Tabora Utd yabaki Ligi Kuu, yaizima Biashara kibabe

Muktasari:

  • Katika mchezo wa leo, shujaa wa Tabora alikluwa ni Mcongomani Patrick Lembo aliyefunga mabao yote mawili dakika ya 27 kwa njia ya penalti baada ya Mganda Ben Nakibinge kufanyiwa madhambi eneo la hatari na beki wa Biashara, Isaya Kuzoza kabla ya kuongeza jingine dakika ya 55.

Kazi imeisha! Baada ya Tabora United jioni ya leo Jumapili kufanya kweli ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora kwa kuinyoosha Biashara United kwa mabao 2-0 na kujihakikisha kusalia katika Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.

Tabora ilipata ushindi huo unaoifanya iizuie Biashara Utd kurejea Ligi Kuu katika pambano la marudiano ya play-off ya kuwania kukamilisha timu ya 16 ya msimu ujao kwa jumla ya mabao 2-1, kwani ilipoteza ugenini Alhamisi ya Juni 12 kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, mjini Musoma mkoani Mara.

Katika mchezo wa leo, shujaa wa Tabora alikluwa ni Mcongomani Patrick Lembo aliyefunga mabao yote mawili dakika ya 27 kwa njia ya penalti baada ya Mganda Ben Nakibinge kufanyiwa madhambi eneo la hatari na beki wa Biashara, Isaya Kuzoza kabla ya kuongeza jingine dakika ya 55.

Tabora ilimaliza Ligi Kuu Bara msimu ulioisha hivi karibuni ikiwa nafasi ya 14 kwa kuvuna pointi 27 baada ya kushinda michezo mitano, sare 12 na kupoteza 13, hivyo kuangukia mechi za mtoano dhidi ya JKT Tanzania iliyomaliza ya 13 na Nyuki wa Tabira walikubali kichapo cha jumla ya mabao 4-0.

Ushindi huo kwa JKT uliifanya ijihakikishe kuicheza Ligi Kuu Bara ijayo na kuiacha Tabora ikipangwa kukutana na Biashara iliyomaliza  nafasi ya nne katika Ligi ya Championship ilikusanya pointi 62 zilizotokana na ushindi wa mechi 19, ikitoka sare tano na kupoteza sita, hivyo kujikatia tiketi ya kucheza play-off ikivaana na Mbeya Kwanza iliyomaliza nafasi ya tatu'.

Katika michezo ya mtoano kwa Ligi ya Championship, Biashara ili pata ushindi wa jumla wa mabao 4-0 dhidi ya Mbeya Kwanza iliyopigwa mabao 2-0 nyumbani na ugenini na kuwaacha 'Wamajeshi wa Mpakani' wakisonga mbele kupambana kusaka tiketi y kurudi Ligi Kuu iliyoishuka misimu mitatu iliyopita, lakini bahati haikuwa yao mbele ya Nyuki wa Tabora na sasa wanaenda kujipanga upya kwa msimu ujao.

Biashara ilishuka daraja msimu wa 2021-2022 baada ya kushika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 28 na kwa Tabora iliyopanda daraja msimu uliopita sasa inaendelea kujipangwa kwa msimu wa pili wa Ligi Kuu ambayo mabingwa wake ni Yanga inayoshikilia taji kwa misimu mitatu mfululizo sasa.