Historia mpya Serengeti Boys ikitinga nusu Fainali AFCON U17
Muktasari:
- Serengeti Boys ni miongoni mwa timu 10 zitakazoiwakilisha Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 zitakazofanyika mwishoni mwa mwaka huu huko Qatar.
Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imeingia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17) baada ya leo Jumapili, Mei 24, 2026 kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 4-3 dhidi ya Algeria katika robo fainali.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa Serengeti Boys kutinga hatua hiyo kwenye Fainali za AFCON kwa vijana wa umri huo.
Serengeti Boys imelazimika kusubiri hadi mikwaju ya penalti iamue ushindi wake baada ya dakika 90 za mechi hiyo kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Penalti nne za Serengeti Boys jana zimefungwa na Razaki Mbegelendi, Elick Yusuph, Luqman Mbalasalu na Hassan Kizinga wakati kwa upande wa Algeria, waliofunga penalti zao ni Ilyes Mekkaoui, Khalil Touali na Dahmas Ayoub huku Noam Benramdane na Mouhammad Valmy wakikosa.
Katika dakika 90 za kawaida za mchezo, Algeria ndio imekuwa ya kwanza kufunga bao kupitia kwa Mouhammad Valmy katika dakika ya nne kabla ya Serengeti Boys kusawazisha katika dakika ya 25 kwa bao la Athanas Dismas..
Valmy aliitanguliza tena Algeria baada ya kuifungia bao la pili katika dakika ya 40 na wakati timu hizo zinajiandaa kwenda Mapumziko, Luqman Mbalasalu akairudisha mchezoni Serengeti Boys kwa kuisawazishia.
Dakika 16 baada ya kipindi cha pili kuanza, Athanas aliitanguliza Serengeti Boys kwa kuifungia bao la tatu ambalo lilidumu kwa dakika nne tu kwani Algeria ilisawazisha katika dakika ya 65 kupitia kwa Noam Benramdane.
Pamoja na matokeo ya leo, Serengeti Boys ina uhakika wa kushiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Qatar, mwishoni mwa mwaka huu.
Serengeti Boys ilikata tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia mara baada ya kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ya AFCON U17.
Katika mechi ya leo, kikosi kilichoanza cha Serengeti Boys kiliundwa na Haji Abdalah, Elick Yusuph, Idrisa Kilendemo, Kassim Juma, Hussein Mbegu, Issa Cholle, Hamis Mihambo, Sadam Hamis, Athanas Adam, Razaki Mbegelendi na Luqman Mbalasalu.