Simba, Yanga kimeeleweka robo fainali CAFCL
Muktasari:
- Simba ndio itakuwa ya kwanza kuikaribisha Al Ahly Ijumaa ya Machi 29 saa 3:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki huku Yanga ikifuata Jumamosi kukabiliana na Mamelodi Sundowns muda kama huo.
Dar es Salaam. Hatimaye imefahamika siku na muda ambao timu za Tanzania, Simba na Yanga zitatupa karata zao za michezo ya robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku mmoja akicheza dhidi ya Al Ahly ya Misri na mwingine dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Simba ndio itakuwa ya kwanza kuikaribisha Al Ahly Ijumaa ya Machi 29 saa 3:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki huku Yanga ikifuata Jumamosi kukabiliana na Mamelodi Sundowns muda kama huo.
Kwa nini saa tatu usiku? Zipo taarifa mpangilio wa muda huo wa mchezo umezingatia kutoa fursa kwa mashabiki ambao ni waumini wa dini ya Kiislamu waliopo katika mfungo wa Mwezi wa Ramadhani kufuturu kabla ya mchezo husika kupigwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Hesabu za mechi hizo za robo fainali zimeanza kwa kila upande licha ya kuwa na wiki ya michezo ya kimataifa mbele kwa mujibu wa kalenda ya FIFA na mabenchi ya ufundi ya timu hizo yanahaha kupata taarifa muhimu ambazo zitawasaidia katika maandalizi yao.
Makocha wa Simba na Yanga, Abdelhak Benchikha na Miguel Gamondi wamebeba matumaini makubwa ya mashabiki wa timu hizo pamoja na wadau wa soka la Tanzania ambao wanatamani kuona watani hao wa jadi wakiandika historia mpya.
Kwa kiasi kikubwa Benchikha ameifanya Simba kuwa kwenye uelekeo mzuri ukitofautisha na hali ambayo timu hiyo ilikuwa ikipitia, Gamondi ni kama ameinogesha tu Yanga ambayo tangu msimu uliopita ilikuwa tishio chini ya mtangulizi wake, Nasreddine Nabi aliyeifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho la Afrika.
Simba na Yanga zinahitaji ushindi kwenye michezo hiyo ili kuwa na mtaji mzuri katika michezo ya marudiano ambayo itamalizia ugenini kati ya Aprili 5 na 6.