Mshambuliaji Yanga ala shavu Asia

Muktasari:
- Yusuph Athuman amewahi kuzichezea Yanga, West Armenia, Coastal Union na Biashara United kwa nyakati tofauti.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Yusuph Athuman ametua katika timu ya Yangon United inayoshiriki Ligi Kuu ya Mynammar kwa mkataba mwa mwaka mmoja.
Yangon United ni bingwa mara sita wa Ligi Kuu Mynammar na imewahi kushiriki Ligi ya Mabingwa bara la Asia mara kadhaa.
Athuman ambaye anejiunga na Yangon United kama mchezaji huru, amekamilisha uhamisho huo mwanzoni mwa wiki hii na ataitumikia timu hiyo katika msimu wa 2025/2026.
Kabla ya kujiunga na Yangon, Athuman aliitumikia West Armenia ambayo aliachana nayo Juni mwaka jana baada ya kuitumikia kwa msimu mmoja.
Katika dirisha dogo la usajili msimu huu, mchezaji huyo alikaribia kujiunga na Fountain Gate FC lakini mpango huo ulikwama dakika za mwisho kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22, anamudu kucheza nafasi zote za winga na pia mshambuliaji wa kati huku silaha yake kubwa ikiwa ni kasi na unyumbulifu.
Yusuph mwenye kimo cha Mita 1.92 ameeleza kufurahishwa na usajili huo wa kujiunga na Yangon United.
"Nina furaha kujiunga na timu hii. Yangon United ni miongoni mwatimu zenye mafanikio katika Ligi ya Mynammar na ninaona fahari kuwa hapa.
"Nitatoa kilicho bora zaidi kwa timu hii na kushindania taji la ligi. Nawakaribisha mashabiki kuja uwanjani kutusapoti na tutashangilia mafanikio," amesema Athuman.