Pacome kuikosa JKT Tanzania leo, awasubiria Coastal Union

Muktasari:

  • Pacome Zouzoua ameifungia Yanga, mabao saba katika Ligi Kuu msimu huu ambao ni wa kwanza kwake baada ya kujiunga nayo akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema kuwa kiungo wake Pacome Zouzoua badon hajawa tayari kutumika katika mechi dhidi ya JKT Tanzania leo kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam ingawa anaweza kucheza mechi ijayo dhidi ya Coastal Union, Aprili 27.

Kiungo huyo tangu alipopata majeraha ya goti katika mechi dhidi ya Azam, Machi 17, hajaonekana uwanjani akiuguza majeraha yake na pia kufanya mazoezi ya utimamu na sasa Gamondi amethibitisha kwamba anaweza kuonekana uwanjani kuanzia mechi dhidi ya Coastal Union.

 "Yeye (Pacome) ataanza mazoezi na timu baada ya mchezo na labda atakuwa fiti kwa mchezo ujao," alisema Gamondi.

Ushindi katika mchezo wa leo utaifanya Yanga kufikisha pointi 61 na hivyo kuhitajika kupata ushindi katika mechi tano tu kati ya saba itakazobakiza ili ijihakikishie ubingwa pasipo kutegemea matokeo ya timu nyingine.

Mabingwa hao watetezi wanaingia katika mechi hiyo wakiwa wametoka kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba, Jumamosi iliyopita, matokeo ambayo hapana shaka yanawaongezea morali na hamasa katika mchezo wa leo ili kuzidi kusafisha njia ya ubingwa.

Lakini kingine ambacho kinaweza kuwapa matumaini Yanga kupata ushindi katika mechi ya leo ni kiwango kisichoridhisha ambacho kimekuwa kikionyeshwa na JKT Tanzania kilichopelekea kuifanya timu hiyo ijikute  ikiwa nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi na pointi zake 22.

Ni mchezo ambao unasubiriwa kwa hamu pia kuona kama kiungo wa Yanga, Stephane Aziz Ki ataendeleza makali yake ya kufumania nyavu yaliyomfanya awe kinara hadi sasa kwenye ligi akiwa nayo 15.

Wenyeji JKT Tanzania wamekuwa hawana muenendo mzuri kwenye mechi zao za Ligi Kuu za hivi karibuni ambapo katika mechi 10 zilizopita hawajapata ushindi hata mara moja, wakitoka sare sita na kupoteza mechi nne.

Wanakutana na Yanga iliyo ya moto ambayo imekuwa mfupa mgumu kwa wapinzani na kudhihirisha hilo, katika mechi zake 10 zilizopita za Ligi, imepata ushindi mara tisa na kupoteza mchezo mmoja tu.

Mahitaji ya ushindi ni makubwa zaidi kwa JKT Tanzania kwani ikifanikiwa kuondoka na pointi tatu leo, itafikisha pointi 25 na kusogea hadi nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi.

Hata hivyo JKT Tanzania itapaswa kuwa bora zaidi hasa katika safu yake ya ushambuliaji inayowategemea Sixtus Sabilo, Matheo Anthony, Shiza Kichuya na Daniel Lyanga ili iweze kuondoka na ushindi katika mchezo wa leo.

Safu hiyo ya ushambuliaji ya JKT Tanzania ndio inaonekana kuchangia kuiangusha kwa kiasi kikubwa msimu huu kwani hadi sasa, timu hiyo imepachika mabao 16 tu katika mechi 22 ilizocheza, jambo linaloifanya yenyewe na Tabora United ziwe timu zilizofunga mabao machache zaidi katika ligi hadi sasa.

Kocha msaidizi wa  JKT Tanzania George Mketo alisema kuwa wamejiandaa asilimia 100 kukabiliana na Yanga katika mchezo licha ya ukweli kwamba wanakabiliana na timu ngumu zaidi katika ligi.
 
"Hatuko katika nafasi nzuri kabisa na tunahitaji kushinda ili kuepuka eneo la kushushwa daraja.
Hivyo kila mchezo tunauona kama fainali na tunapaswa kucheza kwa bidii zote. Yanga walishinda 5-0 katika mchezo wa kwanza katika Uwanja wa Azam Complex, lakini sasa tuko katika uwanja tofauti na pia tuna mtazamo tofauti wa mchezo. Tunahitajika kuwa makini sana pia," alisema Mketo.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema wanaichukulia mechi hiyo kwa uzito mkubwa na wanahitaji ushindi ili kuendelea kuongoza na kusogelea ubingwa.

 "Siwezi kuzungumza sana kuhusu maandalizi kwani tulicheza Jumamosi na wachezaji walipumzika Jumapili na kufanya mazoezi Jumatatu (jana). Hivyo hatukupata muda wa mazoezi vya kutosha pamoja na ukweli kuwa tunatokea mchezo mgumu. Hata hivyo, hilo halitabadilisha lengo letu la kukusanya alama tatu na kuendelea kuongoza ," alisema Gamondi.