Prime
Aucho ajiandaa kutimka Yanga
Muktasari:
- Hata hivyo, mambo yamebadilika fasta, baada ya kushindwa kukubaliana juu ya dau la usajili kubadilika kutoka upande wa kiungo huyo.
Mashabiki wa Yanga wanajua kwamba wapo mastaa wataachana na timu hiyo mwisho wa msimu huu lakini kama kuna jina limewashtua ni mido Khalid Aucho kuwa katika hatua za mwisho kuikimbia klabu hiyo.
Aucho ambaye Yanga ilimtambulisha rasmi Agosti 9, 2021 kuwa kiungo wao mpya akitokea Misr Lel Makkasa SC ya Misri, amekuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya ubingwa na makali ya kikosi cha timu hiyo.
Taarifa za uhakika ambazo Mwananchi imezipata ni kwamba, awali kiungo huyo alikuwa ameshakubaliana kila kitu na uongozi wa Yanga kwamba atasaini mkataba wa mwaka mmoja kusalia ndani ya timu hiyo.
Hata hivyo, mambo yamebadilika fasta, baada ya kushindwa kukubaliana juu ya dau la usajili kubadilika kutoka upande wa kiungo huyo.
Mabadiliko hayo yalitokana na ofa mbili ambazo kiungo huyo amezipokea ndani ya wiki chache tangu arudi kwao Uganda kwa mapumziko.
Ingawa Aucho ameshindwa kujibu taarifa hizo lakini Mwananchi linafahamu kwamba, kiungo huyo alipewa ofa ya Dola 45,000 (Sh117.5 milioni za Kitanzania) kwenda Vietnam lakini pia Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ilikuwa inampigia hesabu.
Aucho ambaye ni raia wa Uganda, alitaka Yanga impe Dola 35,000 (Sh91.4 milioni) hadi 40,000 (Sh104.4 milioni) ili aweze kubaki hatua ambayo iliwalazimu mabosi wa klabu hiyo kuomba muda wafikirie zaidi.
Yanga wasiwasi wao ulikuwa ni gharama hizo kubwa lakini pia namna kiungo huyo alivyotumika msimu uliopita, akikosa baadhi ya mechi kutokana na majeraha.
Msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara, Aucho alicheza mechi 22, akitumia dakika 1735 uwanjani, akifanikiwa kufunga bao moja alilowafunga Mashujaa kwao, katika ushindi wa mabao 5-0 na kutoa asisti moja.
Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Yanga ilianzia hatua ya awali na kuishia makundi ikicheza jumla ya mechi nane, Aucho alicheza mechi sita kwa dakika 525 akiwa hajafunga wala kuasisti.
Mabosi wa klabu hiyo wakaenda mbali zaidi wakiona hata hatua ya wao kuingia sokoni kutafuta kiungo mkabaji shoka kama Moussa Bala Conte wanayeipigania saini yake ni kutokana na wasiwasi wa matumizi ya uhakika ya Aucho.
"Unapofanya maamuzi makubwa ya mbele lazima uangalie ni nani unampa fedha kama hizo, sote tunafahamu kwamba Aucho kama yuko sawa ni kiungo wa kazi hasa lakini kwasasa uhakika huo ni vigumu kuupata tukiangalia tu msimu uliomalizika,"alisema bosi huyo wa juu.
"Kwahiyo uwezekano wa kubaki ni mdogo sana, ni ngumu kukubali kuimuachia lakini kuna wakati unalazimika kukabiliana na changamoto mpya, tutapata watu wengine bora.
Inaelezwa Aucho alikerwa na hatua ya Yanga kuwa kimya baada ya kuomba muda wa kutafakari ofa ambayo aliwapa kupitia mazungumzo ya mwisho.
Mwananchi linafahamu kwamba kufuatia ukimya huo wa mabosi wa Yanga, Aucho amewasilisha maombi ya kupewa barua ya kuachwa huru baada ya mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu huu.
Katika kipindi cha misimu minne ambayo Aucho ameitumikia Yanga, amekuwa mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza huku akichangia mafanikio makubwa iliyopata klabu hiyo katika kushinda mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA katika misimu ya 2021–2022, 2022–2023, 2023–2024 na 2024–2025. Pia mataji matatu ya Ngao ya Jamii (2021, 2022 na 2024).
Msimu wa 2022-2023, Aucho alikuwa mchezaji muhimu wa kikosi cha Yanga kilichocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria, na kupoteza fursa ya kutwaa ubingwa licha ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2, lakini sheria ya bao la ugenini iliwahukumu kufuatia Yanga nyumbani kufungwa 1-2 na ugenini kushinda 0-1.