Pamba Jiji yapata ajali, wachezaji wapo salama

Muktasari:
- Basi la Pamba Jiji lililokuwa limewabeba wachezaji na benchi la ufundi likiwa linatokea mjini Bukoba mkoa wa Kagera kuelekea Morogoro kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB, liligongwa kwa nyuma na Semi Truck saa 11 alfajiri wilayani Bahi, Dodoma na kusababisha mshtuko kwa wachezaji.
Daktari wa klabu ya Pamba Jiji, Joseph Chacha amesema wachezaji wako sawa kiafya baada ya ajali ya gari iliyotokea leo mkoani Dodoma, ambapo kikosi hicho kimeendelea na safari yao ya kwenda Morogoro kucheza mchezo dhidi ya Kiluvya United.
Basi la Pamba Jiji lililokuwa limewabeba wachezaji na benchi la ufundi likiwa linatokea mjini Bukoba mkoa wa Kagera kuelekea Morogoro kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB, liligongwa kwa nyuma na Semi Truck saa 11 alfajiri wilayani Bahi, Dodoma na kusababisha mshtuko kwa wachezaji.
Pamba Jiji ilikuwa safarini kutoka Bukoba mkoani Kagera kwenda Morogoro baada ya kumaliza mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wao Kagera Sugar, uliomalizika kwa kupoteza kwa mabao 2-1.
Akizungumzia hali za wachezaji hao, Dk Chacha amesema wamepata mshtuko wa kawaida isipokuwa mchezaji, Mwaita Gereza aliyekuwa amekaa eneo ambalo gari liligongwa na lori hilo na kusababisha vioo vilivyopasuka kumsababishia mikwaruzo.
Dk Chacha amesema mchezaji huyo alipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Bahi kwa uchunguzi zaidi ambapo ameruhusiwa na msafara wa kikosi hicho umeendelea na safari yao kwenda Morogoro kucheza mchezo huo dhidi ya Kiluvya United.
"Imetokea tu kama ajali zingine zinavyotokea gari imepata shida na wachezaji wetu wamepata tu mshtuko wa kawaida ingawa mchezaji mmoja (Mwaita Gereza) alipata mikwaruzo kidogo na maumivu ya kawaida kwa sababu ya mshtuko wa ajali lakini amepata huduma amehudumiwa amefanyiwa check up (uchunguzi) yuko vizuri na timu imeendelea na safari kama kawaida," amesema Dk Chacha.
Ameongeza kuwa; "Wachezaji walipata mshtuko wa kawaida tu hakukuwa na sababu ya kuwacheki wote isipokuwa tu yule aliyekuwa amekaa kule nyuma ambako gari limegongwa yeye ndiye amepata shida kidogo kwasababu ya vile vioo vilivyopasuka vilimsababishia mikwaruzo."
Daktari huyo amesisitiza kuwa licha ya kujiridhisha kwa sasa kwamba wachezaji hao wako sawa lakini wataendelea na uangalizi wa karibu kwa saa 24 mpaka 72 ili kujiridhisha zaidi.
"Mambo ya ajali yana vitu vingi unajua inapotokea ajali tunaangalia kwa muda tuone labda kutakuwa na madhara gani baadaye, huwezi kutoa suluhisho muda huo huo kwamba mtu yuko sawa," amesema Chacha na kuongeza;
"Ingawa yeye anasema yuko sawa ni mshtuko tu na kichwa kinagonga tu kidogo tunajaribu ku-observe (kufuatilia kwa karibu) kwa masaa 24 mpaka 72 tuone, kwa kifupi iko hivyo tu."
Hiyo ni ajali ya pili ya basi la timu ya Ligi Kuu Bara mwaka huu wakati ikiwa kwenye ratiba za mechi, ambapo Februari 10, 2025 Dodoma Jiji ilipata ajali ya basi katikati ya Nungurukuru na Somanga wakati kikosi cha timu hiyo kikitokea Ruangwa mkoani Lindi kwenda jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wao Namungo FC, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2.