Yanga, Simba mechi ya ubingwa

Muktasari:

  • Kumbukumbu ya mchezo uliopita wa ligi baina ya timu hizo ambao Yanga iliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 hapana shaka ndio unafanya mechi ya leo kuteka zaidi hisia za mamilioni ya Watanzania watakaoitazama wakiwa uwanjani au kwenye luninga.

Dar es Salaam. Homa ya mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba itamalizwa leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11 jioni ikiwa ni mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu huu.

Kumbukumbu ya mchezo uliopita wa ligi baina ya timu hizo ambao Yanga iliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 hapana shaka ndio unafanya mechi ya leo kuteka zaidi hisia za mamilioni ya Watanzania watakaoitazama wakiwa uwanjani au kwenye luninga.

Lakini kwa upande mwingine ni mechi ambayo ina nafasi kubwa ya kuamua vita ya ubingwa wa ligi msimu huu kulingana na msimamo wa ligi ulivyo.

Ushindi kwa Yanga leo, utaifanya ijikite zaidi kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha pointi 58 ambazo zitakuwa 12 zaidi ya zile za Simba iliyo katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 46, pengo ambalo kiuhalisia litakuwa gumu kwa Simba kuliziba na kuipiku Yanga kwa idadi ya michezo itakayobakia.

Kwa Simba, ushindi utaifanya ifikishe pointi 49 na hivyo kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa kwani itabakia na mchezo mmoja mkononi ambao kama ikipata ushindi, maana yake itakuwa nyuma ya Yanga kwa pointi tatu tu.
Chunga sana hawa

Stephane Aziz Ki na Maxi Nzengeli hapana shaka ndio wachezaji wanaopaswa kuchungwa zaidi katika kikosi cha Yanga kutokana na uwezo wao mkubwa wa kufunga mabao na kupiga pasi za mwisho.

Hadi sasa Aziz Ki ameshahusika na mabao 21 akifunga 14 na kupiga pasi za mwisho saba wakati Nzengeli amehusika na mabao 11 akifunga tisa na kupiga pasi mbili zilizozaa mabao.

Kwa upande wa Simba, wachezaji wa kuchungwa zaidi ni Clatous Chama na Saido Ntibanzonkiza.

Chama ameshahusika na mabao 12 akifunga saba na kupiga pasi tano za mwisho huku Ntibazonkiza akihusika na mabao tisa, akifunga saba na kutoa pasi mbili zilizozaa mabao.


Shilingi imesimama

Matokeo ya mechi tano zilizopita za Ligi Kuu baina ya timu hizo mbili yanaonyesha hakuna mbabe kati ya Yanga na Simba na pengine itakayopata ushindi leo itakuwa imejiweka katika mzingira mazuri ya kutamba mbele ya nyingine.

Timu hizo katika mechi tano zilizopita, kila moja imepata ushindi mara moja na zimetoka sare tatu, Yanga ikifunga mabao sita na Simba ikifumania nyavu mara nne.


Vita ya rekodi

Hamu ya wengi bila shaka ni kuona kama rekodi kadhaa zilizowahi kuwekwa kwenye mechi baina ya timu hizo hapo nyuma zinaweza kurudiwa, kufikiwa au kuvunjwa kupitia mchezo wa leo.

Ushindi kwa Yanga utaifanya irudie kile ilichokifanya katika msimu wa 2015/2016 ilipoibuka na ushindi katika mechi zake zote mbili za ligi dhidi ya Simba katika msimu huo ikishinda kwa mabao 2-0 katika kila mechi.

Nyota wa zamani wa Simba, Abdallah Kibaden katika mechi baina ya timu hizo Julai 19,1977, alifunga mabao matatu peke yake (Hat Trick), rekodi ambayo inasubiriwa kwa hamu leo kama itavunjwa au itabakia kama ilivyo.

Rekodi nyingine ambazo zinasubiriwa kama zitafikiwa au kuvunjwa ni kipa au makipa kufunga bao/mabao, idadi kubwa zaidi ya mabao kufungwa au ya wageni/wazawa kufunga idadi kubwa zaidi ya mabao.


Arajiga na rekodi yake

Mwamuzi Ahmed Arajiga kutoka Manyara aliyepewa kibarua cha kuchezesha mchezo huo anaingia akiwa na rekodi ya kuchezesha mechi mbili za watani wa jadi kwenye Ligi Kuu ndani ya msimu mmoja.

Arajiga ndiye alichezesha mechi ya mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo Novemba 5 mwaka jana ambayo Simba ilipoteza kwa mabao 5-1.

Huo ulikuwa ni mchezo wa tatu kwa Arajiga baina ya timu hizo ambapo hapo kabla alichezesha mechi mbili za mashindano ya Kombe la Shirikisho Tanzania ambazo kila timu ilipata ushindi mara moja.

Julai 25, 2021 alichezesha mechi ya fainali baina ya timu hizo kwenye kombe la shirikisho ambapo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na mwaka uliofuata, Mei 28 akachezesha mechi ya nusu fainali ya mashindano hayo ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Makocha wapiga mikwara
Wakizungumza jana katika mkutano wa waandishi wa habari, makocha Miguel Gamondi wa Yanga na Selemani Matola ambaye ni msaidizi kwa upande wa Simba, kila mmoja alitoa tahadhari kwa upande wa pili kuelekea mchezo huo.

"Mchezo wa kesho ni mchezo mgumu na tunajua wanataka kuja kucheza ili washinde mechi na kulipa kisasi lakini tumejiandaa kwa hilo. Sisi tuna timu imara ambayo inaweza kucheza kwenye presha ya aina yoyote. Kama wanadhani wakija na presha ya kulipa kisasi inaweza kuwasaidia basi linaweza pia kuwa kosa.

"Mashabiki wetu wamekuwa nyuma yetu wakati wote, hata dakika ambazo hatuchezi vizuri uwanjani wamekuwa wakiendelea kushangilia kwa nguvu na kutupa nguvu. Nina amini kesho kutakuwa na namba kubwa ya mashabiki wetu uwanjani na tumejiandaa kwa mchezo mzuri," alisema Gamondi.

Kwa upande wake Matola alisema kuwa wamejipanga kutorudia makosa yaliyopelekea wapoteze mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Yanga.

"Mwalimu huwa anaumia sana kuona tunakosa nafasi nyingi sana na hili tulilichukua kwa uzito mkubwa, tumelifanyia kazi mazoezini kuona tunamaliza hili tatizo na hivyo mashabiki wetu wategemee kitu kipya kwenye mchezo wetu wa kesho (leo) dhidi ya Yanga SC," alisema Matola.


Matokeo misimu 11 Iliyopita 2013/14    

Simba    3-3    Yanga
Yanga    1-1    Simba

2014/15
Yanga    0-0    Simba
Simba    1-0    Mtibwa

2015/16
Simba     0-2    Yanga
Yanga    2-0    Simba

2016/17
Yanga    1-1    Simba
Simba     2-1    Yanga

2017/18
Yanga     1-1    Simba
Simba     1-0    Yanga

2018/19
Simba    0-0    Yanga
Yanga    0-1    Simba

2019/20
Simba    2-2    Yanga
Yanga    1-0    Simba

2020/21
Yanga    1-1    Simba
Simba    0-1    Yanga

2021/22
Simba    0-0    Yanga
Yanga    0-0    Simba

2022/23
Yanga    1-1    Simba
Simba    2-0    Yanga

2023/24
Simba    1-5    Yanga