Pacome apewa dakika 20, Yanga ikitinga nusu fainali FA

Muktasari:

  • Pacome ambaye alipata majeraha katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam, Machi 17, alikosa michezo miwili ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelod Sundowns nyumbani na ugenini.

BAADA ya kukosekana katika michezo saba katika mashindano tofauti sawa na dakika 630, kiungo Pacome Zouzoua amecheza dakika 20 wakati Yanga ikitinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa kuichapa mabao 3-0  Tabora United  kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Pacome ambaye alipata majeraha katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam, Machi 17, alikosa michezo miwili ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelod Sundowns nyumbani na ugenini.

Pia alikosa mechi ya FA dhidi ya Dodoma Jiji na michezo minne ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Fountain Gate, Simba, JKT Tanzania na Coastal Union ambayo Yanga haikupoteza.

Fundi huyo mwenye mabao saba katika ligi aliingia leo katika mchezo huo dakika ya 70 wakati Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-0 ambayo yalifungwa na Stephane Aziz KI dakika ya 35 na Kennedy Musonda dakika ya 65.

Mwanaspoti linafahamu Pacome aliomba kwa kocha wa Yanga, Miguel Gamondi kuanza kutumika taratibu tangu mchezo wa dabi dhidi ya Simba ambao Wananchi waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Lakini Gamondi hakuwa na haraka ya kumtumia nyota huyo ambaye ni kati ya wachezaji hatari kwenye kikosi  chake ambacho kina nafasi ya kutetea mataji  mawili msimu huu, lile la ligi na FA.

Wakati akiingia kuchukua nafasi ya Aziz KI mashabiki wa Yanga walimshangilia na muda mfupi baadaye Yanga ikapata bao la tatu lililofungwa na Joseph Guede dakika ya 83.

Licha ya kutoonekana kuwa fiti kwa asilimia kubwa, lakini dakika 20 alizocheza Pacome hakuonekana kukaa na mpira muda mwingi kama alivyozoeleka.

Muivory Coast huyo alikuwa akiachia mpira kwa haraka pengine kwa hofu ya kutoneshwa goti ambalo alionekana kufunga bandeji yenye rangi ya bluu.

Kwa matokeo hayo, Yanga imetinga nusu fainali ambayo itacheza na Ihefu ambayo imeing'oa Mashujaa kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya kutoka suluhu ndani ya dakika 90.