Haaland atupia mawili, Norway ikifuzu mtoano Kombe la Dunia
Muktasari:
- Haaland sasa amefikisha idadi ya mabao manne sawa na Mbappe wa Ufaransa huku wakitarajiwa kukutana katika mechi ya mwisho ya kundi I.
Mshambuliaji Erling Haaland, ameibeba Norway ikishinda kwa mabao 3-2 dhidi ya Senegal, katika mchezo wake wa pili kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2026.
Norway imekuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza dakika ya 43 likifungwa na beki wa kulia, Marcus Pedersen, akinufaika na makosa ya safu ya ulinzi ya Senegal.
Beki na nahodha wa Senegal, Kalidou Koullibaly, atajilaumu kwenye bao hilo kwa kutoa pasi kwa mfungaji.
Pedersen, amefunga bao hilo akitokea benchi, baada ya Julian Ryerson, kuumia na kutolewa dakika ya 13. Norway ikaenda mapumziko ikiongoza kwa bao 1-0.
Norway ikarudi na moto kipindi cha pili ambapo dakika ya 48, Haaland akaipa timu hiyo bao la pili akitumia asisti ya nahodha wake, Martin Odegaard.
Nahodha wa Norway, Martin Odegaard wakati alipokuwa akijaribu kupiga shuti katika mechi ya kundi I ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Senegal, Juni 23, 2026. Picha na Mtandao
Senegal ikarudi mchezoni ikipata bao la kwanza kupitia mshambuliaji Ismaila Sarr dakika ya 53, akitumia pasi ya Sadio Mane.
Wakati Senegal ikirudi mchezoni, ikajikuta inaruhusu bao la tatu likifungwa na Haaland tena dakika ya 58, akitumia asisti ya kiungo Patrick Berg.
Bao hilo linakuwa la 59 kwa Haaland kwenye timu ya Taifa, akiyafunga ndani ya mechi 52, akizidi kuwa mshambuliaji tishio kwa taifa hilo.
Sarr tena akaipa bao la pili Senegal dakika 90+3 akitumia asisti ya Nicolas Jackson, Senegal ikipambana kulinda heshima yake lakini mpaka mwisho wa mchezo ikajikuta inapoteza kwa mabao 3-2.
Matokeo hayo yanaifanya Norway kushika nafasi ya pili kwenye Kundi I sawa na Ufaransa iliyopo nafasi ya kwanza zote zikifanikiwa kutinga hatua inayofuata ya mtoano kwa kufikisha pointi sita.
Kwa upande wa Senegal, italazimika kuifunga Iraq katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ili kuangalia uwezekano wa kufuzu hatua ya mtoano.
Kwa mujibu wa mashindano hayo yenye makundi 12, timu mbili za juu kila kundi zitafuzu moja kwa moja hatua ya 32 bora, kisha nane zilizomaliza nafasi ya tatu zikiwa na matokeo bora zaidi, zitaungana nazo kukamilisha idadi.
Kwa sasa msimamo wa timu zinazopambania kufuzu mtoano kwa kuangalia ubora wao wa kuwepo nafasi ya tatu, Senegal ipo ya 12. Juu yake kuna Sweden, Scotland na Paraguay kila moja ikiwa na pointi tatu, kisha Cape Verde na Ubelgiji zenye mbili, huku Ureno, Czech, Ecuador na Bosnia & Herzegovina nazo zina pointi moja. Panama, Jordan, kisha Senegal zinafuatia hazina kitu.
Ureno, Panama na Jordan, zina nafasi ya kujiweka pazuri zaidi pengine kutoka kabisa katika eneo hilo kwani zina mechi mbili za kucheza huku zingine katika orodha hiyo zikibakiwa na moja.