Neymar…Mambo sasa ni magumu kwake

Muktasari:
- Hii ina maana kuwa Mbrazil huyo amecheza mechi saba tu akiwa na kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu ya Saudia, Saudi Pro League.
Riyadh, Saudi Arabia. Maisha ya staa mkubwa duniani, Neymar kwenye soka yanaelekea kufika ukingoni baada ya kuandamwa na majeraha kwa mwaka mzima sasa, likiwa ni pigo kwa wengi waliokuwa wana matarajio makubwa kwake.
Neymar staa wa Kibrazili alirejea uwanjani hivi karibuni baada ya kukaa nje kwa muda mrefu, lakini alitumika kwenye mechi mbili tu na kurejea tena kwenye kitanda kuunguza majeraha.
Awali Neymar alitajwa kama mmoja kati ya mastaa duniani ambao wanaweza kutwaa tuzo kubwa ikiwemo Ballor d’or, lakini mambo yamekuwa magumu na hafikiriwi tena kuhusu hilo kutokana na majanga ya mara kwa mara.
Wakati anajiunga na Hilal vyombo vingi vya habari vilisema kuwa Neymar ni mtoto wa mfalme ambaye hawezi kuwa mfalme, vikimaanisha kuwa kutokana na uwezo wake wa awali aliaminika kuwa anaweza kuiteka duniani, lakini sasa amefika mwisho na hawezi tena.
Juzi staa huyo, alicheza kwa dakika 29 kwenye mchezo wa Asian Champions League na kutolewa nje baada ya kuumia nyama za paja, ikiwa ni siku chache tu tangu alipocheza mchezo wake wa kwanza baada ya mwaka mmoja kupita.
Huu unaonekana unaweza kuwa mchezo wa mwisho kwa mshambuliaji huyo kuitumikia klabu ya Al-Hilal baada ya mabosi wa timu hiyo kutangaza kuwa wanaweza kuuvunja mkataba wa staa huyo wa pauni 130 milioni kwa mwaka.
Hii ina maana kuwa Mbrazil huyo amecheza mechi saba tu akiwa na kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu ya Saudia, Saudi Pro League.
Mabosi wa timu yake ambao walikuwa na matumaini makubwa na Neymar na walikaa kikao juzi na kuna uwezekano mkubwa wakavunja mkataba wake Januari mwakani kama mchezaji huyo atakuwa anaendelea kusumbuliwa na majeraha wakiwa pia wameshamtoa kwenye listi ya wachezaji wanaocheza mechi za ligi.

Staa huyo mwenye miaka 32, amekuwa na majeraha sugu ya goti, nyama za paja na wakati mwingine kifundo cha mguu.
Huku ikielezwa kuwa amekuwa na tatizo la kutopumzika muda mwingi akionekana mara kwa mara kwenye baadhi ya klabu akicheza kamari jambo ambalo pia alilaumiwa nalo mwaka 2018 akiwa na PSG.
Jeraha kubwa la mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona na PSG, ni lile la goti Oktoba mwaka jana, ambalo lilimweka nje hadi Oktoba mwaka huu.
Pamoja na daktari wa timu hiyo kusema kuwa Neymar atakaa nje kwa wiki tatu tu na kurejea uwanjani, lakini inaonekana kuwa rekodi ya majeraha yake inaweza kumfanya akaachana na timu hiyo moja kwa moja kabla mkataba haujamalizika.
Ikifika Januari, staa huyo atakuwa amebakiza mkataba wa miezi sita ambao klabu yake inaona kuwa itakuwa rahisi kuuvunja kuliko hali ilivyo kwa sasa.
Wakati Al-Hilal, ikitaka kuuvunja mkataba wake na kocha wa timu hiyo, Jorge Jesus tayari inaelezwa kuwa ameridhia hilo, inaonekana kuwa kutakuwa na wakati mgumu kwa staa huyo kupata timu nyingine ya kuchezea Ulaya au Asia kutokana na umri wake, fedha atakayotaka kulipwa na rekodi ya majeraha yake.
Hata hivyo, atakuwa na nafasi ya kurudi nchini kwao Brazil akiwa amekuwa akiwindwa na timu yake ya zamani ya Santos kwa muda mrefu sasa.
"Ninaumia nikiona siwezi kucheza, nafikri kwenye maisha yangu ya soka majeraha ndiyo jambo ambalo linaniumiza zaidi, nafikiri naweza kurudi tena nikiwa na nguvu kubwa,” ilikuwa kauli ya Neymar baada ya kuumia.
Al Hilal kabla ya majeraha ya Neymar ilikuwa na mpango wa kupuguza wachezaji wenye umri mkubwa kwenye timu hiyo.
Pamoja na staa huyo wa Kibrazili timu hiyo ina wachezaji nane ambao umri wao ni miaka 21 na kuendelea ikiwa inazuiwa kuingiza mchezaji mwingine mgeni kutokana na kanuni ya Ligi Kuu ya Saudia.
Kama atakubali kushusha mshahara wake na rekodi yake ya majeraha ikiwa nzuri anaweza pia kujiunga na mastaa wenzake ambao amewahi kucheza nao nchini Hispania, Lionel Messi na Luis Suarez kwenye Ligi Kuu ya Marekani MLS baada ya kudaiwa kuwa Inter Miami ambayo mmiliki wake ni David Beckham, imekuwa ikimwania.
Al Hilal imekuwa ikionekana kuwa ilisharudisha fedha zake kiasi cha pauni 78 milioni ilipomsajili kutoka PSG mwaka 2023 kutokana na mauzo ya jezi zake ambapo ziliuzika kwa kiwango kikubwa alipotua Saudia.
Hata hivyo, uwanjani wameonekana kupata hasara kutokana na mchezaji huyo kucheza michezo saba tu ambapo amefanikiwa kufunga bao moja na kutoa pasi tatu za mabao, yaani asisti, kuanzia mwanzoni mwa msimu uliopita.
Hata hivyo, timu hiyo haina presha kubwa ya kuachana na mchezaji huyo kwa kuwa msimu uliopita ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Saudi Pro League bila msaada wa staa huyo.
Kwa sasa pia staa huyo hachezi, lakini timu hiyo ipo kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imeshinda mechi nane na kutoka sare mchezo mmoja huku nyota wa kikosi hicho Aleksandar Mitrovic, akiwa kinara wa ufungaji baada ya kufunga mabao 13 kwenye mashindano yote hadi sasa.
Hata hivyo, Neymar mwenye tuzo binafsi zaidi ya 50 analaumiwa na klabu yake kuwa hatumii juhudi kubwa kupunguza uzito na kuhakikisha anapona haraka.
Akiwa na Barcelona ambayo aliiisadia kutwaa makombe nane na PSG makombe 13 , Neymar aliwahi kulaumiwa mara kwa mara akidaiwa kuwa alikuwa anajiumiza ili aweze kwenda kushiriki sherehe ya kuzaliwa ya dada yake Rafaella Santos kila Machi 11, tangu mwaka 2013.
Hii ilikuwa habari kubwa, ambapo mwaka huu pia inaelezwa alishiriki kwenye sherehe hiyo pamoja na kwamba alikuwa akisumbuliwa na majeraha.
Inaelezwa kuwa Rafaella ambaye ni mwanamitindo ndiye rafiki mkubwa zaidi wa Neymar kwenye familia yao.
Mechi ambazo Neymar aliwahi kuzikosa kutokana na sherehe ya kuzaliwa ya dada yake:
2013/14 - Neymar hakutumika kwenye mchezo huu bila sababu, alienda Brazil.
2014/15 – Alipewa kadi ya njano ambayo ilimfanya kukosa mchezo uliofuata Machi 8, na akaenda Brazil kwenye sherehe ya dada yake.
2015/16 – Alikuwa na adhabu ya kufungiwa mechi mbili, akaenda Brazil.
2016/17 – Hakuwepo kwenye klabu kutokana na majeraha ya misuli, alikuwa Brazil.
2017/18 – Neymar alikuwa nje akitibu majeraha, siku moja kabla ya kumbukumbu ya dada yake alienda Brazil .
2018/19 – Alikuwa nje tena akitibu majeraha ya goti, siku ya sherehe alionekana.
2019/20 – Alicheza na kufunga bao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Dortmund. Wengi walishangaa
.2020/21 –Hakuwepo klabuni alikuwa akisumbuliwa na jeraha la misuli, akaenda kuungana na dada yake.
2022/23 – Alikuwa akisumbuliwa na majeraha, hivyo alienda Brazil kula keki.
Mechi alizocheza
Santos: 225 mabao 136
Barcelona: 186 mabao 105
PSG: 173 mabao 118
Al Hilal: 7 mabao 1