Yanga na kibarua cha kupindua meza Caf

Kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Al Hilal ya Sudan kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Novemba 26, 2024, kiliwaacha mashabiki wa Yanga wakiwa na maswali mengi kuliko majibu.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara walionekana kutokuwa kwenye kiwango bora, hali iliyowafanya kufungwa kirahisi na wageni wao kutoka Sudan katika mchezo huo wa kwanza wa Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Sasa, safari ya Yanga kuvuka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika imechukua sura mpya inayohitaji wafunge mkanda na kuanza upya mapambano yenye ulazima wa kurekebisha mambo kwa haraka.
Kwa Yanga, kipigo hicho si mwisho wa safari, bali ni changamoto ambayo wanaweza kuigeuza kuwa daraja la mafanikio. Huku mechi nyingine zikiwa bado mbele yao, timu hii yenye historia kubwa ina nafasi ya kujifunza kutokana na makosa, kuboresha udhaifu wao na kurejesha matumaini ya mashabiki wao kwa kufanya vyema katika michezo iliyosalia.
Kwenye mchezo dhidi ya Al Hilal, ukuta wa Yanga ulionekana dhaifu na usio na mawasiliano. Mabeki wa kati, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Dickson Job, walijikuta wakishindwa kushirikiana vizuri, hali iliyowapa wapinzani nafasi ya kutumia mianya yao kufunga mabao mawili. Kosa moja lilikuwa kupoteza mipira ya juu na kuruhusu mashambulizi ya haraka, jambo ambalo liliiumiza Yanga kwa kiwango kikubwa.
Katika michezo ijayo, Kocha wa Yanga, Sead Ramovic anahitaji kuimarisha nidhamu ya ulinzi kwa kuhakikisha wachezaji wanakuwa na mawasiliano bora. Mazoezi maalum ya kuimarisha safu ya ulinzi dhidi ya mipira ya juu yanapaswa kupewa kipaumbele.
Kipa Djigui Diarra naye anahitaji kujipanga vyema katika mawasiliano ya haraka na mabeki wake. Katika mchezo dhidi ya Al Hilal, mara kadhaa alionekana kusitasita kutoka langoni, hali iliyowapa faida washambuliaji wa Al Hilal. Hili ni eneo ambalo linaweza kufanyiwa kazi kwa haraka.
Lakini pia kiungo cha Yanga kilionekana kupwaya bila uwepo wa Khalid Aucho, ambaye alikosekana kutokana na majeraha. Mudathir Yahya na Duke Abuya walijitahidi, lakini walikosa uimara wa kuzuia mashambulizi ya wapinzani na kusambaza mipira kwa haraka katika maeneo sahihi.
Aziz Ki, ambaye alicheza kama kiungo mchezeshaji, alionekana kupungukiwa na msaada kutoka kwa wenzake. Katika michezo ijayo, Yanga inahitaji kuhakikisha Ki anapata nafasi zaidi ya kucheza mipira ya mwisho kwa washambuliaji, jambo linaloweza kuimarisha mashambulizi yao.
Changamoto nyingine kwa Yanga ilijitokeza ni uwezo duni wa washambuliaji wake kutumia nafasi walizotengeneza. Prince Dube alikosa nafasi kadhaa wazi ambazo zingeweza kubadili matokeo ya mchezo.
Hali hii inahitaji mabadiliko ya haraka. Kocha anapaswa kufanya mazoezi ya umaliziaji wa mipira kwa wachezaji wake wa mbele, hasa Dube. Aidha, Yanga inaweza kufikiria kumpa nafasi Clement Mzize ambaye anaweza kuwa fiti kwa ajili ya mchezo ujao kama mshambuliaji wa kati.
Kocha Ramovic anatakiwa kuwa na mipango madhubuti ya kiufundi kwa michezo ijayo. Pia, nidhamu ya kiufundi inapaswa kuimarishwa. Wachezaji wanatakiwa kufuata maelekezo ya kocha kwa umakini na kuhakikisha kila mmoja anatekeleza majukumu yake ndani ya mfumo. Hili linahitaji mazoezi ya mara kwa mara na mikakati ya kina kuelekea kila mchezo.
Baada ya kipigo cha nyumbani, morali ya wachezaji na mashabiki inaweza kuwa chini. Hii ni changamoto nyingine ambayo Yanga inahitaji kuishughulikia haraka. Benchi la ufundi lina jukumu la kuhamasisha wachezaji na kuwapa imani kuwa wanaweza kufanya vizuri katika michezo ijayo.
MSIKIE RAMOVIC
Kocha Ramovic amesema: "Inaumiza, nimeanza na matokeo mabaya ya kipigo, kama timu kubwa tunarudi kujipanga na mechi zijazo, tunajua tuna mechi nyingi mbele, tutahamikisha tunafanya vizuri.
"Ukiangalia utimamu wa wachezaji upo chini kulinganisha na aina ya soka ninalotaka kucheza…