Prime
Ongezeko ya kodi wanaoshinda 'mikeka’ lazua gumzo
Muktasari:
- Ongezeko hilo linalenga kuwezesha upatikanaji wa fedha za kusaidia serikali kupambana na ugonjwa wa Ukimwi na pia kuchangia bima ya afya.
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiongeza kiwango cha kodi inayotoza kwa washindi wa michezo ya kubashiri matokeo ya michezo ‘betting’, kumekuwa na mitazamo tofauti ya mkakati huo.
Baadhi ya watu wameonyesha sintofahamu kwenye ongezeko hilo huku wengine wakibainisha ni biashara kama zilivyo biashara nyingine.
Jana Juni 12, 2025, akisoma Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2025/26 Waziri wa fedha Mwigulu Nchemba alisema ongezeko hilo linalenga kuwezesha upatikanaji wa fedha za kusaidia serikali kupambana na ugonjwa wa ukimwi na pia kuchangia bima ya afya.
Alisema kiwango cha fedha kitakachopatikana, asilimia 70 itaenda katika mfuko wa serikali kupambana na ukimwi na asilimia 30 kuchangia mfuko wa bima ya afya.
“Kufanya marekebisho kwenye sheria ya michezo ya kubahatisha sura namba 41. Kuongeza kiwango cha kodi kwenye zawadi ya ushindi kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15,” amesema Waziri huyo.
Wakichambua ongezeko hilo, wapo waliotamani Serikali isingetumia betting kama sehemu ya mapato hayo wapo waliodai hiyo ni biashara hivyo ni sahihi kuwa na ongezeko la kodi.
Nyota wa zamani wa Simba, Quiresh Funguo alisema kuongeza kodi kwenye betting hakufai akidai mchezo ya kubashiri katika hali ya kimaisha haifai.
"Kwa sasa vijana wengi hawataki kufanya kazi zaidi ya kubeti, kunawaharibu hawataki kujiajiri wanaiona hiyo ndiyo ajira yao, hata wazee wapo baadhi nao ni kushinda kwenye betting, Serikali ingeona namna ya kusaidia kundi hilo kuliko kupandisha kodi," amesema Quiresh.
Msanii wa Hip Hop, Seleman Msindi (Afande Sele) amesema yeye amekuwa na mtazamo tofauti akisema ni sawa Serikali kuweka ongezeko la kodi kwenye betting.
"Betting sio kitu cha lazima japo inaonekana watu wengi wamejiajiri kwa upande huo kwa sababu wengi hawana ajira na kwenye wengi ndipo kuna kodi, vijana wengi wanakimbilia huko sababu ya ukosefu wa ajira, mitaji, maarifa na wengi wao wanaona 'kamari' ndiyo kazi rahisi," amesema.
Japo pia ameshauri kama mtangulizi wake kwamba Serikali ingeangalia vyanzo vingine vya mapato na kuona namna ya kupunguza wimbi la watu kubeti tofauti na sasa wapo wanaoamka asubuhi na hiyo ndiyo kuwa kazi yao siku nzima.
Mwanariadha nyota wa zamani, Filbert Bayi amesema kubeti sio lazima, hivyo ongezeko hilo ni sawa ili wanaojikita huko waamue.
"Ile ni biashara, ilichokifanya Serikali ni sawa sawa, mtu aamue kupata au kukosa," amesema, kauli sawa na iliyotolewa na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah ambaye naye alisisitiza hiyo ni biashara kama nyingine.