Algeria yafuzu Kombe la Dunia, Uganda yanyemelea mchujo
Muktasari:
- Algeria itacheza na Uganda, Jumanne, Oktoba 14, 2025 katika mechi ya mwisho ya kundi G la mashindano ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Algeria imekuwa timu ya nne barani Afrika kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya leo Alhamisi, Oktoba 9, kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Somalia.
Matokeo hayo kwenye mechi hiyo iliyochezwa katika Uwanja wa Miloud Hadef, Oran, yameifanya Algeria kufikisha pointi 22 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote kwenye kundi G.
Mashujaa wa Algeria katika mechi hiyo ni Mohamed Amoura aliyefunga mabao mawili na lingine moja likipachikwa na Ryad Mahrez.
Kwa kufuzu huko, Algeria itashiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya tano baada ya kufanya hivyo 1982, 1986, 2010 na 2014.
Mafanikio makubwa ya Algeria kwenye Kombe la Dunia ni kufika hatua ya 16 bora katika fainali za mwaka 2014 zilizofanyika Brazil.
Wakati Algeria ikifuzu, Uganda imejitengenezea mazingira mazuri ya kucheza mechi za mchujo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Botswana.
Bao la Jude Ssemugabi limeifanya Uganda kufikisha pointi 18 na hivyo kujihakikishia kumaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi G.
Uganda sasa itatakiwa kupata ushindi katika mchezo wa mwisho ugenini dhidi ya Algeria ione kama itamaliza ikiwa miongoni mwa timu nne zenye matokeo mazuri zaidi katika hatua ya makundi.
Timu nne za Afrika tayari zimeshajihakikishia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia 2026 ambazo ni Morocco, Tunisia, Misri na Algeria.