Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msako wa rekodi Simba ikitafuta kurudi kileleni Ligi Kuu

Kinda wa Simba, Bashiri Kibaila (kulia) wakati akishangilia bao, kushoto ni mshambuliaji Seleman Mwalimu. Picha na Simba

Muktasari:

  • Leo Simba ina nafasi ya kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kupita muda mrefu tangu ikae hapo Oktoba Mosi, 2025 ilipoifunga Namungo mabao 3-0, kisha ikaja kushushwa Oktoba 18, 2025, siku ambayo Mbeya City iliichapa KMC mabao 3-0.

NI takribani siku 215 zimepita tangu Simba ishushwe kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na Mbeya City ambapo hapo kati, timu mbalimbali zimepishana kukaa juu ya msimamo wa ligi hiyo ikiwemo JKT Tanzania na Yanga inayoongoza sasa, huku Wekundu hao wa Msimbazi wakishindwa kurejea.

Leo Simba ina nafasi ya kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kupita muda mrefu tangu ikae hapo Oktoba Mosi, 2025 ilipoifunga Namungo mabao 3-0, kisha ikaja kushushwa Oktoba 18, 2025, siku ambayo Mbeya City iliichapa KMC mabao 3-0.

Mashabiki wengi watakuwa bize kufuatilia mechi hiyo ya Simba inayocheza dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kuanzia saa 12:30 jioni. Kabla ya hapo, saa 10:00 tutashuhudia JKT Tanzania ikikabiliana na Fountain Gate, kisha saa 3:00 Namungo itaikairibisha Mbeya City.

Baadhi ya wachezaji wa Simba wakishangilia ushindi wa 4-0 katika mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya TRA United. Picha na Simba


Coastal Vs Simba

Simba inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na lengo moja kubwa, ushindi unaoweza kuwapa nafasi ya kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi kabla ya wapinzani wao, Yanga kucheza Ijumaa dhidi ya Singida Black Stars.

Kwa sasa, Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 54, huku Simba ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 52, tofauti ya pointi mbili inafanya kila mchezo kuwa wa uamuzi.

Hali hiyo inaweka presha kubwa kwa Simba ambayo inajua wazi kwamba kupoteza au sare inaweza kuwapa Yanga nafasi ya kuendelea kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa huo.

Kwa upande wa Coastal Union iliyopo nafasi ya 11 na pointi 25, mchezo huu ni nafasi ya kujithibitisha mbele ya moja ya timu ngumu zaidi kwenye ligi, hasa ikicheza nyumbani Tanga mbele ya mashabiki wao ili kujihakikishia nafasi ya kusalia kwenye ligi.

Historia ya mechi za Ligi Kuu Bara kati ya timu hizi mbili inaonyesha wazi ubabe wa Simba ambao katika michezo 25 walizokutana tangu 2011 ndani ya msimu 13, wameshinda mara 17, sare mara saba huku Coastal Union ikishinda mara moja.

Katika mchezo wa mwisho kwa timu hizo kukutana ambapo ilikuwa Aprili 2, 2026 kwenye mzunguko wa kwanza, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 ikiwa nyumbani. Mabao ya Wekundu hao wa Msimbazi yalifungwa na mshambuliaji, Seleman Mwalimu na beki, Ismael Toure.

Mechi pekee ambayo Coastal Union iliibuka na ushindi dhidi ya Simba ilikuwa Mei 23, 2014, hivyo Wagosi hao wa Kaya watakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha wanaondokana na mfululizo wa matokeo mabovu ambao wamekuwa nao dhidi ya Mnyama.

Takwimu zinaonyesha kuwa Simba imefunga jumla ya mabao 51 dhidi ya Coastal Union tangu 2011 huku ikiruhusu mabao 12 na mechi iliyotoa mabao mengi ilikuwa Mei 8, 2019 ambapo yalifungwa mabao tisa.

Katika mchezo huo ilishuhudiwa Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 8-1 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Mganda Emmanuel Okwi na Meddie Kagera kila mmoja alitupia mabao matatu 'hat-trick', mabao mengine yalifungwa na Clatous Chama na Hassan Dilunga huku bao pekee la Coastal likifungwa na Razin Hafidh ambaye kwa sasa yupo Mtibwa Sugar.

Mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama wakati akipiga mpira wa kona. Picha na Simba


Chama na Coastal

Ni miaka saba sasa tangu Chama kuhusika katika maumivu ya Coastal Union kuchapwa mabao manane kwenye ligi, Wagosi hao wanakutana tena na mwamba huyo wa Lusaka akiwa kwenye kiwango bora.

Chama ndiye mchezaji hatari zaidi kwa sasa kwenye kikosi cha Simba kufuatia kufunga katika michezo mitano mfululizo ya mashindano yote.

Kiungo huyo mshambuliaji ambaye hii ni awamu yake ya pili kuichezea Simba, alianza kuwaka tangu Mei 3, 2026 katika Dabi ya Kariakoo ambapo wekundu wa Msimbazi walitoa sare ya mabao 2-2, alifunga bao ambalo ni gumzo hadi sasa na kutoa asisti moja.

Akiwa amerejea Simba katika dirisha dogo tu la usajili, Januari mwaka huu, akafunga tena dhidi ya JKT Tanzania na kuifanya timu hiyo kuibuka na ushindi wa bao 1-0, kisha akawapigisha kwata maafande wa Tanzania Prisons kwa kufunga na kutoa asisti kwenye ushindi wa mabao 4-0.

Chama alifanya tena balaa dhidi ya Mashujaa kwa kufunga mabao mawili kati ya matatu, matokeo ambayo yaliifanya Simba kupunguza tofauti ya pointi dhidi ya Yanga kutoka tano hadi mbili kabla ya kucheka tena na nyavu katika mechi ya robo fainali ya Kombe la CRDB Confederation dhidi ya TRA United.

Kocha wa Coastal Union, Fikiri Elias alisema wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba huku akisisitiza kuwa lengo lao ni kuwapa upinzani mkubwa ndani ya dakika zote 90 za mchezo.

“Hatutaki kuwa daraja la kumnyanyua yoyote lazima tutafute alama tatu kwa ajili ya timu yetu na kujiweka kwenye nafasi nzuri zaidi,” alisema kocha huyo.

Aidha kocha huyo alisema kila mchezo una umuhimu na ladha yake tofauti, hivyo wamefanya maandalizi ya kutosha kwa heshima ya mpinzani wao huku akidai wataingia uwanjani kwa tahadhari na nidhamu kubwa.

Kwa upande wa kocha wa Simba, Steve Barker alisema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo muhimu dhidi ya Coastal Union huku akisisitiza umuhimu wa kupata matokeo chanya ili kuendelea kuwa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Barker alisema wanautambua ubora wa Coastal Union na ushindani uliopo kwenye Ligi Kuu lakini wamefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo.

“Kila mchezo kwetu ni muhimu katika kipindi hiki cha msimu. Tunahitaji kucheza kwa nidhamu, umakini na kutumia nafasi zetu vizuri ili kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema.

Barker alisema benchi lake la ufundi limejikita zaidi katika kuwaweka wachezaji kwenye hali nzuri ya ushindani na kuhakikisha timu inaingia uwanjani ikiwa tayari kupambana kwa ajili ya wanasimba.


JKT Vs Fountain Gate

Kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Dar, wenyeji JKT Tanzania waliopo nafasi ya tano kabla ya mechi za jana na pointi zake 36, ina kazi ya kuikaribisha Fountain Gate yenye pointi 25 katika nafasi ya 11.

Tofauti chache ya pointi kwa timu hizo kwenye msimamo dhidi ya timu zingine, inaufanya mchezo huu kuwa na ushindani kwani kila moja inahitaji kujiweka pazuri zaidi.

Novemba 30, 2025, ilishuhudiwa Fountain Gate ikiwa nyumbani ikifungwa 2-0 na JKT Tanzania, hivyo itaingia uwanjani ikitaka kulipa kisasi na kujitoa kwenye hatari ya kushuka daraja.

Safari hii, Kocha Fred Felix Minziro anaiongoza Fountain Gate tofauti na mwanzo alikuwepo Mohamed Ismail 'Laizer', lakini JKT Tanzania wanaye yuleyule Ahmed Ally.

Akizungumzia mechi hiyo, Minziro, alisema: “Tumewaandaa vijana kulingana na aina ya mpinzani, JKT ni kati ya timu bora, lakini tumejipanga kupambana hadi mwisho kusaka alama tatu.”


Namungo Vs Mbeya City

Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, utashuhudiwa mchezo wa mwisho kwa leo ambapo zinakutana timu zilizopishana nafasi moja kwenye msimamo.

Namungo ambayo ni mwenyeji, ina pointi 24 katika nafasi ya 13, ni mwenyeji wa Mbeya City iliyokusanya pointi 21 ikishika nafasi ya 14, tofauti ya pointi tatu pia inaufanya mchezo huu kuwa na mvuto wa aina yake.

Juma Mgunda anayeinoa Namungo, ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha anavunja rekodi mbovu ya timu hiyo iliyonayo kwani tangu Januari 31, 2026 iliposhinda 1-0 dhidi ya KMC, haijashinda tena kwenye ligi ikicheza mechi 13, imeambulia sare sita na vichapo saba.

Mbeya City nayo haina mwendo mzuri, ikiwa inafundishwa na Salum Mayanga, kocha aliyeletwa kwa ajili ya kuinusuru na janga la kushuka daraja, amepoteza mechi mbili mfululizo zilizopita dhidi ya JKT Tanzania (1-0) na Coastal Union (2-0).

Mayanga amezungumzia mchezo huo akisema: "Hatuna kikubwa zaidi ya kuja Ruangwa kuhakikisha tunapata alama tatu hii ni kutokana na nafasi tuliyopo kwenye msimamo wa ligi."