Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TFF na mwanzo mpya baada ya Uchaguzi

Muktasari:

  • Katika Uchaguzi huo Rais aliyekuwa anatetea nafasi yake, Wallace Karia aliidhinishwa na wajumbe wote wa mkutano mkuu kuendelea kuhudumu katika nafasi hiyo.

Ni taswira ya safari mpya na ya mabadiliko ya miaka minne ya uongozaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada ya Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho hilo uliofanyika juzi Jumamosi, Agosti 16, 2025 jijini Tanga.

Kamati mpya ya Utendaji iliyoundwa baada ya Uchaguzi huo inaonyesha wazi kuwa familia ya mpira wa miguu imefungua mlango kwa fikra mpya kuingia katika chombo hicho ambacho ni cha pili kimamlaka baada ya Mkutano Mkuu.

Katika Uchaguzi huo Rais aliyekuwa anatetea nafasi yake, Wallace Karia aliidhinishwa na wajumbe wote wa mkutano mkuu kuendelea kuhudumu katika nafasi hiyo.

Uidhinishwaji wa Karia ulifanywa kwa vile yeye alikuwa ni mgombea pekee wa nafasi hiyo hivyo kwa mujibu wa katiba, hapigiwi kura za ndio au hapana.


Sura mpya zateka kamati

Ni uchaguzi ambao umeipa kamati ya utendaji idadi kubwa ya watu ambao hawakuwa sehemu yake katika awamu iliyopita jambo ambalo wengi hawakulitegemea.

Kuanzia kwa wale ambao wameingia kwenye Kamati ya Utendaji kwa kuchaguliwa hadi wale wa kuteuliwa na Rais wa shirikisho hilo kwa mujibu wa katiba, wageni wa kamati hiyo wameonekana kuwa wengi kulinganisha na wazoefu.

Katika kanda sita ambazo zilikuwa zikigombewa kwenye uchaguzi huo, ni wajumbe watatu tu waliokuwa katika Kamati ya Utendaji iliyopita waliofanikiwa kutetea nafasi zao.

Wajumbe hao ni  Khalid Mohamed wa kanda namba moja ambaye yeye hakupigiwa kura bali aliidhinishwa na mkutano mkuu kwa vile alikuwa mwenyewe kama ilivyokuwa kwa mgombea wa kanda namba sita Issa Bukuku.

Wa tatu ni James Mhagama ambaye tofauti na wenzake, yeye alishinda kupitia boksi la kura kwa kumuangusha Cyprian Kwiyava.

Wakati wao wakibaki, uchaguzi huo uliangusha wazoefu wawili wa kamati ya utendaji ambao ni Vedastus Lufano aliyekuwa Mjumbe wa Kanda namba tano ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa miguu Geita, Salum Kulunge.

Kanda namba moja nayo ilimpata bosi mpya tofauti na aliyekuwa amezoeleka hapo awali. Mshindi katika kanda namba moja safari hii alikuwa ni Hosseah Lugano ambaye amemuangusha Lameck Nyambaya aliyekuwa akiishikilia nafasi hiyo.’

Mategemeo yalienda tofauti katika uteuzi wa Karia kwa majina manne ya kuingia katika Kamati ya Utendaji ambapo alifanya uteuzi wa sura tatu mpya huku akimrudisha mmoja tu kutoka wale aliowateua awali.

Kati ya wale walioteuliwa na Karia  katika awamu iliyopita, Jina la Athuman Nyamlani ndio pekee lilipata uteuzi wa kurudi katika Kamati ya Utendaji kupitia mamlaka ya kikatiba inayompa Rais wa TFF fursa ya kuteua Wajumbe Wanne wa Kamati hiyo.

Majina yaliyotegemewa kama Ahmed Mgoyi na Said Soud awamu hii hayakupata fursa hiyo na badala yake Karia aliteua sura nne ambazo zinaingia kwa mara ya kwanza katika kamati hiyo ya Utendaji.

Wajumbe wanne ambao Karia amewateua kuingia katika Kamati ya Utendaji na kisha wakapitishwa na Mkutano Mkuu ni Evance Mgeusa, Debora Mkemwa, Athuman Nyamlani na Azan Muft.


Mkeka mpya Kamati TFF

Kutorudi kwa baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa awamu iliyopita na ingizo la sura mpya katika kamati hiyo hapana shaka kutasababisha mabadiliko ya lazima katika baadhi ya kamati za TFF ili kukidhi matakwa ya kikatiba.

Katiba ya TFF inafafanua kwamba Mwenyekiti wa Kamati iliyo chini ya Shirikisho hilo anapaswa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ingawa sio lazima kwa Kamati za Kimahakama za shirikisho.

Mfano wa kamati ambazo zitaguswa na mabadiliko baada ya Uchaguzi huo ni ile ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokuwa ikiongozwa na Said Soud ambaye safari hii hajateuliwa tena kuwemo katika Kamati ya Utendaji.

Mwanahabari Somoe Ng’itu ambaye ameingia katika Kamati ya Utendaji ya TFF kwa tiketi ya Uenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wanawake Tanzania (TWFA) au Debora Mkemwa, mmojawapo anaelekea kuchukua nafasi ya uenyekiti wa kamati ya soka la wanawake.

Hata hivyo kubakia kwa Bukuku, Khalid Abdallah, Mohamed Aden na Mhagama kunawapa fursa ya kuendelea kuwa wenyeviti wa kamati za shirikisho hilo walizowahi kuziongoza awali au kupewa mpya.


Majukumu ya Kamati ya Utendaji

Kamati ya Utendaji ya TFF miongoni mwa majukumu yake makubwa ni kusimamia na kutekeleza maelekezo na maagizo ya Mkutano Mkuu wa Shirikisho hilo. Ni chombo ambacho kinasimamia uendeshaji wa shughuli za mpira wa miguu hapa nchini.

Kama ilivyoainishwa juu, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ndio wanakuwa wenyeviti wa kamati tofauti za Shirikisho hilo. Jukumu lingine la Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo ni kumsaidia na kumshauri Raia wa TFF.


Karia, wadau wafunguka

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa juzi, Karia ameomba wadau wa soka kuungana pamoja katika kusogeza mbele mchezo huo na kuondoa visasi.

"Tunajukumu kubwa la kuhakikisha tunaendelea kupiga hatua za kimaendeleo, Tanzania tunaendelea kukuwa kwa kasi sana nadhani tutajikita huko.

"Tutawataka wadau wetu kufuata utaratibu na kanuni, tutakwenda kubadilisha kanuni mbalimbali kama ambavyo wadau wametoa mapendekezo.

"Tutakwenda kuipa nguvu Bodi ya Ligi hatutataka tena lawama kwa TFF. Sisi TFF tutatabaki kusimamia mambo makubwa ya utawala na maboresho ya soka,” amesema Karia

Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kutoka Lindi, Rehule Nyaulawa amesema ana imani kubwa na uongozi uliochaguliwa.

“Nawapongeza washindi na hata wale ambao hawajapata fursa ya kuchaguliwa. Naamini mambo mazuri yanakuja mbele hivyo tunapaswa kuwaunga mkono viongozi wetu wapya ili tuzidi kupeleka mbele soka letu,” alisema Nyaulawa