Klopp acharuka kuhusishwa kujiunga Real Madrid
Kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Klopp amesisitiza kuwa hana mpango wa kurejea kufundisha kwa sasa.
Kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp, ameonesha hasira kali kufuatia tetesi zinazoendelea kumhusisha kujiunga na Real Madrid, akizitaja taarifa hizo kuwa ni upuuzi na zisizo na msingi wowote.
Klopp, mwenye umri wa miaka 58, amezungumza hayo katika mkutano na waandishi wa habari nchini Ujerumani baada ya kutangazwa kuwa mchambuzi wa Kombe la Dunia kupitia kituo cha Televisheni cha Magenta, ambapo atashirikiana na wachezaji nyota kama Thomas Muller na Mats Hummels.
Katika mkutano huo, Klopp ameulizwa kuhusu mustakabali wake wa ukocha, ikiwemo uwezekano wa kuinoa timu ya taifa ya Ujerumani, lakini akajibu kwa utulivu akisema kwa sasa hana mpango wowote.
Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla alipoulizwa kuhusu kujiunga na Real Madrid.
Kwa hasira, Klopp alihoji uhalali wa taarifa hizo, akisema, “Ni lini habari inakuwa habari? Ni pale mtu anaandika tu kitu, au pale kuna ukweli ndani yake?”
Amesisitiza kuwa hajawahi kuwasiliana hata mara moja na viongozi wa Real Madrid, akiwemo rais wa klabu hiyo.
Kwa sasa, Klopp anafanya kazi kama mkuu wa masuala ya soka katika kampuni ya Red Bull tangu mwaka jana, akishirikiana na klabu kama RB Leipzig na RB Salzburg. Hata hivyo, amekuwa akihusishwa na tetesi za kuondoka katika nafasi hiyo jambo ambalo amelikanusha.
Klopp amewashambulia waandishi wa habari walioripoti tetesi hizo, akisema baadhi yao hawajui wanachokiandika, na kuongeza kuwa watu wengi wanakimbilia kueneza taarifa bila uthibitisho.
Licha ya ripoti zinazodai kuwa nafasi yake ya sasa huenda haimridhishi kikamilifu, Klopp ameendelea kusisitiza kuwa hana mpango wa kurejea kufundisha kwa sasa, akionyesha kuwa anafurahia majukumu yake ya sasa nje ya benchi la ufundi.