Uganda yatwaa ubingwa CECAFA ikiichapa Serengeti Girls
Kikosi cha timu ya taifa ya wanawake ya Uganda chini ya umri wa miaka 17 wakishangilia baada ya kuibuka mabingwa wa michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA)
Muktasari:
- Mechi hiyo ya fainali iliyopigwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, ilizikutanisha timu hizo ambazo zilifanya vizuri kuanzia makundi hadi kufika fainali.
Timu ya Taifa ya wanawake ya Uganda chini ya umri wa miaka 17 imeibuka bingwa mpya wa michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa umri huo baada ya kuichapa timu ya Taifa ya Tanzania 'Serengeti Girls' mabao 3-0.
Mechi hiyo ya fainali iliyopigwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, ilizikutanisha timu hizo ambazo zilifanya vizuri kuanzia makundi hadi kufika fainali.
Mabao matatu ya Uganda yamefungwa na Justine Ayerango dakika ya 38 kabla ya Brenda Nassaka kuongeza la pili dakika ya 42 na lile la Flavia Yagala aliloweka kambani dakika ya 48.
Kikosi cha timu ya taifa ya wanawake ya Uganda chini ya umri wa miaka 17 wakishangilia baada ya kuibuka mabingwa wa michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA)
Uganda imechukua ubingwa huo mbele ya wenyeji na ikiweka rekodi ya kutoruhusu bao hata moja tangu ilipoanza michuano hiyo Julai 13, mwaka huu.
Timu hiyo ilianza hatua ya makundi ikishinda mechi zote tatu za kundi B, ikifunga mabao 20 ukiwa ni wastani wa mabao matano kwa kila mechi.
Katika hatua ya nusu fainali iliitoa Kenya kwa mabao 3-0, kisha ikatinga fainali ilipokutana na Serengeti na kuifunga idadi hiyo ya mabao.
Kwa upande wa Serengeti ilimaliza ikiwa kinara wa kundi A ikikusanya pointi saba, ilianza kwa kuitandika Somalia mabao 4-0 kisha kuichapa Sudan Kusini mabao 10-0 na kumaliza hatua ya makundi kwa sare ya 1-1 dhidi ya Kenya.
Kikosi cha timu ya taifa ya wanawake ya Uganda chini ya umri wa miaka 17 wakishangilia baada ya kuibuka mabingwa wa michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA)
Ilipotinga hatua ya nusu fainali ikaitoa Sudan Kusini kwa mabao 4-0 kisha kupokea kichapo cha kwanza dhidi ya Uganda kwenye fainali.
Mashindano hayo yalijumuisha timu nane kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuwania taji hilo ambazo ni Somalia, Djibouti, Kenya, Uganda, Tanzania, Sudan Kusini, Sudan na Zanzibar.