Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JICHO LA MWEWE: Kwa Juma Kaseja, labda maandiko yametimia

JICHO Pict

Muktasari:

  • Timu zilikuwa zimetoka mapumzikoni na Kaseja akawakusanya wachezaji wenzake na kuanza kutoa maelekezo. Mwaisabula aliniambia Kaseja alikuwa anamaanisha yote yaliyoongelewa na kocha katika vyumba vya kubadilishia nguo hayakuwa na muhimu zaidi kuliko maelekezo yake.

Rafiki yangu, kocha wa zamani wa Yanga na Bandari Mtwara, Kennedy Mwaisabula 'Mzazi' siku fulani tukiwa tunatazama mechi ya Simba alikuwa akinieleza tabia ambayo makocha wengi wasingeipenda kutoka kwa kipa wa Simba wa wakati huo, Juma Kaseja.

Timu zilikuwa zimetoka mapumzikoni na Kaseja akawakusanya wachezaji wenzake na kuanza kutoa maelekezo. Mwaisabula aliniambia Kaseja alikuwa anamaanisha yote yaliyoongelewa na kocha katika vyumba vya kubadilishia nguo hayakuwa na muhimu zaidi kuliko maelekezo yake.

Hata wakati pambano linaendelea inapotokea fursa ya mwamuzi kusimamisha pambano kwa sababu ya majeraha ya mchezaji, Kaseja angekusanya kundi kubwa la wachezaji na kuanza kutoa maelekezo ya nini kinapaswa kufanyika.

Ni nadra kukutana na wachezaji wa namna hii. Mara nyingi wachezaji wanakimbilia katika benchi kwenda kusikiliza maelekezo ya ghafla ya kocha na si ya mchezaji mwenzao. Kaseja alikuwa na uwezo huu wa kuwakusanya wenzake wamsikilize.

Nimemkumbuka Mwaisabula baada ya Kaseja kutangazwa kuwa kocha mpya wa Kagera Sugar hivi karibuni na tayari kaiongoza katika mechi mbili na zote kashinda, moja ya Ligi Kuu Bara na nyingine na Kombe la Shirikisho.

JIC 01

Nahisi maandiko yametimia. Juma, hodari langoni kama alivyo, alikuwa anapenda kutoa maelekezo kwa wachezaji wake na sasa amepewa jukumu rasmi.

Angetoa maelekezo kila wakati kwa mabeki wake, baadaye angehamia kwa viungo na wachezaji wa mbele. Kwa Juma kuwa kocha labda maandiko yametimia. Hadi leo wachezaji wa aina yake huwa tunawaita viongozi wa uwanjani.

Mara nyingi inatokea zaidi kwa makipa au walinzi wa kati au viungo. Hawa huwa wanautazama uwanja kwa mapana yake. Takwimu zinaonyesha ni washambuliaji wachache walioweza kuwa makocha wazuri.

Diego Maradona hakuwa kocha mzuri. Pele hakujaribu kazi yenyewe. Ronaldo di Lima hakujaribu kazi yenyewe. Ronaldinho Gaucho hakujaribu kazi yenyewe na ameishia kutangatanga sehemu za starehe na warembo.

JIC 05

Hawa kina Mauricio Pochettino, Mikel Arteta, Pep Guardiola, Diego Simeone, Xabi Alonso na wengineo wengi walikuwa viungo.  Makipa pia wanautazama mpira kwa mapana yake na sasa mikononi mwetu tuna kocha mpya, Juma Kaseja.

Kile ambacho Juma alikuwa anawavuruga kina Mwaisabula kwa kwenda kutoa maelekezo mengine baada ya wao kutoa yao sasa hivi inabidi akifanye mwenyewe. Wazee wa zamani wanasema mchawi mpe mwanao amtunze.

Inamaanisha nini Kaseja kupewa Kagera Sugar? Kwanza kabisa nadhani maandiko yametimia. Wakati ule anacheza soka nilikuwa najua Kaseja angeweza kuwa kocha mzuri siku za usoni. Namna ambavyo alikuwa anatoa maelekezo kwa wachezaji wenzake, lilikuwa jambo la muda tu kuwa kocha.

JIC 02

Jambo jingine ni huenda kazi hii ya ukocha ikahitimisha ndoto za Kaseja kucheza soka. Tangu namfahamu hadi leo sijawahi kuona mchezaji anapenda kucheza soka kama Kaseja. Anapenda mazoezi, anapenda mechi.

Kaseja ni kama Cristiano Ronaldo wa langoni. Hamu ya mpira haijawahi kumuisha. Kaseja ninayemfahamu hajawahi kutangaza kustaafu. Kaseja ninayemfahamu hata leo angependa kuwa katika lango la Kagera Sugar badala ya kukaa katika benchi. Labda kuwa kocha mkuu kunahitimisha rasmi safari yake ya kucheza soka.

Kwa sasa majukumu yake yatakuwa mengi. Atalazimika kuandaa timu yake na mambo mengine. Nadhani huu ndiyo utakuwa mwisho wa ndoto zake za kuendelea kucheza soka tena na tena. Labda Kelvin Yondani tu ndiye mchezaji ambaye atakuwa amecheza ligi yetu kwa muda mrefu kando ya Kaseja.

JIC 04

Kaseja kuwa kocha pia kunamaanisha anakuwa mchezaji mwingine wa kikosi cha Simba cha mwaka 2003 ambacho kiliitoa Zamalek pale Misri na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Wachache walipata bahati ya kuwa makocha. Amri Saidi, Ulimboka Mwakingwe, Boniface Pawasa na Suleiman Matola ndio wachezaji ambao kwa haraka haraka nimewakumbuka walikuwa makocha baada ya kucheza soka maridadi usiku ule wa kukumbukwa. Sio kila mchezaji mahiri wa zamani anaweza kubadilisha kazi na kuja kuwa kocha.

Na sasa linakuja swali jingine. Ataweza kuwa kocha mahiri? Hili ni jambo jingine na hii ni kazi nyingine. Akiwa amepita katika mikono ya makocha wengi wazungu, Kaseje labda anaweza kuja na kitu tofauti kama kocha. Akiwa na maono mengi kama mchezaji wakati huo labda sasa anaweza kuja na kitu tofauti.

Kuwa kipa mahiri ni jambo moja. Kuwa kipa anayeweza kutoa maelekezo ni jambo jingine. Lakini kuwa kocha kunamaanisha kuna mambo mengi ndani yake. Namna ya kuiandaa timu. Namna ya kusajili wachezaji. Namna ya kudhibiti nidhamu za wachezaji. Namna ya kuwasiliana na wachezaji ni jambo muhimu pia.

JIC 03

Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia namna wachezaji mahiri wa zamani wanavyoshindwa kuwasiliana na wachezaji. Mara nyingi huwa wanaamini wachezaji wanaweza kufanya kama kile ambacho wao walikuwa wanafanya zamani.

Mifano mingi ya makocha ambao walikuwa wachezaji mahiri huwa wanajizungumzia zaidi wao walivyokuwa wanafanya au wachezaji wenzao wa zamani walivyokuwa wanafanya kuliko kutoa maelezo ya kile kinachohitajika leo.

Huwa inasemwa pia hii ndiyo sababu  hata wachezaji wengi mahiri wa zamani ndani na nje ya nchi kushindwa kuwa wachambuzi. Badala ya kuelezea kile ambacho kinapaswa kufanyika leo wao huwa wanalezea mambo ambayo walikuwa wanafanya zamani.

Kila la kheri kwa Kaseja. Wakati huu tukiwa tumeanza kupiga chapuo kwa makocha wazawa kupewa nafasi katika timu ya taifa na pia klabu za Simba na Yanga, Kaseja anapaswa kuthibitisha ubora wa makocha wazawa kwa namna ambavyo atakisuka kikosi cha Kagera Sugar.