PSG yatetea ubingwa League 1
Muktasari:
- Mabingwa hao wa Ulaya wamefanikiwa kutwaa taji hilo baada ya kuwafunga wapinzani wao wa karibu Klabu ya Lens.
Paris, Ufaransa. Klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) imeendelea kutawala soka la Ufaransa baada ya kutwaa ubingwa wa Ligue 1 kwa msimu wa tano mfululizo kufuatia ushindi waliopata jana dhidi ya wapinzani wao wa karibu, Lens.
PSG ilihitaji kuepuka kipigo katika mchezo huo ili kutangaza ubingwa na ikaonyesha ubora wake kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 uliowapa taji la 14 la ligi katika historia ya klabu hiyo.
Mshambuliaji wa PSG, Desire Doue (katikati) wakati akijaribu kupiga shuti katika mechi ya Ligi Kuu Ufaransa dhidi ya Lens. Picha na Mtandao
Nyota wa kimataifa wa Georgia, Khvicha Kvaratskhelia, aliifungia PSG bao la kwanza dakika ya 29 kabla ya Ibrahim Mbaye kuongeza la pili katika muda wa nyongeza na kuzima matumaini ya Lens.
Licha ya PSG kung’ara katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kufika fainali kwa msimu wa pili mfululizo, safari yao ya ndani ya Ligue 1 haikuwa nyepesi baada ya kupoteza michezo dhidi ya Olympique Lyon, AS Monaco, Olympique Marseille na Stade Rennais.
Wachezaji wa PSG wakati wakimrusha juu kocha wao Luis Enrique baada ya kuiongoza timu hiyo kutetea taji la League 1. Picha na Mtandao
Hata hivyo, kikosi hicho kinachonolewa na Luis Enrique kimeandika historia mpya kwa kuwa timu ya pili kutwaa taji la Ligue 1 mara tano mfululizo baada ya Lyon iliyofanya hivyo kuanzia mwaka 2001 hadi 2006.
Baada ya kutwaa ubingwa huo, sasa PSG inaelekeza nguvu zake katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambako itakutana na Washika Mitutu wa London, Arsenal ikiwa na lengo la kutetea taji hilo.