Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Trump aionya Australia isiwarudishe wachezaji wa Iran

Muktasari:

  • Trump amesema Australia inaweza kufanya kosa kubwa la kibinadamu iwapo itawalazimisha wachezaji hao kurejea Iran.

Rais wa Marekani Donald Trump ameionya Australia kutoiruhusu timu ya taifa ya Wanawake ya Iran kurejea nyumbani, akisema wachezaji hao wanaweza kukabiliwa na adhabu kali au hata kuuawa.

Kauli hiyo imekuja baada ya baadhi ya wachezaji wa Iran kukosolewa vikali na vyombo vya habari vya nchi yao kwa kukataa kuimba wimbo wa taifa kabla ya mechi dhidi ya Korea Kusini katika michuano ya Kombe la Wanawake barani Asia inayofanyika Australia.

Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya Wanawake wa Iran, wakiwa ndani ya gari ambalo lilizuiliwa baada ya mmoja wa wachezaji hao kuonyesha ishara ya Kimataifa ya kuomba msaada (SOS). Picha na Mtandao


Ishara ya kuomba msaada

Baada ya Iran kutolewa kwenye mashindano hayo kufuatia kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Philippines, mmoja wa wachezaji alionekana akitoa ishara ya kimataifa ya kuomba msaada (SOS) akiwa ndani ya basi la timu.

Ishara hiyo hutolewa kwa kuficha kidole gumba ndani ya kiganja na kukikunja kwa vidole vingine ishara inayotambulika kimataifa kuwa mtu anahitaji msaada.

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameitaka Serikali ya Australia kuhakikisha timu ya Wanawake ya Iran, inabaki nchini humo kwa sababu za kiusalama. Picha na Mtandao


Trump ataka wapewe hifadhi

Kupitia mitandao ya kijamii, Trump amesema Australia inaweza kufanya kosa kubwa la kibinadamu iwapo itawalazimisha wachezaji hao kurejea Iran.

“Australia inafanya kosa kubwa la kibinadamu kwa kuiruhusu timu ya Wanawake ya Iran kurejeshwa Iran ambako wana uwezekano mkubwa wa kuuawa. Wapewe hifadhi,” ameandika Trump akimlenga Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese.

Trump amesema amezungumza na Albanese kuhusu suala hilo na kudai kuwa baadhi ya wachezaji tayari wamepelekwa katika eneo salama.

Ofisi ya mrithi wa zamani wa ufalme wa Iran aliye uhamishoni, Reza Pahlavi, imesema imefahamishwa kuwa wachezaji watano, Fatemeh Pasandideh, Zahra Ghanbari, Zahra Sarbali, Atefeh Ramazanzadeh na Mona Hamoudi wamepelekwa katika eneo salama.

Inadaiwa wachezaji hao walihamishwa kutoka hoteli yao katika eneo la Gold Coast na kupelekwa katika nyumba salama inayolindwa na polisi wa Australia.

Mlinda lango wa Iran, Raha Yazdani (kulia), Melika Motevalli (katikati) na Fatemeh Amineh (kushoto) wakisimama wakiwa wamepiga saruti kutoa heshima wakati wimbo wa taifa ukipigwa kabla ya mechi yao dhidi ya Ufilipino. Picha na Mtandao


Hatma ya wachezaji wengine haijulikani

Hata hivyo, hatma ya wachezaji wengine wa timu hiyo bado haijulikani. Ofisa wa Shirikisho la Soka la Australia (PFA), Beau Busch, amesema kwa sasa ni vigumu kuwasiliana nao.


Vyombo vya habari Iran vyawashambulia

Vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na serikali ya Iran vilishutumu hatua ya wachezaji kukataa kuimba wimbo wa taifa, vikisema ni usaliti mkubwa. Mtangazaji Mohammad Reza Shahbazi alionya kuwa wasaliti wakati wa vita wanapaswa kuadhibiwa vikali.


Shinikizo la kimataifa

Wanaharakati wa haki za Wanawake na makundi ya kijamii wameiomba serikali ya Australia kuhakikisha usalama wa wachezaji hao.

Mwanzilishi wa kundi la haki za Wanawake la AUSIRAN, Rana Dadpour, amesema serikali inapaswa kukutana na wachezaji hao faraghani ili kujua kama wanahitaji hifadhi.

Kwa sasa, serikali ya Australia imekuwa makini kuzungumzia suala hilo hadharani ikihofia kwamba taarifa nyingi zinaweza kuhatarisha usalama wa wachezaji hao pamoja na familia zao nchini Iran.  

Moja ya sehemu mashambulizi yanayoripotiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati. Picha na Mtandao

Taarifa hizo zinakuja baada ya operesheni ya kijeshi iliyolenga maeneo kadhaa ya miji mikuu ya Iran, ikiwamo Tehran, kufuatia wiki kadhaa za mvutano wa kisiasa na kijeshi kati ya Iran na Marekani.

Mashambulizi hayo yamefanyika wakati kukiwa na mazungumzo kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran, ambapo Washington ilikuwa ikishinikiza kusitishwa kwa juhudi za Iran kumiliki silaha za nyuklia kwa kubadilishana na kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi.