Ten Hag: Nataka kubaki United

Muktasari:

  • United inashika nafasi ya nane pointi 54, ikifunga mabao 52 na kufungwa 55, imepoteza michezo 13 na kushinda 16 tu msimu huu.

Manchester, England. Kocha wa Manchester United, Erik ten Hag amesema bado anataka kuendelea kupambana kuhakikisha anakuwa kocha wa timu hiyo msimu ujao pamoja na kupata matokeo mabaya.

United iliwashanga wengi jana baada ya kuchapwa mabao 4-0 na Crystal Palace kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliopigwa Uwanja wa Selhurst Park na sasa timu hiyo inatakiwa kuhakikisha inashinda michezo iliyobaki ili kurudisha matumaini.

Hata hivyo, mchezo unaofuata wa timu hiyo ni dhidi ya Arsenal ambayo inawania ubingwa wa Ligi Kuu England ambayo inataka kuhakikisha inapata ushindi ili kuendelea kuipa presha Man City ambayo nayo inawania ubingwa huo.

Kichapo cha juzi kimeifanya United kuweka rekodi ya kufungwa michezo mingi kwa msimu mmoja baada ya hadi sasa kupoteza 13, baada ya kuruhusu mabao 81 kwenye michuano yote ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 1977.

Ten Hag amesema timu yake imepoteza nguvu ya kupambana, lakini anatakiwa kufanya kazi kubwa kuhakikisha inaanza kushinda upya ikiwa imebakiza michezo mitatu imalize msimu.

"Nafikiri tumekuwa tukipata matokeo mabaya, lakini lazima tuendelee kupambana kama ambavyo mashabiki wamekuwa wakifanya kwenye michezo yetu.

"Hakika bado natakiwa kuendelea kupigana, siyo kubaki hapa tu bali kuhakikisha timu inaendelea kufanya vizuri hadi tumalize msimu huu," alisema kocha huyo ambaye timu yake inashika nafasi ya nane na pointi 54, ikifunga mabao 52 na kufungwa 55.