Aucho, Mukwala waitwa ghafla Uganda, wajisalimisha mapema
Muktasari:
Septemba 5, 2025, Uganda itacheza na Msumbiji katika mchezo wa kundi G la mashindano ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Siku tatu baada ya timu ya Taifa ya Uganda kutangaza kikosi chake kwa ajili ya mechi mbili za kuwania kufuzu Kombe la Dunia huku Khalid Aucho na Steven Mukwala wakiwekwa kando, nyota hao wawili leo Jumamosi, Agosti 30, 2025 wamerudishwa ghafla kikosini.
Aucho anayeitumikia Singida Black Stars na Mukwala aliyepo Simba, waliwekwa kando na Kocha Mkuu wa Uganda, Paul Put katika kikosi chake cha nyota 28 alichokiita awali kwa ajili ya mechi mbili dhidi ya Msumbiji na Somalia mapema mwezi ujao.
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) leo Jumamosi, Agosti 30, 2025 imesema kuwa wawili hao wameongezwa kikosini.
“Aucho, Mukwala ndani: Kikosi cha Uganda Cranes kitaanza kukusanyika kesho katika Hoteli ya FUFA Kisaasi kikiongozwa na wachezaji 11 wa CHAN.
“Walioongezwa karibuni, Nahodha Khalid Aucho na Steven Mukwala wanategemewa kujiunga na timu Jumatatu, Septemba Mosi 2025 kufanya namba ya jumla iwe 30,” imefafanua taarifa ya FUFA.
Kikosi hicho cha Uganda kinajiandaa na mechi mbili za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 ambazo itacheza dhidi ya Msumbiji, Septemba 5 na dhidi ya Somalia, Septemba 8.
Wachezaji 30 wanaounda kikosi cha Uganda ni Denis Onyango, Salim Magoola, Nafian Alionzi, Joel Mutakubwa, Elvis Bwomono, Herbert Bockhorn, Elio Capradossi, Rogers Torach, Toby Sibbick na Hilary Mukundane.
Wengine ni Jordan Obita, Aziz Kayondo, Herbert Achayi, Gavin Kizito, Ronald Ssekiganda, Kenneth Semakula, Joel Sserunjogi, Khalid Aucho, Abdul Karim Watambala na Travis Mutyaba.
Wapo pia Steven Mukwala, Denis Omedi, Allan Okello, Joseph Mpande, Rogers Mato, Reagan Mpande, Jude Ssemugabi, John Dembe, Patrick Kakande na Uchechukwu Ikpeazu.