TFF mtegoni rufaa kesi ya kumfungia Katabazi
Muktasari:
- Mahakama Kuu katika uamuzi wake huo uliotolewa na Jaji Butamo Philip wa Septemba 26, 2025, ilikubalina na rufaa hiyo ya Kocha Katabazi, hivyo ikatengua uamuzi wa Kisutu, na ikaamuru jalada lirejeshwe Kisutu iendelee kuisikiliza madai ya msingi ya Kocha Katabazi.
Dar es Salaam. Rufaa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) kupinga usikilizwaji kesi ya Kocha Listoni Katabazi dhidi yake iko njia panda baada ya Kocha Katabazi kuiweka mtegoni kwa kuibua pingamizi la hoja za kisheria kuhusu uhalali wake.
Katika pingamizi hilo Kocha Katabazi anayewakilishwa na mawakili wake Peter Majanjara na Melchzedeck Joachim ameibua hoja mbili, kwanza akidai kuwa, kwanza rufaa hiyo si halali kwa kuwa inatokana na uamuzi na amri ya mahakama ambayo haihitimishi kesi na pili kuwa ....
TFF, ambaye ni mrufani wa kwanza na Bodi ya Wadhamini wake Waliosajiliwa, wanapinga uamuzi wa Mahakama Kuu katika rufaa ya madai namba 28749/2024 aliyoikata Kocha Katabazi, akipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, iliyofuta kesi yake ya msingi.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake huo uliotolewa na Jaji Butamo Philip wa Septemba 26, 2025, ilikubalina na rufaa hiyo ya Kocha Katabazi, hivyo ikatengua uamuzi wa Kisutu, na ikaamuru jalada lirejeshwe Kisutu iendelee kuisikiliza madai ya msingi ya Kocha Katabazi.
TFF na wadhamini wake katika rufaa hiyo ya madai namba 2575 /2025 waliyoikata Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu, kupitia wakili wao Makubi Kunju, katika sababu zao za rufaa,wanadai kuwa Mahakama Kuu ilikosea kisheria:
Mosi, kwa kushindwa kuzingatia kuwa migogoro inayohusiana na mpira wa miguu haitashughulikiwa na mahakama za kawaida za kiraia kwa kuwa ina jukwaa maalum na hivyo Mahakama ya mwanzo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza madai ya mjibu rufaa.
Mbili, kwa kuamua kwamba uanachama wa mjibu rufaa (Kocha Katabazi) katika TFF ulikuwa katika mgogoro.
Tatu, kwa kutathmini vibaya kumbukumbu za Mahakama ya awali (Kisutu) na hoja zilizowasilishwa na hivyo kufikia uamuzi usio sahihi.
Kisheria amri au uamuzi wowote wa mahakama ambao hauhitimishi shauri, haukatiwi rufaa wala kufanyiwa mapitio.
Uamuzi wa Mahakama Kuu ambao TFF imeukatia rufaa, ambapo ilitengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu wa kuifuta kesi Kocha Katabazi na kuelekeza mahakama hiyo ya chini iendelee na usikilizwaji wa kesi ya msingi hiyo si uamuzi wa kuhitimisha kesi.
Ni kwa msingi huo Katabazi kupitia mawakili wake wakati akiwasilisha majibu dhidi ya sababu za rufaa hiyo zilizotolewa na TFF pamoja na hoja za maandishi, ameibua pingamizi hilo la awali kwamba rufaa hiyo haina uhalali kwa kuwa inatokana na uamuzi usiohitimisha shauri.
Kutokana na pingamizi hilo, TFF, mahakama itasikiliza kwanza pingamizi hilo kabla ya kusikiliza rufaa ya TFF na uamuzi wa mahakama katika pingamizi hilo ndio utakaotoa hatima ya usikilizwaji wa rufaa hiyo ya TFF.
Kama mahakama itakubaliana na pingamizi hilo, basi rufaa ya hiyo itakuwa imefia hapo kwani itatupiliwa mbali bila hata kusikilizwa na hivyo, Mahakama ya Kisutu itaendelea na usikilizwaji wa kesi ya msingi ya Kocha Katabazi.
Lakini iwapo mahakama italikataa pingamizi hilo, basi itaendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo ya TFF na katika uamuzi wale itapima iwapo sababu za rufaa za TFF zina mashiko au la.
Kwa sababu hiyo TFF bado ina kibarua kigumu kwanza cha kupangua pingamizi hilo kwa hoja zitakazoishawishi Mahakama kuwa uamuzi huo wa Mahakama Kuu japo hauhitimishi kesi ya msingi, bado unaweza kukatiwa rufaa.
Kama itafaulu kuvuka kizingiti hicho cha pingamizi kibarua cha pili ni kuishawishi mahakama kuwa sababu zake za rufaa zina mashiko kiasi cha kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu.
Kocha Katabazi anayejitambulisha kuwa mdau wa soka na kocha wa mchezo huo mwenye leseni ya daraja C, iliyotolewa na TFF, alifungua kesi hiyo dhidi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa TFF na TFF yenyewe mwaka 2024.
Alifungua kesi hiyo baada ya kufungiwa na TFF kujishughulisha na soka ndani na nje ya nchi maisha yake yote, kufuatia barua aliyoliandikia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Juni 15, 2021, akiilalamikia TFF kushindwa kusimamia soka kulingana na Sheria, Kanuni na miongozo yake.
Kutokana na barua hiyo aliitwa katika Kamati ya Maadili ya TFF, lakini hakuhudhuria akijibu kuwa yeye si mwanachama wa TFF kwani si mwanachama wa Chama cha Makocha Tanzania (Tafca) ambacho kiko chini ya usimamizi wa TFF.
Hivyo Juni 24, 2021 TFF lilichapisha katika tovuti yake uamuzi wa kumfungia Katabazi maisha kujishughulisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi, ndipo akafungua kesi hiyo.
Katika kesi hiyo ya madai namba 14708/2024, Kocha Katabazi alidai kuwa Kamati ya Maadili ya TFF haikuwa na mamlaka ya kumpa adhabu hiyo kwani Kanuni za Maadili za TFF, Toleo la Mwaka 2021, zilizotumika kumfungia si halali.
Alidai kuwa kanuni hizo hazijasajiliwa na BMT kulingana na matakwa ya Sheria ya BMT namba 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake, hivyo kuzifanya kuwa batili kutumika kwa wanachama wake na mtu mwingine yeyote.
Pia alidai kuwa amri hiyo iliingilia haki yake ya kufanya kazi katika nyanja ya soka na hivyo kumkosesha fursa ya kupata mshahara na kipato kwa ajili ya kuendeleza maisha yake ya kila siku na familia yake, na kumsababishia maumivu ya kisaikolojia.
Hivyo aliiomba mahakama iiamuru TFF imlipe Sh600 milioni kama fidia ya madhara ya jumla aliyoyapata kutokana na uamuzi huo wa kumfungia maisha uliotolewa kwa maksudi, kimakosa na kwa nia ovu.
Pia aliomba alipwe Sh100 milioni kama fidia ya adhabu kwa kitendo cha wadaiwa kutoa uamuzi huo wakijua kuwa hawana mamlaka ya kisheria kumchukulia hatua hiyo, riba ya kiwango cha Mahakama kwa tuzo (fedha ambazo ingeamuriwa alipwe) na gharama za kesi.
Vilevile aliiomba mahakama itoe zuio la matumizi ya Katiba na Kanuni za Maadili za TFF, akidai kuwa si vyombo halali kwa kutokusajiliwa kwa utaratibu na unaofaa.
Kocha Katabazi aliwasilisha mahakamani hapo barua ya BMT ya Juni 13, 2022 iliyothibitisha kuwa yeye si mwanachama wa TFF.
Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Kiswaga, iliifuta kesi hiyo baada ya kukubaliana na pingamizi la TFF.
Hakimu Kiswaga alikubali kuwa Katabazi ni mwanachama wa TFF na kwamba kwa Katiba ya TFF, alipaswa kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya Maadili, na asingeridhika anaweza kwenda Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).
Hivyo alikubaliana na TFF kuwa kwa kuwa Katabazi hakufuata utaratibu huo, mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Katabazi alikata rufaa Mahakama Kuu ambayo ilitoa uamuzi huu unaopingwa na TFF.