukataji wa miti. Carbon Tanzania inauza kiwango kilicho okolewa kwenye soko la hiari la kaboni (VCM), ambapo mauzo haya huzipa jamii fursa ya kufikia mfumo wa kifedha wa kimataifa.
Jamii za vijiji, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Wilaya, zinapanga mipango ya bajeti na utoaji wa mapato hayo kwa kuzingatia malengo ya maendeleo yao na Taifa kwa mujibu wa kanuni zilizotolewa na Serikali hivi karibuni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Carbon Tanzania, Marc Baker alisema “Fidia za mapato ya kifedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabinchi ni fursa kubwa kwa Tanzania na kama mwekezaji mkuu katika ulinzi wa misitu ya asili hapa nchini, Carbon Tanzania inalenga kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ulinzi wa misitu.”
Mpango huu unaoongozwa na jamii ni kielelezo muhimu cha jinsi jamii za Kitanzania zinavyoweza kulifikia soko la kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabinchi kupitia soko huria la kaboni (VCM).
Kuhusu Carbon Tanzania
Carbon Tanzania ni kampuni ya kitanzania ambayo inachangia katika kukuza uchumi wa nchi na watu wake kwa kutunza misitu asili na viumbe hai kupitia uuzaji wa vyeti vya hewa ukaa iliyookolewa na kuwawezesha watanzania kupata mapato kutokana na uhifadhi wa mazingira yao.
Vyeti hivi hununuliwa na mashirika ya kimataifa yenye malengo na mikakati chanya ya kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kwa kuwekeza katika shughuli za kiasili zinazochochea na kuleta matokeo bora ya uhifadhi katika utunzaji wa hali ya hewa, jamii na wanyamapori nchini.
Kuhusu mradi wa Milima ya Ntakata
Mradi wa Milima ya Ntakata unasimamia hekta 216,994 za pori la Miombo katika mfumo wa Ikolojia wa Mahale, Magharibi mwa Tanzania. Vijiji nane vinavyojumuisha watu 57,189 vinajishughulisha na mradi huu.
Kwa kuendeleza Hifadhi ya Misitu ya Vijiji (VLFRs) jamii hizo zinaweza kulinda makazi muhimu ya Sokwe wa Mashariki walio hatarini kutoweka. VLFR pia husimama kama kiungo muhimu kati ya mfumo wa ikolojia wa Greater Mahale na Hifadhi ya Taifa kwa Tembo Katavi.
Jamii za wakulima za Bende na Tongwe hulinda msitu wao na thamani ya hewa ukaa iliyohifadhiwa jambo linalowezesha kuzalisha mapato kutokana na mauzo ya vyeti vya hewa ukaa kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za uhifadhi kupitia MKUHUMI (REDD).
Mradi wa MKUHUMI (REDD) umeidhinishwa na VCS na CCB, unazuia miti milioni 1.5 kukatwa kila mwaka na kuepuka tani 550,000 za uzalishaji wa kaboni kila mwaka.
Faida za kimazingira
Kabla ya maendeleo ya mradi huu, ukataji miti katika eneo la mradi ulikuwa kwa asilimia 3.5, juu ya kiwango cha wastani cha kitaifa cha ukataji miti. Viwango vya ukataji miti vinatarajiwa kupungua sana. Mradi unazuia miti milioni 1.5 kukatwa kwa mwaka.
Mradi huu unalinda Sokwe wa Mashariki walio hatarini kutoweka, Mbwa mwitu, Tai wa Misri na Lappet-faced. Pia hulinda viumbe walio katika mazingira magumu ikiwa ni pamoja na tembo, pembe za ardhini, Tai wa kijeshi, Twiga, Pangolini, Chui, Simba, White-backed, na Ruppell’s Griffon Vulture walio hatarini kutoweka.
Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
Mradi huu unaepusha tani 550,000 za uzalishaji wa hewa ukaa kwa mwaka. Mradi huu hutoa fidia ya hewa ukaa iliyoidhinishwa kwa kulinda misitu iliyo hatarini na utoaji wa fidia kwa kampuni zinazoendesha miradi ya kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
Mapato yanayopatikana kutokana na mauzo ya fidia ya hewa ukaa hutumika kulipa mishahara kwa walinzi wa kijamii na vijiji (VGS), kusaidia mifuko ya afya na ada za elimu, na kufadhili miradi ya maendeleo ya jamii. Mradi huu umeidhinishwa na VCS & CCB ya VERRA, wenye viwango vya kimataifa.